Ijumaa tarehe 26 Machi 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 12 Shaabani 1442 Hijria sawa na 26 Machi 2021.
Katoka siku kama ya leo miaka 944 iliyopita aliaga dunia Hassan bin Hafiz Ghassani mpokeaji hadithi na tabibu mashuhuri wa Andalusia, sehemu ya Uhispania ya leo. Ghassani alikuwa mwanafasihi mahiri na tabibu mweledi. Aidha alikuwa na hati za kuvutia sana na mwenye kipaji kikubwa cha kutunga mashairi.
Siku kama hii ya leo miaka 110 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Marekani, Tennessee Williams. Alivutiwa sana na fasihi na mvuto huo ulikolea na kuimarika zaidi wakati alipokuwa masomoni katika chuo kikuu na hatimaye alifanikiwa kuwa mwandishi mkubwa. Tennessee Williams alitumia uhodari wake kueleza fikra zake kwa lugha ya michezo ya kuigiza. Kazi zake nyingi zilieleza hali ya watu wa tabaka la chini na wanaosumbuliwa na ukata katika jamii ya Marekani. Miongoni mwa kazi za mwandishi huyo mashuhuri ni Cat on a Hot Tin Roof, Sweet Bird of Youth na The Glass Menagerie.
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, yalianza mapambano ya Mau-Mau yakiongozwa na Mzee Jomo Kenyatta, mwasisi wa nchi huru ya Kenya, dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Katika kipindi cha vita viwili vikubwa vya dunia, Kenya ilikumbwa na machafuko na vurugu nyingi. Hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wananchi wa nchi hiyo waliamua kupambana kufa na kupona ili kuikomboa nchi yao kutoka mikononi mwa wakoloni wa Ulaya. Wakoloni wa Kiingereza waliweka sheria kali katika maeneo tofauti ya Kenya hasa katika maeneo ya Wakikuyu lakini hilo halikuzuia kuasisiwa harakati ya Mau-Mau. Kaulimbiu kuu ya wapiganaji wa Mau-Mau ilikuwa ni kuweko usawa na uadilifu katika masuala ya kijamii na kisiasa baina ya wenyeji wa Kenya na Wazungu. Hatimaye harakati hiyo ya Mau-Mau kwa uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta ilifanikiwa kuikomboa Kenya kutoka mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza mwanzoni mwa muongo wa 60.
Tarehe 26 Machi mwaka 1971 katika siku kama hii ya leo, Pakistan Mashariki ambayo hivi sasa inajulikana kwa jina la Bangladesh iliamua kujitenga na Pakistan baada ya kuzuka mivutano mikubwa ya kisiasa na uasi nchini humo. Pakistan Mashariki na ile ya Magharibi ilikuwa nchi moja, iliyoamua kujitenga na India mwaka 1947. Wabangladeshi waliokuwa wakiishi Pakistan Mashariki na kuunda jumla ya asilimia 98 ya watu wa eneo hilo, hawakuridhishwa na vitendo vya kibaguzi vilivyokuwa vikifanywa na serikali kuu huko Pakistan Magharibi na kwa msingi huo awali walitaka kupewa mamlaka ya kujiendeshea mambo yao wenyewe. Baadaye walianzisha mapambano ya silaha na kufanikiwa kulifukuza jeshi la Pakistan Magharibi wakisaidiwa na jeshi la India. Pakistani Mashariki ilipewa jina la Bangladesh.
Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ahmad Sekou Toure kiongozi mkubwa wa nchi ya Kiafrika ya Guinea. Sekou Toure alizaliwa Januari 9 mwaka 1922 katika moja ya miji ya katikati mwa Guinea. Aliingia katika harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana na alikuwa akitaka uhuru wa chi yake kutoka kwa wakoloni wa Kifaransa. Hatimaye mwaka 1958 nchi hiyo ilipata uhuru na mwaka mmoja baadaye Touré akateuliwa kuwa rais na kusalia madarakani hadi mwaka 1984 alipofariki dunia.