Jumamosi, 20 Februari, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 8 Rajab 1442 Hijria mwafaka na tarehe 20 Februari 2021 Miladia.
Tarehe 8 Rajab miaka 409 iliyopita alizaliwa faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabal Amil nchini Lebanon. Baada ya utafiti na uchunguzi wa muda mrefu Sheikh Aamili alitokea kuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa zama hizo hususan katika elimu za fiqhi na Hadithi. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi katika taaluma hizo na miongoni mwao ni kile cha Wasailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika elimu ya fiqhi. Kitabu kingine muhimu cha mwanazuoni huyo ni Hidayatul Ummah. Mwanazuoni huyo aliaga dunia mwaka 1114 Hijria.***
Katika siku kama ya leo miaka 344 iliyopita, Ufaransa ilivishinda vikosi vya Uhispania huko Haiti na kuanza kuikoloni ardhi ya nchi hiyo. Wafaransa waliikalia kwa mabavu Haiti iliyoko katika Bahari ya Atlantic kwa karibu miaka 130. Hata hivyo kufuatia harakati na mapambano makubwa ya watumwa weusi mnamo mwaka 1804 nchi hiyo ilijipatia uhuru na kuwa nchi ya kwanza katika eneo la Amerika ya Latini kujipatia mamlaka ya kujitawala.***
Miaka 155 iliyopita katika siku kama ya leo ya Februari 20, vita kati ya Ufaransa na wapigania uhuru wa Mexico vilimalizika kwa ushindi wa Ufaransa na kushika hatamu za uongozi mwanamfalme wa Austria, Maximilian. Katika vita hivyo vilivyoendelea kwa kipindi cha miaka 5, awali Ufaransa iliungana na Uhispania na Uingereza na baada ya muda mfupi nchi hizo mbili zilijitenga na Ufaransa ambayo iliendeleza vita dhidi ya wapigania uhuru wa Kimexico waliokuwa wakiongozwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Benito Juárez. Benito Juárez aliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kifaransa hata baada ya kurudi nyuma na kukimbilia katika maeneo ya milimani ya Mexico. Kiongozi huyo hatimaye alifanikiwa kuuangusha utawala wa Maximilian akisaidiwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Februari 1947, Uingereza hatimaye ilikubali kuipatia India uhuru wake baada ya kuikoloni nchi hiyo kwa zaidi ya karne mbili. Uhuru wa India ulipatikana kutokana na mapambano ya muda mrefu yaliiyoongozwa na Mahatma Gandhi. Katika kipindi chote cha utawala wake wa kikoloni huko India, Uingereza ilipora utajiri na maliasili za nchi hiyo na kuwasababishia hasara kubwa raia wa India. Mwezi Agosti mwaka huohuo India ikajipatia rasmi uhuru wake na ikagawanyika katika nchi mbili za India na Pakistan. ***
Na tarehe 20 Februari miaka 5 iliyopita aliaga dunia Sheikh Ahmad A'mir, qarii na msomaji maarufu wa Qur'ani Tukufu wa Misri. Alizaliwa mwaka 1927 katika eneo la Salihiyah huko mashariki wa Misri na kuhifadhi Qur'ani yote akiwa bado mdogo. Baadaye alijiunga na jeshi na mwaka 1963 alifanya kazi kwenye radio ya nchi hiyo. Qarii huyo mashuhuri wa Misri alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kusoma Qur'ani na alifika nchini Iran mara kadhaa katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu kama jaji wa mashindano hayo. Mara ya mwisho msomaji huyo mkubwa wa Qur'ani alitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 2013 na kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu. Baada ya mashindano hayo, Sheikh Ahmad A'mir alisoma Qur'ani katika majlisi iliyohudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei wakati huo akiwa na umri wa miaka 86. Qiraa ya Sheikh Ahmad A'mir katika majlisi hiyo iliwagusa sana hadhirina na kuwafanya wengi wabubujikwe na machozi. ***