May 13, 2021 02:18 UTC
  • Alkhamisi tarehe 13 Mei 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Shawwal 1442 Hijria sawa na tarehe 13 Mei mwaka 2021.

Leo tarehe Mosi Shawwal inasadifiana na sikukuu ya Idul-Fitr. Idul Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola Manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada huyo. Iddi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kujisafisha. Katika siku kama hii ya leo ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kusali Swala ya Iddul Fitr. Kuhusiana na utukufu wa siku hii Mtukufu Mtume (saw) anasema: "Mtu yeyote atakayemuasi Mwenyezi Mungu katika siku ya Idi, basi ni kama mtu aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya Miadi- yaani Siku ya Kiama." Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani.

Siku kama ya leo miaka 1189 iliyopita yaani tarehe Mosi Shawwal mwaka 253 Hijria Qamariya mpokezi mashuhuri wa hadithi wa Ahlusunna, Imam Muhammad Ismail Bukhari aliaga dunia. Abu Abdullah Muhammad Ismail aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Imam Bukhari ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa hadithi wanaoaminiwa na Ahlusunna. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta hadithi za Mtume (saw). Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni kile cha Jamius Swahih maarufu kama Sahihi Bukhari. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni: Al Adabul Mufrad, Tarikhul Ausat na As Sunan.

Muhammad Ismail Bukhari

Tarehe Mosi Shawwal miaka 873 iliyopita Said Bin Mubarak maarufu kwa jina la Ibn Dahhan, mfasiri, mwanafasihi na malenga wa Kiislamu alifariki dunia. Alizaliwa mjini Baghdad na baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alianza kusoma lugha sambamba na kupokea hadithi kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake. Mtaalamu huyo mkubwa wa lugha alitilia maanani taaluma ya fasihi hususan katika kusoma mashairi na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi wake katika usomaji mashairi.

Said Bin Mubarak

Miaka 836 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi mashuhuri kwa jina la Fakhrurazi msomi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Rey jirani na Tehran na alifanikiwa kwa haraka kujifunza elimu mbalimbali za Kiislamu kama Fiqihi, Tafsiri, Falsafa na Mantiki kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya Fakhrurazi ni al Tafsirul Kabiir, Sherh Nahaj al-Balagha, Nihayat al-Uquul wa Siraj al-Quluub.

Fakhrurazi

Siku kama ya leo miaka 308 iliyopita alizaliwa mjini Paris, Alexis Cloude Clairaut mwanahesabati mashuhuri wa Ufaransa. Alikuwa na hamu kubwa na somo la hesabati ambapo akiwa na umri mdogo wa miaka 18 alifanikiwa kujiunga na Chuo cha Sayansi cha Ufaransa. Clairaut alipata umashuhuri mkubwa duniani kutokana na utafiti makini aliofanya katika nyanya tofauti za sayansi. Msomi huyo aliaga dunia mwaka 1765.

Alexis Cloude Clairaut

Katika siku kama ya leo miaka 114 iliyopita alizaliwa Bi Daphne du Maurier mwandishi wa riwaya, wasifu na thamthiliya wa Kiingereza. Maurier alizaliwa katika familia ya wanasanaa na iliyokuwa pia na wanafasihi. Ni kutokana na kukulia katika mazingira kama hayo, ndipo Bi Daphne du Maurier akafanikiwa kukuza kipaji chake katika uwanja wa uandishi. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Scapegoat na Rebecca. Mwandishi huyo aliaga dunia mwaka 1889.

Daphne du Maurier

Na siku kama ya leo miaka 42 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsiya, mkataba wa kutoshtakiwa Wamarekani nchini Iran au Capitulation Accord ulifutwa nchini kufuatia mapambano yasiyosita ya wananchi Waislamu wa Iran, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu na kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kwa mujibu wa sheria za mkataba huo, raia wa Marekani aliyekuwa nchini Iran alikuwa na kinga kamili ya kisheria dhidi ya kufunguliwa mashtaka. Kwa kadiri kwamba hakuna taasisi au chombo chochote cha kisheria cha Iran kilichokuwa na mamlaka ya kumfungulia mashtaka na kumhukumu raia wa Marekani aliyekuweko Iran na kesi za raia hao wa Kimarekani zilipaswa kusikilizwa katika nchi yao.