Jumamosi, 25 Septemba, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 18 Mfunguo Tano Safar 1443 Hijria, sawa na tarehe 25 Septemba 2021 Miladia.
Siku kama ya leo ya tarehe miaka 1406 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, aliuawa shahidi Uways al Qarani, mmoja kati ya wafuasi waaminifu wa Mtume Mtukufu SAW na Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika vita vya Siffin. Uways Qarani aliishi katika eneo la Qaran lililoko Yemen na alikuwa mchamungu mkubwa. Licha ya kuwa na mapenzi makubwa kwa Mtume Mtukufu SAW, Uways Qarani hakubahatika kumuona mtukufu huyo, kwa kuwa kipindi hicho alikuwa akimuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa. Baada ya Mtume Mtukufu SAW kufariki dunia, Uways Qarani alikuwa miongoni mwa wafuasi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Hata hivyo Mtume Muhammad (saw) alimzungumzia Uways na kumsifu licha ya kwamba hakuwahi kuonana naye. Shakhsia huyo akiwa pamoja na wapiganaji wengine katika jeshi la Imam Ali (as), alishiriki kikamilifu kwenye vita vya Siffin kati ya jeshi la Imam Ali na lile la Muawiya bin Abi Sufiyan na akauawa shahidi katika vita hivyo. ***
Miaka 137 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 18 Mfunguo Tano Safar alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Mir Hamid Hussein Mussawi Hindi. Alizaliwa mwaka 1246 Hijria nchini India na kupata elimu katika taaluma za fiqhi, Hadithi, teolojia na elimu nyingine za Kiislamu. Miir Hamid Hussein alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufunza elimu za kidini na kuandika vitabu. Kitabu muhimu zaidi cha Allamah Miir Hussein Hindi ni A'baqaatul Anwar. Vitabu vingine vya msomi huyo wa Kiislamu ni pamoja na Asfarul Anwar na Sham'ul Majalis.***
Katika siku kama ya leo miaka 124 iliyopita alizaliwa mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. Faulkner hakukamilisha masomo yake ya juu na alianza kujishughulisha na kazi mbalimbali ka ajili ya kuendesha maisha. Mwandishi huyo mashuhuri alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa sasa nchini Marekani. Mwaka 1950 mwandishi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel. ***
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita iliasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Jumuiya hiyo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa na nchi wanachama 57 katika mabara zaidi ya manne. Jumuiya hiyo inahesabiwa kuwa sauti ya ulimwengu wa Kiislamu yenye jukumu la kulinda maslahi ya Waislamu, kueneza moyo wa amani na kuratibu masuala ya Waislamu. Jumuiya hiyo iliundwa katika mkutano wa Kihistoria uliofanyika Rabat nchini Morocco tarehe 25 Septemba mwaka 1969 kama jibu la hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa al Aqsa huko Baitul Muqaddas. ***
Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita aliaga dunia Edward Said, mwandishi na mwanafikra wa Kipalestina kutokana na maradhi ya saratani. Said alizaliwa mwaka 1935 katika familia ya Kikristo. Alielekea Marekani kwa ajili ya kudumisha elimu akiwa na umri wa miaka 17 na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo kikuu cha Harvard. Kitu kilichompa umashuhuri zaidi Prf. Edward Said katika upeo wa kimataifa ni jitihada zake kubwa za kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina bila ya kusita. Mwanafikra huyo mtajika alifikisha sauti ya kudhulumiwa wananchi wa Palestina katika masikio ya walimwengu kupita makala na vitabu vyake. Ameandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la Orientalism ambacho ndani yake anaeleza jinsi wataalamu wa masuala ya Mashariki wa Wamagharibi wanavyotumiwa kama wenzo wa wakoloni kwa ajili ya kuhalalisha uporaji wa mali na maliasili za mataifa ya Mashariki mwa dunia. ***