Apr 23, 2020 02:43 UTC
  • Alkhamisi tarehe 23 Aprili mwaka 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Shaabani 1441 Hijria sawa na Aprili 23 mwaka 2020.

Katika siku kama hii ya leo miaka 1123 iliyopita alifariki dunia Ibn Mundhir faqihi, mfasiri na mpokeaji hadithi wa Kiislamu. Ibn Mundhir alijifunza masomo ya fiqih na hadithi kwa wasomi watajika wa zama zake. Ibn Mundhir aliishi katika mji wa Makka hadi mwisho wa maisha yake baada ya kuwasili mjini humo kwa lengo la kuzidisha elimu na maarifa ya kidini. Msomi huyo wa Kiislamu aliandika vitabu kadhaa akiwa Makka. Kitabu alichokipa jina la al Ashraaf ni miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ambacho ndani yake ameonyesha umahiri wake mkubwa katika taaluma ya Hadithi.

Katika siku kama ya leo miaka 404 iliyopita, aliaga dunia William Shakespeare, mshairi na mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Uingereza. Shakespeare alianza kazi zake za usanii sambamba na kushiriki katika michezo ya kuigiza. Alipata umashuhuri mkubwa katika taaluma hiyo. Kazi zake za kisanii zilikuwa mchanganyiko wa sanaa iliyoakisi majonzi na vichekesho. Miongoni mwa kazi maarufu zaidi za Shakespeare ni Romeo and Juliet, Hamlet, King Lear na The Merchant of Venice.  

William Shakespeare

Miaka 162 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mwanafizikia Max Plank wa Ujerumani ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hisabati aliyebuni Nadharia ya Kwanta katika elimu ya fizikia. Mwaka 1918 Max Plank alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel kwa kugundua nadharia ya kwanta. Plank ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler, alifanya utafiti mkubwa katika nyanja za mwendojoto (sayansi ya uhusiano wa joto na kazi za mitambo), fizikia nadharia, joto, mnururisho na nuru na kuandika vitabu kadhaa katika medani hiyo.

Max Plank

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 4 Ordibehesht 1319 Hijria Shamsia, ilianzishwa Idara ya Redio nchini Iran na kurushwa matangazo ya moja kwa moja kupitia kituo cha matangazo cha Redio Tehran. Mwanzoni mwa kuanzishwa redio nchini Iran taasisi hiyo kilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Posta, Simu na Telegrafu. Miaka mitano baada ya kuanzishwa kituo cha redio mjini Tehran, hatua kwa hatua huduma hiyo ilipanuliwa katika miji mbalimabali hapa nchini. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu 1979, zilianzishwa redio na televisheni kadhaa, zikiwemo zile za matangazo ya ng'ambo, zinazotangaza kwa kutumia zaidi ya lugha thelathini za dunia.

Redio

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Khordad 1362 Hijria Shamsia, Bi. Nusrat Amin, faqihi na mfasiri mkubwa wa Qurani Tukufu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 97 katika mji wa Esfahan ulioko katikati mwa Iran. Bi. Nusrat Amin alikuwa mwanamke wa kwanza kufikia daraja ya juu ya elimu za fiqhi na usuli ya ijtihadi katika ulimwengu wa Kiislamu. Aliutumia muda wake wote katika kuishughulikia Qurani Tukufu, na alifanikiwa kufasiri juzuu 15 za Qur'ani na kuandika vitabu kadhaa. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ni pamoja na 'al Arbain al Hashimiyyah' na 'al Nafahatur Rahmaniyya'.

Bi. Nusrat Amin

Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Aprili 1992, alifariki dunia Satyajit Ray mwandishi na mtengeneza filamu mashuhuri wa India. Satyajit Ray alizaliwa mwaka 1921, na filamu zake za kijamii ziligusa zaidi hisia za jamii ya wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kupendwa zaidi na wananchi wa India.

Satyajit Ray

Na tarehe 23 Aprili miaka 25 iliyopita Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku hii ya kuwa Siku ya Kimataifa ya Kitabu na Haki za Mwandishi. Lengo la kutangazwa siku hiyo ni kuonesha umuhimu wa kitabu na haki za waandishi wa vitabu, kuhamasisha watu kusoma vitabu, kuwapongeza watu wanaoandika vitabu kwa ajili ya kukuza na kustawisha utamaduni wa jamii ya mwanadamu na vilevile kuunga mkono na kusaidia ustawi wa sekta ya kusambaza vitabu. Utamaduni wa kusoma vitabu umeshamiri zaidi katika dunia ya sasa hususan miongoni mwa tabaka la vijana kutokana na kusambaa zaidi vitabu vya elektroniki kupitia mitandao ya intaneti.

 

Tags