Jumanne tarehe 3 Novemba 2020
Leo ni Jumanne tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 3 Novemba 2020.
Siku kama ya leo miaka 1495 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume na mama yake, Amina binti Wahab, alifariki dunia mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita. Katika kipindi cha mwanzoni mwa ujana wake, Muhammad alikuwa akijitenga na jamii ya kijahilia ya watu wa Makka na kwenda kwenye pango la Hiraa lililoko karibu na mji wa Makka na kuketi huko kwa masaa kadhaa akitafakari katika maumbile ya dunia na kufanya ibada. Alipotimiza umri wa miaka 40, Malaika Jibrilu alimteremkia mtukufu huyo akiwa katika pango hilo na kumpa ujumbe wa Mola Muumba. Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) alikumbana na mashaka mengi katika jitihada zake za kufuta ibada ya masanamu na kueneza imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja.
Siku kama hii ya terehe 17 Rabiul Awwal miaka 1359 iliyopita pia alizaliwa mjukuu wa mtukufu huyo Imam Ja'far Swadiq (as) katika mji mtakatifu wa Madina. Kipindi cha maisha yake kilikuwa zama za kuchanua elimu na maarifa, tafsiri ya Qur'ani na kusambaa elimu mbalimbali. Imam Sadiq (as) alitumia fursa hiyo ambayo ilisadifiana na kuanza kuporomoka utawala wa Bani Umayyah na kuchukua madaraka utawala wa Bani Abbas, kwa ajili ya kueneza maarifa asili ya Kiislamu na kulea kizazi cha wasomi na maulama katika nyanja mbalimbali. Kwa minasaba hii adhimu Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote duniani.
Miaka 64 iliyopita muwafaka na leo, wakati wa kujiri mashambulio ya askari wa utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Misri, wanajeshi wa utawala huo waliuvamia mji wa Khan Yunis katika Ukanda wa Gaza huko Palestina na kuwaua kwa umati wakazi wa mji huo. Baada ya kuukalia kwa mabavu mji huo, askari hao waliwanyonga askari 25 wa Kimisri. Unyama wa askari hao haukuishia hapo, kwani waliishambulia hospitali ya mkoa mjini Khan Yunis na kuwaua kwa umati wauguzi, madaktari na wagonjwa wote waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo. Watu wapatao 275 waliuawa katika mashambulio hayo.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, askari vibaraka wa utawala wa Shah uliokuwa ukitawala Iran waliivamia nyumba ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini mjini Qum na kumtia mbaroni. Baada ya kumhamishia mjini Tehran utawala wa Shah ulimbaidishia Imam Khomeini nchini Uturuki. Utawala wa Shah uliamua kufanya hivyo kutokana na uungaji mkono wa Imam Khomeini kwa harakati za mapambano za wananchi Waislamu wa Iran za kutaka kujitawala, uhuru na kutetea thamani za Kidini. Lengo la kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini lilikuwa kusimamisha mapambano yake na wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala huo kwani utawala wa Shah ulitambua kwamba kuwepo Imam nchini kunapelekea kuamka wananchi dhidi ya utawala huo wa kidikteta.
Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, alifariki dunia Jenerali Jean-Bedel Bokassa mtawala wa Afrika ya Kati. Bokassa alichukua madaraka mwaka 1921 kupitia mapinduzi ya kijeshi, baada ya kuiondoa madarakani serikali ya Rais David Dacko kwa uungaji mkono wa Ufaransa. Katika miaka 14 ya utawala wake, kiongozi huyo alitenda jinai na mauaji mbalimbali na kujilimbikizia mali nyingi.