Dec 15, 2020 08:27 UTC
  • Jumanne Disemba 15, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 29 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 15 Desemba 2020 Miladia.

Katika siku kama ya leo Miaka 769 iliyopita alizaliwa Muhammad bin Ahmad Dhahabi, anayejulikana kwa lakabu ya Shamsuddin, mpokeaji wa hadithi na mwanahistoria mashuhuri wa zama hizo. Dhahabi alikuwa akipenda sana kukusanya hadithi na alifanya safari nyingi katika pembe mbalimbali duniani ili kukamilisha elimu hiyo. Muhammad bin Ahmad Dhahabi alisimuliwa hadithi nyingi sana kutoka kwa wazee na maulamaa katika safari zake hizo. Dhahabi alifuatilia matukio ya historia ya Uislamu na watu mashuhuri wa kuanzia wakati wa kudhihiri Uislamu hadi mwaka 704 na kuandika habari na matukuio ya wataalamu wa hadithi wa zama hizo. Matukio hayo aliyakusanya katika kitabu alichokipa jina la Historia ya Uislamu. Vitabu vingine vya msomi huyo ni pamoja na Tabaqatul Qurraa, al Muujamul Saghiir na al Muujamul Kabiir.

 

Katika siku kama ya leo miaka 188 iliyopita alizaliwa Alexandre Gustave Eiffel mhandisi na msanifu wa mnara mashuhuri wa Eiffel. Umashuhuri wa Alexandre Gustave unatokana zaidi na usanifu na uhandisi wake wa mnara wa Eiffel mjini Paris ulioanza kujengwa tarehe Mosi Julai 1887 chini ya usimamizi wake. Mnara wa Eiffel una urefu wa mita 324 ambapo katika zama zake ulikuwa mnara mrefu zaidi duniani. Alexandre Gustave Eiffel aliaga dunia tarehe 27 Desemba 1923 akiwa na umri wa miaka 91.

 Alexandre Gustave Eiffel

 

Siku kama ya leo miaka 168 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa Henri Becquerel. Becquerel ambaye alivumbua mnunurisho au miale ya Radioactive baada ya kufanya utafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo. Alianza kufanya jitihada za kupata vitu vinavyotoa miale ya X baada ya miale hiyo kugunduliwa na mwanafizikia wa Kijerumani, Wilhelm Conrad Röntgen tarehe 8 November 1895. Mwaka 1896 Becquerel aligundua mnunurisho  unaoweza kuzalisha miale ya X. Utafiti wa mwanafikizia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tuzo ya Nobel mwaka 1903. Msomi huyo alifariki dunia mwaka 1908.

Henri Becquerel

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, alifariki dunia Walt Disney shakhsia mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto. Disney alizaliwa mwaka 1901 huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya uzamifu katika taaluma ya uchoraji na uchongaji (Fine Art). Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni.

 

Na siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, yaani sawa na tarehe 15 Disemba 1975, zilimalizika zama za udhibiti na ushawishi wa Uhispania huko Sahara ya Magharibi baada ya nchi hiyo kulazimika kuondoka katika eneo hilo. Polisario ni moja ya harakati za ukombozi wa Sahara Magharibi zilizowalazimisha Wahispania kukimbia eneo hilo. Harakati hiyo iliundwa mwaka 1973 baada ya wanamapinduzi wa Sahara kuasisi makundi kadhaa ya kupigania ukombozi wa eneo hilo.

Bendera ya Sahara Magharibi

 

Katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita kanali ya televisheni ya Sahar ya Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha Shirika la Redio na Televisheni la Iran ilianza kazi zake kwa kurusha matangazo ya lugha za Kiarabu, Kiazari, Kibosnia, Kituruki, Kifaransa, Kiingereza na Kiurdu. Televisheni za kanali hiyo zinatayarisha na kurusha matangazo mbalimbali yanayolenga familia katika masuala ya kijamii, kisiasa, filamu, sinema za matukio ya kweli, masuala ya kiuchumi na kadhalika. Vilevile televisheni hizo huakisi habari za matukio mbalimbali ya kieneo na kimataifa.