Jumamosi 8 Januari, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 5 Mfunguo Tisa Jamadi Thani 1443 Hijria sawa na tarehe 8 Januari 2022 Miladia.
Miaka 823 iliyopita Ebn-e Ghodameh Maghdesi fakihi na mpokezi wa hadithi Mwislamu wa Damascus Syria aliaga dunia. Alisoma na kumaliza masomo ya msingi katika mji wa Damascus na kisha baadaye akajifunza Qur'ani na hadithi katika mji huo huo. Baadaye Ebn-e Ghodameh Maghdesi alielekea Baghdad, Iraq na kunufaika na bahari ya elimu ya wanazuoni na Maulamaa mahiri wa zama hizo. Msomi huyu alikuwa amebobea katika kualifu na kuandika vitabu. ***
Siku kama ya leo miaka 771 iliyopita sawa na tarehe 5 Jamadithani mwaka 672 alifariki dunia Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Maulawi, mshairi mkubwa wa Iran katika mji wa Kunya ambao ni moja kati ya miji ya zamani ya Iran ulioko kusini mwa Uturuki ya leo. Maulawi alihesabiwa kuwa mshairi mkubwa na maarufu zaidi katika karne ya 9 Hijria Shamsia na miongoni mwa wanafikra na wachamungu wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Maulawi alizaliwa mwaka 604 Hijria Shamsia katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya sasa na baada ya muda akahamia katika mji wa Konya akiandamana na baba yake. Baadaye alielekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maulawi, Fihi ma Fihi, Maktubat Maualana na Rabaiyat. ***

Miaka 380 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia Galileo Galilei akiwa na umri wa miaka 78. Alizaliwa katika mji wa Pisa na alisoma fasihi hadi alipofikisha umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya Abu Raihan Biruni msomi mashuhuri wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, Kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa ni kafiri na akahukumiwa. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake. ***
Katika siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, yaani tarehe 8 Januari mwaka 1932 ulianza utawala wa kifalme wa Abdul-Aziz Ibn Saud katika eneo la Bara Arabu kupitia msaada wa Uingereza. Abdul-Aziz Ibn Saud, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa makabila ya Hijaz, alianzisha mapigano dhidi ya utawala wa Othmania mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 na kupata ushindi. Mwaka 1903 mtawala wa Kiothmania alitimuliwa katika eneo la ya al-Ahsa huko Hijazi na tukio hilo lilikuwa jiwe la msingi wa kuasisiwa utawala wa Aal-Saud katika maeneo hayo. Katika kipindi cga Vita vya Kwanza vya Dunia, Aal-Saud waliingia ubia wa urafiki na Uingereza. Hatimaye mwishoni mwa vita hivyo vilivyomalizika kwa kushindwa vibaya utawala wa Othomania, utawala huo ulifikia tamati kikamilifu katika eneo hilo la Bara Arabu. Katika vita vilivyopiganwa baina ya Abdul-Aziz Ibn Saud na mtawala Hussein Bin Ali Sharif aliyekuwa mtawala wa mji wa Makkah, Ibn Saud aliibuka mshindi na akatwaa kwa nguvu eneo hilo la Hijaz. Hatimaye mwaka 1926 na kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwepo kati ya Uingereza na mtawala huyo huyo wa Kiwahabi, Abdul-Aziz Ibn Saud alijitangaza kuwa kiongozi wa Hijaz. Mwaka 1927 Ibn Saud alijitangaza rasmi kuwa mtawala wa Hijaz na Najd na tarehe 8 Januari mwaka 1932 Abdul Aziz alitangazwa kuwa mfalme wa Saudi Arabia. Hadi kutwaa madaraka ya eneo lote la Hijaz, watu wa kizazi cha Aal Saudi walifanya mauaji mengi na umwagaji damu mkubwa na kuwalazimisha watu wa maeneo hayo kufuata fikra na itikadi potufu za kiwahabi. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Tabatabai, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu na maulamaa wapigania uhuru wa Iran. Wakati wa mapinduzi ya kikatiba nchini Iran, Sayyid Muhammad Tabatabai alikuwa akihesabika kuwa mmoja kati ya viongozi wakubwa wa mapinduzi hayo. Tabatabai alishirikiana na Sayyid Abdullah Behbahani ambaye naye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya kikatiba dhidi ya utawala wa Qajari nchini Iran. ***