Alkhamisi, 16 Aprili, 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Shaabani 1441 Hijria sawa na Aprii 16 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 853 iliyopita alifariki dunia Ibn Shahr Ashub, alimu na mtaalamu mkubwa wa elimu ya hadithi. Muhammad Bin Ali Ibn Shahr Ashub alizaliwa katika mji wa Mazandaran nchini Iran na kupewa jina la Ibn Shahr Ashub kama ambavyo pia alipewa lakabu ya 'Zainud-Din na Rashidud-Din,' ambapo alitambuliwa kuwa na upeo wa juu wa elimu ya theolojia, hatibu, mtaalamu wa elimu ya fasihi na kadhi mashuhuri wa Waislamu wa Kishia. Kutokana na masuala ya kimadh'hab, Ibn Shahr Ashub alilazimika kuondoka Iran katika kipindi cha utawala wa Maseljuq na kukimbilia mjini Aleppo, Syria ya leo. Aliheshimiwa sana na hata wasomi wakubwa wa Kisuni wa zama zake. Ibn Shahr Ashub alipewa idhini ya kupokeza hadithi na maulama wakubwa wa zama zake kama vile Zamakhshari, Imam Muhammad Ghazali na Khatwib Khawarazmi. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Maalimul-Ulamaa' 'Manaaqib Aali Abi Twalib' 'Mutashaabihul-Qur'an' na 'Al-Arbaiin.'

Siku kama ya leo miaka 668 iliyopita Ibn Hajar Asqalani, faqih, mwanahadithi, mwanahistoria na mshairi Mwislamu wa Misri alizaliwa mjini Cairo Misri. Alimpoteza baba yake mzazi alipokuwa na umri wa miaka mitano tu na katika umri huo akaanza kujifunza Qur'ani Tukufu pamoja na masomo mengine ya kidini. Kufikia miaka 10 alikuwa amehifadhi Qur'ani nzima na alisafiri katika nchi tofauti kwa lego la kupata masomo ya juu. Alionyesha kipawa na ujuzi mkubwa katika taaluma ya hadithi kiasi kwamba alifahamika kwa jina la Muhifadhi Mkubwa wa Hadithi. Ibn Hajar Asqalani anahesabiwa kuwa mmoja wa waandishi mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa kadiri kwamba ameandika vitabu vinavyopata 150. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Lisaan al-Mizaan, Fat'h al-Bari fii Sharh Hadith al-Bukhari na al-Ishara fii Tamyiz as-Swahaba. Ibn Hajar al-Asqalani aliaga dunia mwaka 852 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita, alizaliwa mjini Paris, Anatole France, mwandishi na malenga wa Kifaransa. Tangu akiwa kijana alivutiwa na elimu ya fasihi na uandishi ambapo kutokana na kipawa alichokuwanacho akatokea kupata umashuhuri katika uga wa mashairi na fasihi. Anatole France ameacha athari mbalimbali kikiwemo kitabu kinachoitwa 'Mfalme wa Sabai.' Mwaka 1914 Anatole France alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na kuandika kitabu alichokipa jina la 'Uasi wa Malaika' huku akifariki dunia mwaka 1924.

Miaka 131 iliyopita, Charles Spencer Chaplin mcheza filamu na msanii mashuhuri wa tasnia ya filamu alizaliwa katika viunga vya mji wa London Uingereza. Alipokuwa mdogo, alianza na michezo ya kuigiza na kupata umashuhuri hatua kwa hatua. Mwanzoni mwa ujana wake, Chaplin alielekea nchini Marekani kwa lengo la kutengeneza filamu. Lakini kutokana na kutengeneza filamu ya ukosoaji na yenye kuonyesha mshikamano wake na matabaka ya kimasikini katika jamii ya Marekani, serikali ya nchi hiyo ilitoa amri ya kubaidishwa kwake mnamo mwaka 1952. Chaplin alikumbana na mazingira magumu ya kufanya shughuli zake nchini Marekani na hivyo akahamia nchini Uswisi pamoja na mkewe. Msanii huyo katika tasnia ya filamu alifariki dunia mwaka 1977.

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita alifariki dunia Allamah Sheikh Muhammad Jawad Balaghi, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Katika zama zake alikuwa mtaalamu wa elimu ya fiqhi, mwalimu na mwandishi mkubwa. Allamah Balaghi alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama zake kama vile Mirza Shirazi na kutokea kuwa mmoja wa walimu na waandishi wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Al Balaghul-Mubin' kinachothibitisha uwepo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo Wazayuni waliokuwa na silaha walishambulia kambi ya zamani wa askari wa Uingereza huko Palestina na kuua Wapalestina 90 na kujeruhi wengine wengi. Kwa upande mmoja, maafa hayo yalitokea wakati askari wa Uingereza walipokuwa wakiondoka katika kambi hiyo na kurejea nchini kwao; na kwa upande wa pili, Wazayuni walikuwa wameshadidisha mauaji hayo ya Wapalestina wasio na hatia kwa lengo la kuasisi dola haramu la Israel. Matokeo ya mauaji hayo yaliyofanyika kwa uratibu wa Uingereza, ilikuwa kuuawa idadi kubwa zaidi ya Waislamu wa Palestina na kutangazwa dola bandia la Israel mwezi mmoja baadaye.

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita ulitokea mlipuko mkubwa ulisababishwa na mtungi wa gesi na kusambaza moto kwenye mahema ya Mahujaji huko Mina kilomita 10 kutoka katika mji wa mtakatifu wa Makka. Mahujaji wasiopungua 343 walifariki dunia na wengine 1,290 kujeruhiwa katika tukio hilo. Aidha mahema yasiyopungua elfu sabini yaliteketea kwa moto huo. Hilo linahesabiwa kuwa tukio kubwa la pili la janga la moto kutokea wakati wa msimu wa Hija. Mnamo mwaka 1975, ulitokea moto mkubwa huko Mina nchini Saudi Arabia uliosababisha vifo vya maelfu ya Mahujaji na wengine wengi kujeruhiwa. Kutokana na matukio hayo, Saudi Arabia ililazimika kuweka katika eneo la Mina, mahema yasiyoshika moto ili kuepusha ajali za moto.
