Alkhamisi tarehe 6 Januari mwaka 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Jamadithania 1443 hujria sawa na Januari 6 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita alikufa shahidi Bibi Fatima al Zahra, binti mtukufu wa Mtume wetu Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa Nabii Muhammad (saw) na mtukufu huyo akampa jina la Fatima. Alipewa malezi na wazazi wake wawili yaani Bibi Khadija na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kupata maarifa aali ya dini kutoka kwa baba yake. Bibi Fatima alifikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho na kimaanawi ndani ya nyumba ya wahyi na ufunuo. Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib ambaye alikuwa kielelezo halisi cha takwa na uadilifu, Bibi Fatima alikuwa na nafasi kubwa na alitoa mchango wa aina yake katika jamii ya Kiislamu. Alikuwa dhihirisho la uchamungu, ukarimu, kujitolea, subira, kujipinda katika ibada na kuwasaidia watu wote na alilea watu adhimu kama Imam Hassan na Hussein (as).

Siku kama ya leo miaka 784 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alifariki dunia Abu Bakr Muhammad bin Ahmad maarufu kwa jina la Ibn Sayyidun-Naas, faqihi, mtaalamu wa hadithi, mwanahistoria na msomi wa fasihi wa Andalusia au Hispania ya leo. Mwanazuoni huyo alifariki dunia nchini Tunisia. Ibn Sayyidun-Naas alizaliwa mwaka 597 Hijiria katika viunga vya mji wa Seville (Ishbilia) huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na masomo. Abu Bakr Muhammad bin Ahmad alifundisha kwa miaka mingi katika eneo hilo na kulea wanafunzi wengi. Msomi huyo alitabahari pia katika taaluma ya mashairi na fasihi; na mashairi yake mengi yanamsifu Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni kile cha Sira na Maisha ya Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo 161 iliyopita ilianzishwa nchi ya Romania. Mpango wa kuasisiwa nchi ya Romania ulibuniwa tarehe 13 Disemba 1859 kwa kuunganishwa miji miwili midogo ya Moldavia na Wallachia. Miaka miwili baadaye majimbo na miji mingine ilijiunga na umoja huo na kuundwa nchi ya Romania.
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita alifariki dunia Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi na kutokuwa na wizani. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita kulitokea hamasa ya mashahidi wa Huweize iliyoongozwa na Shahidi Alamul Huda katika miezi ya mwanzoni mwa uvamizi wa Iraq dhidi ya ardhi ya Iran. Mwezi Dei mwaka 1359 Hijria Shamsia na baada ya jeshi la Iran ya Kiislamu kuvishinda vikosi zaidi ya viwili vya jeshi la Iraq huko kusini mwa eneo la Susangerd, kundi moja la Jeshi al Sepah la Ahwaz huko kusini mwa Iran lilitumwa katika mji wa Huweize kwenda kuulinda mji huo mbele ya mashambulizi ya Iraq. Hata hivyo kutokana na kuchelewa kufika zana na hujuma kubwa ya Iraq, jeshi la Iran lililazimika kurudi nyuma. Wakati huo zaidi ya wapiganaji mia moja wa Jeshi la Sepah, wapiganaji wa kujitolea na wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi waaminifu wa Imam Khomeini wakiongozwa na Sayyid Muhammad Hussein Alamul Huda walibakia katika mji huo wa Huweize wakipambana na adui na wakauawa shahidi. Baadaye jeshi la Iraq liliuvunja kabisa mji wa Huweize na kuusawazisha na ardhi. Pamoja na hayo ushujaa wa vijana hao shupavu wa Iran waliosabilia roho zao kulinda ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu umebakia hai katika historia ya Iran.