Ijumaa tarehe 12 Machi 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 28 Rajab 1442 Hijria sawa na Machi 12 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, msafara wa Imam Hussein (as), ulianza safari yake kutoka mjini Madina. Hatua hiyo ilitanguliwa na kuaga dunia Muawiya bin Abi Sufiyan hapo tarehe 15 ya mwezi huo huo wa Rajab na nafasi yakke ikachukuliwa na mwanaye, Yazid bin Muawiya. Yazidi alimtaka mtawala wa Madina amlazimishe Imam Hussein ili atoe baia na mkono wa utiifu kwa ajili yake na endapo angekataa, basi amuue. Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa Imam Hussein alikuwa akijua vyema kwamba Yazidi ni mtu muovu na fasiki, alikataa kutoa baia na mkono wa utiifu kwa kiongozi huyo na akaamua kuondoka Madina kuelekea Makka, akiwa na watu wa familia ya Mtume na idadi ndogo ya wafuasi wake.

Miaka 167 iliyopita katika siku kama hii ya leo mkataba wa kihistoria wa Constantinople (Istanbul) ulitiwa saini baina ya Ufaransa, Uingereza na utawala wa kifalme wa Othmaniyyah. Baada ya nchi hizo tatu kutia saini mkataba huo dhidi ya sera za kujitanua za Urusi ya zamani huko Ulaya, zilipata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupata ushindi dhidi ya Urusi katika vita vya Crimea.
Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, sawa na tarehe 28 Rajab mwaka 1337 Hijria, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi maarufu kwa jina la Allamah Yazdi, msomi mashuhuri wa Kiirani. Allamah Yazdi alipatia elimu ya kidini nchini Iran na huko katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq, kutoka kwa maulamaa kadhaa mashuhuri akiwemo Mirza Shirazi na kufikia daraja ya Ijtihad. Msomi huyo ameandika vitabu vingi, kikiwemo kitabu cha 'al U'rwatul Wuthqaa.
Miaka 96 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Sun Yat-sen mwanamapinduzi na Rais wa Kwanza wa China. Sun Yat-sen anayejulikana kama baba wa taifa la China alizaliwa mwaka 1866 huko Nanlang China. Mwaka 1892 alijiunga na Chuo Kikuu na akiwa na umri wa miaka 26 alifanikiwa kupata shahada ya udaktari. Uwanja na mazingira ya Sun Yat-sen ya kuanzisha harakati zake za kisiasa yaliandaliwa baada ya Japan kuishambulia China mnamo mwaka 1894. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanzisha harakati zake dhidi ya mfumo wa kifalme wa Manchu. Baada ya harakati hiyo kushindwa alikimbilia nje ya nchi. Mwaka 1905 alirejea China na kuanzisha Muungano wa Wanamapinduzi wa China lengo likiwa ni kuleta demokrasia katika nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1911 utawala wa familia ya kifalme ya Manchu ulifikia tamati baada ya kupinduliwa. Tukio hilo lilipelekea kutangazwa mfumo wa Jamhuri nchini China na Sun Yat-sen alifanikiwa kushika hatamu za uongozi akiwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya China.
Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Machi 1930 ilianza harakati kubwa ya uasi iliyoongozwa na Mahatma Gandhi, kiongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa India. Harakati hiyo kubwa ambayo iliwashirikisha wazalendo na wapigania uhuru wa India, ilifanyika kwa shabaha ya kukabiliana na maamuzi mapya ya serikali ya kikoloni ya Uingereza kuhusu ongezeko la ushuru wa chumvi. Katika kukabiliana na sheria hiyo ya kidhalimu, Mahatma Gandhi na wenzake elfu 78 walianza kutayarisha chumvi kutoka maji ya baharini. Wakoloni wa Uingereza walikabiliana na harakati hiyo kwa kuwatia nguvuni makumi ya maelfu ya Wahindi na kuwatia korokoroni. Hali hiyo ilisababisha ghasia na vurugu katika idara za serikali. Mapambano hayo ya Mahatma Gandhi yaliilazimisha serikali ya kikoloni ya Uingereza kusalimu amri na kulegeza misimamo yake.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita sawa na tarehe 12 Machi 1968 nchi ndogo ya Mauritius iliyoko kusini mwa Afrika ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Waholanzi waliingia Mauritius katika karne ya 17 na wakafuatiwa na Wafaransa karne moja baadaye. Mwaka 1814 Waingereza walikivamia kisiwa cha Mauritius na kukiunganisha na makoloni yao. Kisiwa hicho kina ukubwa wa kilomita mraba elfu mbili hivi na jamii ya zaidi ya watu milioni moja.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita inayosadifiana na tarehe 22 Esfand 1358 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini MA alitoa amri ya kuundwa taasisi ambayo itakuwa ikishughulikia hali za familia za mashahidi waliouawa wakitetea Mapinduzi ya Kiislamu nchini. Taasisi hiyo hadi sasa bado inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kiutamaduni, kijamii na kiuchumi kwa familia za mashahidi wa harakati za mapinduzi na hali kadhalika familia za mashahidi wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran.
