Jumatatu tarehe 15 Machi 2021
Leo ni Jumatatu tarehe Mosi Shaabani mwaka 1442 Hijria sawa na tarehe 15 Machi 2021.
Mwezi wa shaabani unaoanza leo ni mwezi wa ibada, kujipinda na kuomba maghufira. Mtume Muhammad (saw) aliutukuza mno mwezi huu na kuuita kuwa ni mwezi wake. Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake waliusia mno kufanya ibada hususan kufunga swaumu katika mwezi huu wa Shaabani kwa sababu ndio unaotayarisha uwanja mzuri wa kuingia kwenye mwezi wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na wenye baraka tele wa Ramadhan. Katika mwezi huu wa Shaabani kumetukia mambo mengi muhimu kama kuzaliwa Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw) na pia tukio la kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.

Tarehe Mosi Shaabani miaka 176 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Muhammad Hassan Najafi maarufu kwa lakabu ya Sahib al Jawahir. Sahib al Jawahir alifanya uhakiki mkubwa wa masuala ya fiqhi na kusajili fikra zake katika taaluma hiyo kwa njia ya kuvutia na nyepesi. Kitabu kikubwa zaidi cha mwanazuoni huyo ni "Jawahirul Kalam" ambacho kina thamani na umuhimu mkubwa sana kati ya wataalamu wa taaluma hiyo. Katika kitabu hicho Sheikh Muhammad Hassan Najafi ameandika masuala ya kifiqhi na sheria za Kiislamu kwa kutumia hoja madhubuti na uangaklifu mkubwa.
Siku kama ya leo miaka 167 iliyopita alizaliwa tabibu maarufu wa Kijerumani kwa jina la Emil Adolf von Behring. Behring aliendeleza utafiti wa Louis Pastor, mwanakemia wa Kifaransa wa zama hizo katika uwanja wa kutambua na kuzuia maradhi yanayoambukiza na kupata mafanikio makubwa katika suala hilo. Mwaka 1901 Emil Adolf von Behring alitunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia.
Katika siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, Parvin I’tisami mwandishi na malenga mahiri wa Kiirani aliyekuwa na kipaji kikubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Mshairi huyu alizaliwa katika familia iliyosifika kwa fadhila na heshima. Baba yake ni Yusuf I’tisam al-Mulk aliyekuwa mmoja wa watarjumi na waandishi watajika katika zama zake. Parvin alijifunza fasihi ya Iran na ya Kiarabu kwa baba yake na alionyesha kipaji cha hali ya juu cha mashairi tangu akiwa mdogo. Katika kipindi chote cha masomo, Parvin I’tisami alikuwa mwanafunzi bora shuleni. Safari zote alizifanya akiwa pamoja na baba yake na kujifunza mambo mengi katika safari hizo.
Miaka 33 iliyopita katika siku kama hii ya leo utawala wa zamani wa Baath huko Iraq uliushambulia mji wa Wakurdi wa Halabcha huko kaskazini mashariki mwa Iraq. Makumi ya ndege za kivita za utawala wa Saddam Hussein zilifanya mashambulizi ya kinyama kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Kikurdi wa mji wa Halabcha. Utawala wa Baath ulianzisha mashambulizi hayo katika hali ambayo kwa upande mmoja utawala huo ulikuwa umeshindwa kukabiliana na wapiganaji wa Kiislamu wa Iran na wa Kikurdi wa Iraq na kwa upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabcha waliwakaribisha na kuwaunga mkono wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo waliokuwa wakifanyiwa na Saddam Hussein. Nchi za Magharibi ambazo ndizo zilizoupatia utawala wa Saddam teknolojia na nyenzo zinazohitajika kwa ajili ya uzalishaji wa silaha hizo za kemikali, hazikuchukua hatua yoyote ya kivitendo mbele ya jinai hizo za Saddam Hussein, licha ya karibu watu elfu tano kuuawa katika maafa hayo ya kutisha ya Halabcha.
Siku kama hii ya leo miaka 32 iliyopita ardhi ya Taba huko kaskazini mashariki mwa Misri ilikombolewa baada ya kukaliwa kwa mabavu kwa miaka kadhaa na utawala ghasibu wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulilikalia kwa mabavu jangwa la Sinai katika vita vya mwaka 1967, ambalo upande wa mashariki mwake linapatikana eneo la Taba. Utawala wa Tel Aviv ulikubali kuirejeshea Misri jangwa la Sinai baada ya kusaini mkataba wa Camp David mwaka 1987. Israel iliendelea kulikalia kijeshi eneo muhimu la Taba huko kaskazini mwa Ghuba ya Aqaba, licha ya utawala huo wa Kizayuni kuondoka katika baadhi ya sehemu za jangwa hilo.