Mar 10, 2021 21:20 UTC
  • Alkhamisi tarehe 11 Machi 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Rajab 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 11 Mchi mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1455 iliyopita, Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad Mustafa (s.a.w) alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu. Kipindi hicho Mtume Muhammad (s.a.w) alikuwa na umri wa miaka 40. Mtume Muhammad (saw) alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua juu utukufu wa mwanadamu. Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad (s.a.w) kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alipitisha muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa. Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumpa bishara ya kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake kwa walimwengu wote. Tangu siku hiyo Mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu.

Katika siku kama ya leo miaka 1117 iliyopita kisiwa cha Malta maarufu kama "Herini ya Mediterania", kilitwaliwa na Waislamu na kuunganishwa na mamlaka ya nchi za Kiislamu. Utawala wa Waislamu wa kisiwa cha Malta uliendelea hadi mwaka 1091 yaani hadi zama za udhibiti wa kaumu ya Norman kisiwani humo.

Siku kama ya leo miaka 975 iliyopita alizaliwa faqihi, mfasiri wa Qur'ani na msomi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari. Mwanazuoni huyu pia alikuwa gwiji katika elimu za hadithi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Muqaddimatul Adab na Asasul Balagha. Kitabu muhimu zaidi cha Jarullah Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya "al Kash'shaf". Zamakhshari aliaga dunia mwaka 538 Hijria.

Mahali alipozikwa Jarullah Zamakhshari

Siku kama ya leo miaka 214 iliyopita, alifariki dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tokea kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya msingi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kuwalea wanafunzi wengi na vile vile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.

Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, mgogoro mkubwa katika ngazi za uongozi wa Urusi ya zamani ulifikia kikomo kufuatia kutangazwa kifo cha Konstantin Chernenko na badala yake Mikhail Gorbachev ambaye wakati huo alikuwa mwanachama kijana zaidi katika Idara ya Siasa ya Chama cha Kikomunisti akatangazwa kuchukua nafasi ya Chernenko. Hatua ya kuchaguliwa Gorbachev kuongoza chama hicho cha Kikomunisti ilikwenda sambamba na kujiri mabadiliko makubwa, ambayo hatimaye yalipelekea kusambaratika Umoja wa Kisovieti. 

Mikhail Gorbachev

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita yaani mwaka 2004, watu karibu 200 waliuliwa na wengine 1000 kujeruhiwa kufuatia miripuko 5 ya mabomu iliyotokea kwenye vituo kadhaa vya treni ya chini ya ardhi (Metro) mjini Madrid, Uhispania. Miripuko hiyo inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa vitendo vikubwa vya kigaidi kuwahi kutokea Uhispania na Ulaya tangu mwishoni mwa vita vya Pili vya Dunia. Baada ya kutokea miripuko hiyo serikali ya wakati huo nchini humo iliituhumu kundi la Eta Basque ambalo linadai kujitenga na utawala wa nchi hiyo, kwamba ndilo lililohusika na miripuko, hata hivyo kundi la Al Qaida lilitangaza kuhusika katika miripuko hiyo. Miripuko hiyo ya Machi 11 ilitokea wakati chama cha Socialist kikiwa kimeshinda katika uchaguzi wa Bunge nchini humo na kuondoka vikosi vya Uhispania nchini Iraq.

Tarehe 11 Machi mwaka 2006 dikteta wa zamani wa Yugoslavia, Slobodan Milosevic alifariki dunia ndani ya jela katika mji wa The Hague akiwa na umri wa miaka 64. Miezi 9 baada ya kuanguka utawala wake mwaka 2001, Milosevic alitiwa mbaroni na kukabidhiwa na Yugoslavia ya zamani, kwenye mahakama ya uhalifu wa kivita ya mjini the Hague. Akiwa kijana alijiunga na chama cha Ucomonist cha Yugoslavia ya zamani. Mwaka 1989 Milosevic akawa Rais wa Serbiya. Milosevic aliongoza vita vilivyoanza mwaka 1992 vilivyo dumu kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Katika vita hivyo waislamu wa Bosnia laki mbili waliuawa, huku wengine milioni 2 wakibakia kuwa wakimbizi. Kufuatia kushindwa kwa Slobodan katika uchaguzi mwaka 2000 na kushadidi upinzani wa ndani dhidi yake, hatimaye utawala wake ulianguka na baada ya muda kidogo akatiwa mbaroni. Kesi ya Milosevic ilianza kusikilizwa mwaka 2002, hata hivyo kifo chake kilitokea kabla ya kumalizika kesi hiyo.

Slobodan Milosevic

Miaka 10 iliopita katika siku kama ya leo yaani machi 11 mwaka 2011, tetemeko la ardhi lililokuwa na ukubwa daraja 9 kwa kipimo cha rishta lililikumba eneo la Tohoku lililopo mkoa wa Miyagi Mashariki mwa Japan. Tetemeko hilo lilipelekea kuuawa kwa watu elfu 12 na malaki kadhaa ya wengine kubakia bila makazi kufuatia tetemeko hilo ambalo halijawahi kutokea mfano wake tangu makumi ya miaka yaliyopita nchini humo. Tetemeko hilo lilibomoa miundombinu, makazi ya raia na taasisi mbalimbali na kuiletea hasara ya mabilioni ya pesa nchi hiyo, kiasi kwamba kwa muda kadhaa Japan ilikuwa katika hali mbaya ya kiuchumi. Tetemeko hilo lilizua mawimbi ya Tsunami yaliyokuwa na mwinuko wa mita 15, huku mawimbi mengine madogo madogo yakizikumba nchi nyingine za jirani kufuatia tetemeko hilo.

زلزله‌

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita inayosadifiana na tarehe 27 Rajab 1415 Hijria, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kurusha matangazo yake kwa mara ya kwanza. Matangazo ya Radio Tehran yalianza kurushwa kwa muda wa nusu saa tu usiku, na yalifunguliwa kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kubaathiwa na kupewa Utume, Bwana wetu Muhammad (SAW). Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Tehran yalianza yakiwa na wafanyakazi wachache kama vile Sayyid Muhammad Ridha Shushtari, Sayyid Hashim Shushtari ambaye kwa sasa ni marehemu, Muhammad Baraza, Leyla Kimani, Said Kambi, Amir Ibrahim Rutajengwa, Abdul Fatah Mussa na Ahmed Rashid. Watangazaji wengine wa idhaa hii ni Asmahan Ghanima Mohammad, Salum Bendera, Mubarak Henia na Hussein Hassan Kamau. Lengo la kuasisiwa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kufikisha sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wanaodhulumiwa wa bara la Afrika, kuelimisha na kufichua njama za ubeberu wa kimataifa dhidi ya bara hilo. Kuanzia tarehe 26 Aprili mwaka 1997 Radio Tehran ilianza kutangaza kwa muda wa saa moja kuanzia saa mbili na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki, na matangazo hayo kurejewa siku ya pili yake kuanzia saa 12:30 asubuhi kwa majira ya Afrika Mashariki sawa na saa 11:30 asubuhi kwa majira ya Afrika ya Kati. Mnamo tarehe 23 Mfunguo Tatu (Dhulhijja) 1418 Hijria iliyosadifiana na tarehe 21 Aprili 1998, matangazo ya Radio Tehran yalianza kurushwa hewani kwa muda wa masaa matatu katika nyakati za usiku, asubuhi na machana. Saa moja ilikuwa ni marudio ya matangazo ya asubuhi, ambayo yalikuwa yakisikika kuanzia saa saba kamili hadi saa nane kamili mchana kila siku kwa majira ya Afrika Mashariki. Kwa hivi sasa Idhaa imeongeza wafanyakazi wake ambapo matangazo ya mchana nayo sasa yanasikika kwa njia ya moja kwa moja kuanzia saa 5:30 hadi 6:30 mchana kwa saa za Afrika Mashariki. Inarusha matangazo yake kwa ajili ya nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, mashariki mwa Zambia, kaskazini mwa Malawi na Msumbiji pamoja na Afrika Kusini. Matangazo hayo pia yanarushwa kwa ajili ya nchi za Mashariki ya Kati hususan za Ghuba ya Uajemi na Redio Tehran ina waandishi katika maeneo ya Afrika Mashariki na Kati kama vile KenyaTanzaniaUgandaBurundi na Kongo. Matangazo ya IRIB yanalenga kusambaza habari juu ya Iran na utamaduni wake, kusambaza mitazamo ya Kiislamu na mafundisho ya Mtume Muhammad (as) na Ahlul Baiti zake watoharifu. Vilevile IRIB inawabaishia walimwengu ubeberu wa Marekani na madola ya Kimagharibi dhidi ya mataifa mengine na ukandamizaji wa utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Idhaa ya Kiswahili, Redio Tehran