Jul 17, 2020 02:34 UTC
  • Ijumaa, Julai 17, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 25 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na 17 Julai mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita Nabii Muhammad (saw) akiwa na masahaba na Waislamu zaidi ya laki moja aliondoka Madina na kuelekea Makka kwa ajili ya kuzuru Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu ya al Kaaba. Tangu alipohamia mjini Madina, Mtume (saw) alielekea Makka mara tatu kwa ajili ya kuzuru al Kaaba, lakini ni mara mbili tu ndizo alizofanikiwa kutekeleza ibada ya Hija. Katika safari yake ya mwisho ya Hija mtukufu huyo aliwafunza Waislamu namna ya kutekeleza ibada hiyo kwa njia sahihi. Wakati akirejea Madina, Mtume Muhammad (saw) alifika katika eneo la Ghadir Khum na hapo akawakusanya masahaba zake na kwa amri ya Mola wake akamtangaza Imam Ali bin Abi Twalib kuwa Khalifa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake. Hiyo ilikuwa safari ya mwisho ya Hija ya Mtume ambayo ni maarufu kwa jina la Hajjatul Wadaa. Miezi kadhaa baada ya safari hiyo Mtume Mtukufu aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake.

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita Profesa Roger Garaudy, mwanafalsafa na mwanafikra wa Ufaransa alizaliwa huko katika mji wa Marseille. Garaudy alipata shahada ya daraja ya udaktari katika taaluma tatu za masomo ya falsafa, fasihi na utamaduni. Roger Garaudy alifungwa jela katika kambi ya mateka wa kivita wa Ujerumani tangu mwaka 1940 hadi 1943 kutokana na mapambano yake dhidi ya ufashisti wa Adolph Hitler wakati Ufaransa ilipokaliwa kwa mabavu na Ujerumani. Profesa Garaudy alikuwa mwanachama wa chama cha Kikomonisti cha Ufaransa kwa miaka 36 na pia mwanachama wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka 25. Hata hivyo mitazamo ya kikomunisti na kiliberali haikuweza kukata kiu ya kutafuta ukweli ya msomi huyo wa Ufaransa na hatimaye alikubali dini ya tukufu ya Uislamu baada ya kufanya utafiti mkubwa. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 ulikuwa na taathira kubwa katika mitazamo ya Profesa Roger Garaudy.

Profesa Roger Garaudy

Miaka 52 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo chama cha Baath cha Iraq kilichukua hatamu za uongozi kupitia mapinduzi yaliyoongozwa na Ahmad Hassan al Bakr na kumpindua Rais Abdulrahman Aarif. Baada ya kuchukua madaraka chama cha Baath, Saddam Hussein ambaye alikuwa kiongozi nambari mbili wa chama hicho alianza kuwauwa wapinzani wake nchini Iraq na vikosi vya usalama na vya jeshi la nchi hiyo pia vikaanzisha hujuma kali dhidi ya wapinzani wa Kikurdi, wazalendo, wanaharakati wa Kiislamu na hata Wakomonisti.

Ahmad Hassan al Bakr

Siku kama ya leo miaka 32, iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lilizitaka nchi mbili za Iran na Iraq kusitisha vita na kufanya suluhu. Jamhuri ya Kiislamu ilikubali azimio hilo kutokana na baadhi ya vipengele vyake hususan kile kinachohusiana na kuitambulisha Iraq kuwa ndiye mchokozi katika vita hivyo na kuitaka iilipe Iran fidia ya hasara za vita hivyo. Hata hivyo utawala wa Saddam Hussein ambao pia ulikubali azimio hilo la Baraza la Usalama, uliendeleza mashambulizi dhidi ya ardhi ya Iran.

 

Tags