Sep 09, 2020 02:24 UTC
  • Jumatano tarehe 9 Septemba 2020

Jumatano tarehe20 Muharram 1442 Hijria sawa na Septemba 9 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1448 iliyopita kulianza vita maarufu kwa jina la vita vya miaka saba kati ya madola mawili yaliyokuwa na nguvu ya Iran na Roma, baada ya mfalme Justinian wa Roma kuanzisha mashambulizi yaliyokuwa na lengo la kulikalia eneo la magharibi mwa Iran. Baada ya miaka saba ya vita mfalme wa Iran Anushirvan alimshinda mfalme Justinian wa Roma na hivyo mfalme huyo akalazimika kujiuzulu. Baada ya kujiuzulu mfalme Justinian mfalme Tiberius alishika mamlaka ya utawala wa Roma. Vita hivyo vilimalizika mwaka 579 baada ya Waroma kukubali kuilipa Iran gharama inayofikia sarafu za dhahabu elfu 45.

Siku kama hii ya leo miaka 192 iliyopita alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia. Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na katika kipindi hiki ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokupa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadae alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910.

Leo Tolstoy

Miaka 44 iliyopia katika siku kama ya leo, aliaga dunia Mao Zedong kiongozi wa Uchina. Mao Zedong alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake. Mao alikuwa akisisitiza suala la kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo ilipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina.

Mao Zedong

Katika siku kama ya leo miaka41 iliyopita yaani tarehe 19 Shahrivar aliaga dunia Sayyid Mahmoud Talaqani kiongozi wa kidini, mwanaharakati, mwanamapambano na mfasiri wa Qur'ani Tukufu wa Iran. Ayatullah Talaqani alikuwa akifuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa ya Iran tangu akiwa kijana. Kipindi fulani alitiwa nguvuni na kufungwa jela miaka miwili na utawala wa Kitaghuti wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini kwa kosa la kushiriki katika harakati ya wananchi ya tarehe 15 Khordad. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Imam wa Swala ya Ijumaa ya Tehran.

Sayyid Mahmoud Talaqani

Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita Ahmad Shah Massoud mmoja wa makamanda wakubwa wa Mujahidina wa Afghanistan ambaye pia aliyekuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali ya mpito ya Rais Burhanuddin Rabani wa Afghanistan, aliuawa. Ahmad Shah Massoud alizaliwa mwaka 1952 na alianza kupigana vita na nchi za kigeni katika milima ya kaskazini mwa Afghanistan sambamba na kuingia madarakani wakomunisti huko Afghanistan na mara baada ya kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na jeshi la Urusi ya zamani mwaka 1979.

Ahmad Shah Massoud

 

Tags