Jumatatu tarehe 9 Novemba 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 23 Rabiul Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 9 Novemba mwaka 2020.
Siku kama yya leo miaka 1241 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatma Maasuma dada wa Imam Ali bin Mussa al-Ridha AS aliwasili katika mji wa Qum, Iran. Mwakka mmoja baada ya safari ya kubaidishiwa kaka yake huko katika mji wa Marv, Bibi Maasuma alifunga safari kwa ajili ya kwenda kuonana na kaka yake huyo. Baada ya kuiwasili Qum, aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (SAW). Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake Imam Ridha AS, Bibi Fatima Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa. Hii leo haram ya BibI Fatma Maasuma AS mjini Qum ni moja ya maeneo matakatifu ambapo watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu huenda kufanya ziara katika eneo hilo.
Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita, alizaliwa nchini Pakistan Allama Muhammad Iqbal Lahori mwandishi, mwanafikra na malenga mzungumza lugha ya Kifarsi. Baada ya kumaliza masomo yake ya juu, Iqbal Lahori alielekea katika nchi za Ujerumani na Uingereza kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu zaidi katika taaluma ya falsafa. Alianza kusoma mashairi akiwa kijana na shairi lake la kwanza alilipa jina la 'Naleh Yatiim' kwa maana ya kilio cha yatima. Allama Iqbal Lahori alikuwa mwanaharakati pia aliyepambana kwa minajili ya kuikomboa Pakistan kutoka mikononi mwa India. Allamah Muhammad Iqbal alifariki dunia mwaka 1938.
Miaka 102 iliyopita sawa na tarehe Tisa mwezi Novemba mwaka 1918, mfumo wa jamhuri ulitangazwa huko Ujerumani kufuatia kushindwa mara kadhaa jeshi la Unchi hiyo na vikosi vya waitifaki katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kuzuka uasi nchini humo. Matukio hayo yalipelekea kujiuzulu Wilhelm wa Pili mtawala wa mwisho wa kifalme wa nchi hiyo. Siku mbili baadaye mfalme huyo alikimbilia Uholanzi na hivyo utawala wa Kifalme ukawa umehitimishwa nchini Ujerumani. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kufutwa utawala wa kifalme, Friedrich Ebert alishika madaraka ya nchi kama rais wa kwanza wa nchi hiyo.
Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abdul Aziz bin Saud mfalme wa kwanza wa Saudi Arabia na mwasisi wa nchi hiyo. Abdul Aziz bin Saud ambaye ni mwasisi wa utawala wa kifamilia wa Aal Saud nchini Saudi Arabia, alizaliwa tarehe 15 Mei 1880. Mtawala huyo alikuwa kibaraka wa Uingereza na tangu awali alikuwa na tamaa ya kutawala nchini Saudi Arabia hususa katika maeneo matakatifu ya Makka na Madina.
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, Charles de Gaulle mwanajeshi, mwanasiasa mashuhuri na Rais wa zamani wa Ufaransa aliaga dunia.Jenerali Charles André Joseph Marie de Gaulle aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri na shakhsia muhimu wa kijeshi nchini Ufaransa alizaliwa Novemba 22 mwaka 1890 katika mji wa Lille. Mwaka 1940 aliteuliwa kuwa jenerali kijana zaidi katika Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa. Baada ya majeshi ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani katika vita, Charles de Guelle alikimbilia Uingereza na kuongoza harakati za mapambano ya Ufaransa.
Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Will Durant mwandishi na mwanafalsafa mashuhuri wa Marekani. Msomi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 96. Durant alizaliwa katika jimbo la Massachusetts huko Marekani. Alihitimu masomo yake kwa kupata daraja ya uzamivu (PhD) katika taaluma ya falsafa na kuanza kufundisha. Mwaka 1926 Will Durant alifanikiwa kusambaza kitabu chake cha The Story of Philosophy. Baadhi ya vitabu vingine vya Will Durant ni The Age of Faith, The Life of Greece na The Age of Napoleon.
Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, ukuta wa Berlin ambao ulikuwa ukiugawa mji huo katika sehemu mbili za mashariki na magharibi kwa kipindi cha miaka 28 hatimaye ulivunjwa. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa mji huo lilikuwa likidhibitiwa na Urusi ya zamani, huku eneo la magharibi likidhibitiwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Machafuko yaliyotokea mjini Berlin hapo mwaka 1961 na wakazi wa mashariki kukimbilia upande wa magharibi, kulizitia wasiwasi serikali za Urusi ya zamani na Ujerumani mashariki, suala lililozipelekea nchi hizo kujenga ukuta huo ambao baadaye uliokana kuwa nembo ya kuwaganywa Ujerumani. Hata hivyo kuporomoka kwa Urusi ya zamani ambako kuliacha taathira kubwa pia katika tawala za kikomunisti za Ulaya mashariki kulipelekea kuvunjwa ukuta huo wa Berlin hapo mwaka 1989.