Nov 21, 2020 02:33 UTC
  • Jumamosi, Novemba 21, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 5 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe 21 Novemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 237 iliyopita, iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Novemba mwaka 1783, kwa mara ya kwanza katika historia ya jitihada za mwanadamu za kupaa angani, puto lilitumwa angani. Puto hilo lilikuwa limepandwa na watu wawili mmoja akiwa mwanafizikia wa Ufaransa aliyejulikana kwa jina la Pilatre De Rozier. Tangu alipokuwa masomoni De Rozier alikuwa akifikiria kutengeneza wenzo wa kupaa angani na kwa kutengeneza puto hilo mwanafizikia huyo akawa amefanikiwa kuruka angani. ***

De Rozier

 

Miaka 175 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarahe 5 Mfunguuo Saba Rabiul Thani mwaka 1267 Hijiria, gazeti la kwanza la lugha ya Kifarsi lililoitwa 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilianza kuchapishwa mjini Tehran. Gazeti hilo lilianza kuchapishwa wakati wa kutimia mwaka wa tatu wa ufalme wa Nasir al-Din Shah Qajjar, kwa amri ya Kansela Mirza Taqi Khan Amir Kabir. Gazeti hilo lilikuwa likiandika habari za utawala wa wakati huo wa Iran, dunia na makala za kisayansi zilizokuwa zikitafsiriwa kutoka kwenye magazeti ya Ulaya. Gazeti la 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilichapisha hadi toleo nambari 472 na baada ya hapo liliendelea kuchapishwa kwa majina tofauti. ***

Gazeti la kwanza la lugha ya Kifarsi lililoitwa 'Waqai'e Itifaqiyeh'

 

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Butros Butros Ghali alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa. Butros Ghali alizaliwa mwaka 1922 katika familia ya Kikristo katika mji mkuu wa Misri, Cairo. Baada ya kumaliza masomo yake Butros Butros Ghali alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Siasa cha Cairo. Mwanadiplomasia huyo ndiye aliyemshawishi na kumshajiisha Anwar Sadat Rais wa zamani wa Misri kutia saini mkataba wa Camp David mwaka 1978 na katika kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel. ***

Butros Butros Ghali

 

Katika siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, inayosadifiana na 21 Novemba 1995, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Makubaliano ya Amani ya Dayton", yalitiwa saini. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na Waserbia. Zaidi ya Waislamu laki moja waliuawa kwa umati katika vita vya Bosnia. ***

Mauaji ya umati ya waserbia huko Srebrenica

 

Na katika siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza na kuiainisha siku hii ya tarehe 21 Novemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Televisheni. Lengo la Umoja wa Mataifa la kuianisha siku hii lilikuwa ni kuweko mabadilishano ya vipindi vya runinga hususan vipindi vinavyotayarishwa kwa lengo la kueneza amani, ustawi wa kijamii na kiuchumi na kuimarisha masuala ya kiutamaduni katika jamii. ***

Siku ya Kimataifa ya Televisheni

 

Tags