May 08, 2016 09:49 UTC

Hatima ya mja baada ya kifo, ni miongoni mwa masuala yanayomtia wahka na wasiwasi mkubwa mwanadamu. Je, maisha ya mwanadamu ni hayahaya tuliyonayo hapa duniani yanayoanzia kipindi anapozaliwa hadi anapopatwa na mauti, na hakuna maisha mengine baada ya kufariki dunia? Na je, kuletwa kwetu duniani na kisha kufishwa, kumefanyika kwa malengo maalumu?

Ili kuweza kujibu maswali hayo na mengineyo mengi yanayohusiana na ulimwengu mwingine wa Akhera, kipindi hiki kinachohusiana na safari ya mja kurejea kwa Mola Muumba, kitakujieni kila wiki kikizungumzia kwa mapana zaidi maisha ya humu duniani ya mwanadamu hadi kipindi roho inapotenganishwa na mwili, ulimwengu wa Barzakh, Kiyama, amali za mja, mizani na masuala mengine mengi yanayohusiana na ulimwengu wa baada ya mja kuaga dunia.       <<<<<   >>>>>> 

 Ufufuo na marejeo ya mwanadamu kwa Mola Muumba ni miongoni mwa masuala muhimu sana na yanayohusiana na hatima ya milele. Tunasoma katika Qur'ani Tukufu kwamba, baada ya Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, hakuna maudhui nyingine iliyosisitizwa mno ndani ya kitabu hicho kitakatifu kama maadi, ufufuo na marejeo ya mja baada ya dunia hii.

Miongoni mwa matarajio makubwa zaidi ya mwanadamu katika kipindi chote cha maisha yake ya hapa duniani ni kuwa na maisha ya milele. Bila shaka hakuna mtu anayeweza kuthubutu kusema kwamba anaweza kuepuka kifo. Kuna ushahidi mwingi unaoonyesha kwamba wanadamu katika vipindi mbalimbali vya historia wamekuwa wakijiandaa kwa ajili ya maisha ya milele katika ulimwengu mwingine. Iwapo utapata fursa ya kuyaangalia makaburi mengi ya kale, utaona athari ambazo zinaonyesha kuwa, watu wa kale walikuwa wakiamini kuwepo maisha mengine baada ya umauti na kuaga dunia hii, na kulingana na imani na itikadi zao hizo, walikuwa wakifanya mambo ambayo yanaonesha kuwa walikuwa wakiamini yanawapatia utulivu wafu na jamaa zao waliofariki dunia huko katika ulimwengu wa Akhera. Kwa mfano tu miaka elfu tatu iliyopita, Wagiriki walikuwa wakiamini kwamba, mwanadamu hatokomei na kuisha moja kwa moja baada ya kukutwa na umauti. Wagiriki walikuwa wakiamini kwamba, maiti anahitajia mambo yaleyale aliyokuwa akiyahitajia hapa duniani huko katika ulimwengu wa Akhera. Kwa sababu hiyo, walikuwa wakiweka vyakula ndani ya makaburi ya wafu, ili kuwaandalia masurufu ya awali watakayohitajia katika ulimwengu wa Akhera.

Watu wa nchi ya Mexico pia walikuwa wakimzika mfalme wao akiwa na mavazi yake. Kwa mujibu wa itikadi na imani zao, mavazi anayovishwa mfalme wakati wa kuzikwa humpa hali ya uchangamfu, ucheshi na humuondolea ghamu na huzuni ndani ya moyo wake. Mambo kama haya yalifanywa pia katika baadhi ya nchi za Asia na Afrika kwa namna na sura tofauti.

Juhudi za wataalamu za kupata siri ya kuwa na umri mrefu, ni miongoni mwa hoja na ushahidi wa kifikra wa kubakia milele mwanadamu. Kwa hakika, hamu ya kupata uzima wa milele ni suala lililokuwepo katika dhati na maumbile ya wanadamu. Mwanadamu ndani ya nafsi yake ana hisi za kutaka kubaki milele na wakati huo huo anahisi kuwa mgeni katika dunia hii. Kiumbe huyo anapomaliza kazi zake za kila siku na anasa na burudani za aina mbalimbali, bado atajihisi kuwa na mapungufu ndani ya moyo wake na haridhishwi na jambo lolote. Hivyo, mtu kama huyo hujiuliza maswali mengi ikiwa ni pamoja na kwamba, ni lipi lengo la kuumbwa kwake? Kwa nini ameumbwa? Kwa hakika mwanadamu huyo huhisi kuwa dunia kwake ni mithili ya jela licha ya ukubwa wake. Huuona mwili wake kama tundu anamofungiwa ndege na dunia mithili ya jela kubwa.

Dakta Norman Vincent ambaye ni mtaalamu wa saikolojia wa Marekani anasema kuhusiana na fitra na uhakika wa maisha ya milele kwamba: “Hakuna hata chembe ya shaka kuhusiana na kuwepo maisha baada ya kifo, na mimi ninaamini hivyo. Hisi ya kifitra na kimaumbile ya kuwepo maisha ya milele ni moja kati ya ushahidi mwingi unatufanya sisi tupate uhakika huo”, mwisho wa kunukuu. 

Licha ya dunia ya sasa kupiga hatua kubwa katika medani za sayansi, elimu na teknolojia; lakini elimu hizo hazikanushi suala la kuwepo maisha mengine ya mwanadamu baada ya umauti. Sayansi inathibitisha kuwa, licha ya mabadiliko ya kikemia yanayokumba viumbe na vutu mbalimbali, lakini asili na kiini hakifutiki na kutoweka kabisa bali hubakia. Kwa mfano matone ya maji yanayodondoka ardhini, moshi unaofuka na kuelekea angani na mshumaa uliowashwa, hivyo vyote haviwezi kutoweka na kufutika moja kwa moja. Wanasayansi hao wanaeleza kuwa, iwapo vitapatikana vifaa, suhula na nyenzo makhsusi, inawezekana kuvikusanya tena vitu hivyo bila ya kupungua hata chembe ya mada zilizokuwepo hapo awali. Viungo vya mwili wa mwanadamu pia baada ya kufariki dunia, hutawanyika, hubadilika na hulika na kuwa katika hali nyingine na mwishowe kurejea katika udongo. Ijapokuwa mwili wa mwanadamu utakuwa umelika, kusambaratika na kuchanganyika na udongo, lakini asili au kile ambacho wataalamu wa sasa duniani wanakiita seli shina au seli msingi, hubakia kama ilivyokuwa. Wataalamu na wasomi wa elimu mbalimbali wamepiga hatua kubwa katika uwanja wa sayansi ambayo imethibitisha kuwepo maisha mapya baada ya haya ya sasa. Mafanikio hayo ya kielimu yenyewe yanaonyesha uhakika wa kuwepo maisha ya milele. Kwa sababu hiyo, hakuna shaka kuwa, Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kurejesha kwa mara nyingine tena viwiliwili vilivyotapakaa na kutawanyika katika udongo.

Kuamini suala la kuwepo maisha baada ya kifo na kuamini kuwepo adhabu na malipo kutokana na amali zilizofanywa na mja humu duniani, ni sababu ya kuwepo utulivu wa kinafsi na usalama katika jamii. Mwanadamu asiyekuwa na imani ya kuwepo maisha baada ya mauti, na anayeamini kuwa kifo ni hatua ya mwisho wa uhai, basi maisha ya mtu huyo hayatakuwa na maana yoyote hapa duniani. Tukiangalia kwa makini tutawaona kuwa watu wenye maisha mazuri ya kimaada katika nchi tajiri na zile zilizoendelea, daima wamekuwa wakijishughulisha na masuala ya burudani ili kwa namna fulani wajisahaulishe na maisha ya baadaye, na badala yake wafikirie maisha ya kimaada ambayo si ya kudumu. Lakini mtu kama huyo akiamini kuwepo maisha na makazi mengine ya daraja la juu zaidi kuliko maisha anayoishi humu duniani, hatokubali kushughulishwa na maisha yake ya hivi sasa na bila shaka atapata utulivu mkubwa wa kiroho.

Mtu anayeamini ufufuo hawezi kuhadaika na hizi siku chache za kuishi humu duniani, kwani maisha haya kadri yanavyosonga mbele ndivyo yanavyokuwa machache mno. Katika aya ya 64 ya Suratu al A'nkabut, Mwenyezi Mungu SW anasema:

وَمَا هَذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ لَهْوٌ وَلَعِبٌ وَإِنَّ الدَّارَ الآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ

"Na maisha haya ya dunia si chochote ila upuuzi na mchezo. Na nyumba ya Akhera ndiyo maisha hasa, lau wangelikuwa wanajua".

Kwa minajili hiyo, kuamini ufufuo na siku ya marejeo ni dira ya maisha bora ya mwanadamu. Binadamu ambaye anaamini siku ya ufufuo anaelewa kuwa Mwenyezi Mungu hakumuumba hivihivi bila ya lengo bali iko siku atarejea kwa Mola wake. Mwenyezi Mungu anasema katika Suratul Muuminun aya ya 115 kwamba: أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لا تُرْجَعُونَ

Je, mnadhani kuwa tuliwaumba bure na kwamba nyinyi Kwetu hamtarudishwa? 

 

Tags