Ufufuo na Safari ya Kurejea kwa Allah (2)
Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi katika kipindi kingine cha ufufuo na safari ya kurejea mja kwa Allah. Katika kipindi chetu kilichopita tulielezea maisha ya baada ya kifo na kwamba watu wengi ndani ya nyoyo zao wana hamu ya kuishi milele na kwamba hamu hii ya kimaumbile inapaswa kushibishwa kwa njia sahihi.
Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, je akili inathibitisha hisi hizo zilizoko ndani ya nyoyo za watu? Je, ufufuo na marejeo ya waja kwa Mola Muumba ni jambo linalowezekana au la? Katika kipindi chetu cha leo tutaelezea baadhi ya hoja zinazothibitisha kutokea ufufuo na safari ya mja kurejea kwa Mwenyezi Mungu.
Qur'ani Tukufu imesisitiza mno na kuwataka watu kutumia fikra na akili. Aya nyingi za Qur'ani Tukufu zimesifu suala la kutafakati na kutumia akili kwa kutumia maneno mbalimbali kama kutafakari, uono wa mbali, mazingatio, kufikiri kwa kina na kadhalika. Allamah Muhammad Hussein Tabatabai, mfasiri mkubwa wa Qur'ani Tukufu katika zama hizi anasema kwamba, zaidi ya aya 300 za Qur'ani zinamtaka mwanadamu kutumia fikra, awe mwenye kuzingatia na kutumia akili. Miongoni mwa maudhui inayomsisitiza sana mwanadamu kutumia akili, fikra na kutafakari ni suala hili la ufufuo.
Dini zote za mbinguni zinaamini kuwepo suala la ufufuo na marejeo kwa Mola Muweza na zinasisitiza kuwa, suala hilo ni miongoni mwa misingi muhimu ya kiitikadi. Bila shaka wapo baadhi ya watu ambao hawaamini na wanapinga kabisa suala la kuwepo maisha mengine baada ya kifo na kufariki dunuia. Hata hivyo, watu hao hawana hoja na ushahidi madhubuti wa kielemu wa kukanusha ufufuo. Jambo pekee wanalotumia kama hoja ya kupinga maadi na ufufuo ni kwamba inawezekana vipi kwa mtu aliyefariki dunia na mwili wake ukalikalika na kutawanyika, mifupa yake ikasagikasagika akarejea tena na kuwa hai? Kundi hili ni la watu ambao wanapuuza nguvu na uwezo usio na kikomo wa Mwenyezi Mungu. Watu hawa wanaghafilika kwamba, dunia na maajabu yake vimeumbwa kutokana na nguvu na Mwenyezi Mungu Muweza. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu SW anao uwezo wa kumrejesha na kumhuisha tena mwanadamualiyemuumba Yeye mwenyewe baada ya kufariki dunia. Vilevile akili ya mwanadamu inahukumu kwamba, kukusanya pamoja maungo na vipande vya kitu kilichosambaratika na kutawanyika ni rahisi zaidi kuliko kukiumba kwa mara ya kwanza. Wepesi wa jambo hilo ni sawa na kuunganisha vyombo mbalimbali vya mashine au mtambo fulani kwa mtu aliyeitengeneza hapo awali.
Kuwepo maisha na uhai mwingine baada ya kifo ni jambo linalotasawarika kwa kiumbe mwanadamu ambaye kila siku amekuwa akiona mifano ya kuhuishwa wafu kwa macho yake mwenyewe. Hapana shaka kwamba, kwa watu wanaoishi katika maeneo na nchi zenye baridi kali, wanaweza kuelewa na kuona vyema hali hii iwapo wataamua kutembelea mabustani wakati wa msimu wa baridi. Wakati huo mabustani yaliyokuwa yamenawiri kwa maua ya kupendeza na majani ya kijani kibichi huonekana kama makaburi yaliyogubikwa na kimya cha kutisha. Taswira hiyo ya kuhuzunisha huendelea hivyo hadi katika msimu wa machipuo. Unapoingia msimu wa machipuo na upepo mwanana ukaanza kuvuma, ghafla ardhi na mimea iliyokuwa imenyauka na kufa hupata uhai mpya na miti, maua na mimea yote huonekana kunawiri na kupata harakati tena baada ya kufa. Mwanadamu huishuhudia mandhari hiyo ya kupata uhai mpya na kufufuka mimea ikijikariri kila mwaka. Hata hivyo badala ya kupata ibra na funzo kutokana na hali hiyo, wanadamu wamekuwa wakipuuza na kupita kandokando ya mandhari hiyo yenye ibra na mafunzo tele bila ya kutafakati. Katika aya ya 29 ya Suratul Aaraf Qur'ani Tukufu inaweka wazi uhakikia huo kwa ibara fupi lakini yenye maana tele kwa kusema: "Kama alivyokuumbeni mwanzo ndivyo mtakavyorudi kwake…" Katika aya nyingine Qur'ani Tukufu inafananisha maisha ya baada ya mauti na kufufuka kwa mimea na kusema katika aya za 8 hadi 11 za Suratu Qaaf kwamba: "Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea. Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyobarikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa. Na mitende mirefu yenye makole yaliyozaa kwa wingi. Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyokuwa imekufa. Vivyo hivyo ndivyo utakavyokuwa ufufuaji".
Vilevile Mwenyezi Mungu SW katika aya ya 9 ya Suratu Faatir anawabainisha watu wasioamini Maadi na maisha ya baada ya mauti kwa kutoa mifano inayohisika na ya kimaada kwa kusema: "Na Mwenyezi Mungu Ndiye anayezituma pepo ziyatimue mawingu. Nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyokufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa kwake. Hivyo ndivyo kutakavyokuwa kufufuliwa".
Qurani Tukufu inaelezea maudhui ya kuhuishwa tena miili ya wanadamu baada ya kusambaratika na hata mabadiliko makubwa yatakayotokea ulimwenguni. Qur'ani inasisitiza kuwa, kama ambavyo mwanzoni, Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu kwa utaratibu na mahesabu maalumu, hivyo huko Akhera pia mwanadamu atarejeshewa umbo lake la awali kupitia mfumo na mahesabu maalumu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 5 hadi ya 8 ya Suratu Twariq kwamba: Hebu na ajitazame mwanadamu ameumbwa kwa kitu gani? Ameumbwa kwa maji yanayotoka kwa kuchupa. Yatokayo baina ya mifupa ya mgongo na mbavu. Hakika Yeye ni Muweza wa kumrejesha (baada ya kufariki dunia)".
Katika hatua ya kwanza kabisa, aya hizo zinamhimiza mwanadamu kutafakati kuhusu mwanzo wa kuumbwa kwake, na kisha ajiulize je, Mwenyezi Mungu atashindwa kweli kurejesha tena viungo na vipande vipande vya nyama na mifupa iliyosagika na iliyosambaa huku na kule? Qur'ani Tukufu inatoa hoja ya kiakili kwa kueleza kwamba, mtu anayefanya na kutengeneza jambo huwa na uwezo wa kulirejea au kulikariri jambo hilo.
Tukizitazama kwa makini aya za Qur'ani Tukufu tunaona kuwa, baadhi ya aya hizo zinatoa mifano ya wazi na ya kihistoria kuhusiana na ufufuo, ambazo zote zinaonesha ushahidi wa kuwepo maisha mengine baada ya umauti. Moja kati ya aya hizo inahusiana na kisa cha Uzayr. Qur'ani Tukufu inaelezea kisa hicho katika aya ya 259 ya Suratul Baqarah. Uzayr (as) aliyekuwa safarini juu kipando chake akiwa na chakula na maji kwa ajili ya kutumia njiani, alifika mahala ambapo nyumba za eneo hilo zilikuwa zimebomoka na kuharibika. Alipotazama huku na kule aliona mandhari ya kutisha ya viwiliwili vya wakazi wa kijiji hicho ambavyo mifupa yake ilikuwa imetapakaa na kusagika, hali iliyoonesha kwamba watu hao walifariki dunia miaka mingi iliyopita. Uzayr (as) alijiuliza ndani ya nafsi yake, vipi Mwenyezi Mungu ataweza kuirejesha tena miili hiyo iliyolika, kusagika na kusambaratika?
Uzayr hakuwa akitilia shaka au kukanusha uwezo wa Mwenyezi Mungu, bali alikuwa amestaajabishwa na hali aliyoiona. Mwenyezi Mungu alimfisha wakati uleule na kumfufua tena baada ya kupita miaka mia moja. Kisha alimuuliza, umepitisha miaka mingapi katika eneo hili? Uzayr (as) ambaye alidhani kwamba hakupitisha muda mrefu eneo hilo, alijibu kwa kusema: Siku moja au sehemu ya siku! Akaambiwa umepitisha miaka mia moja katika eneo hili! Akaambiwa, angalia chakula na maji yako, havijaharibika wala kubadilika licha ya kupita miaka yote hiyo. Ili aweze kujua kuwa imepita mia mia moja tangu alipofariki dunia, Uzayr (as) aliambiwa aangalie mnyama aliyekuwa amempanda kabla ya kufishwa na kisha atazame jinsi mifupa yake iliyochakaa na kusambaratika itakavyokusanywa tena na kuhuishwa. Uzayra alipoangalia mandhari ile alisema: Hakika sasa najua kwa yakini kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.