Jan 12, 2022 02:33 UTC
  • Jumatano tarehe 12 Januari 2022

Leo ni Jumatano tarehe 9 Jamadithani 1443 Hijria sawa na tarehe 12 Januari 2022.

 Siku kama ya leo miaka 744 iliyopita yaani tarehe 9 Mfunguo Tisa Jamadi Thani mwaka 699 Hijria, Ibn Farah Eshbily malenga, mshairi na mtaalamu wa elimu ya hadithi katika karne ya saba Hijria alifariki dunia. Alizaliwa katika Andalusia ya zamani ambayo leo ni eneo la kusini mwa Uhispania. Alitiwa mbaroni baada ya majeshi ya Uhispania kuushambulia mji huo. Hata hivyo baada ya kushikiliwa kwa muda, alitoroka na kukimbilia nchini Misri. Akiwa nchini Misri Ibn Farah Eshbily alifanikiwa kuchota elimu na maarifa kwa maulama mashuhuri wa zama hizo mjini Cairo. Baada ya muda alielekea Damascus Syria na kujiendeleza zaidi kielimu. Alimu na msomi huyu wa Kiislamu ameandika vitabu vingi hususan katika uga wa mashairi.

Miaka 357 iliyopita katika siku inayosadifiana na leo, aliaga dunia Pierre de Fermat mwanahisabati wa Kifaransa na muasisi wa nadharia ya leo ya namba yaani Modern Theory of Numbers na ile ya uwelekeo inayojulikana kama Theory of Probability. Pierre de Fermat alizaliwa mwaka 1601 Miladia na alianza kujifunza hesabu tangu akiwa mtoto. Mwanahisabati huyo wa Kifaransa aligundua pia kanuni msingi ya jiometri changanuzi, yaani Analytic Geometry.

Pierre de Fermat

Siku kama ya leo miaka 146 iliyopita, alizaliwa Jack London mwandishi mashuhuri wa nchini Marekani. Kwa miaka kadhaa Jack alifanya safari katika eneo la ncha ya Kaskazini na maeneo mengine na kupata bahati ya kufahamiana na koo na kaumu mbalimbali katika maeneo hayo sambamba na kubainisha taswira ya masuala hayo katika vitabu vyake.  Jack London aliishi kwa muda wa miaka 40 huku akijihusisha na kazi ya uandishi kwa muda wa miaka 18.

Jack London

Miaka 43 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu aliagiza kuundwa Baraza la Mapinduzi katika kipindi hicho muhimu cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Imam aliagiza baraza hilo liundwe wakati Marekani ilipokuwa ikifanya njama za kuulinda utawala wa kifalme wa Pahlavi. Jukumu kubwa la baraza hilo lilikuwa ni kuratibu mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na pia kuandaa uwanja mzuri wa kuundwa serikali ya muda nchini Iran.

Wanachama wa Baraza la Mapinduzi

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, mhadhiri wa nyuklia wa Chuo Kikuu cha Tehran, Dokta Massoud Ali-Mohammadi aliuawa kigaidi. Massoud Ali-Mohammadi aliyekuwa na umri wa miaka 50 aliuawa kwa mlipuko wa bomu la kuongozwa kutoka mbali wakati alipokuwa akitoka nyumbani kwake. Alipata shahada ya uzamivu ya taaluma ya fizikia katika Chuo Kikuu cha Sharif mjini Tehran mwaka 1371 Hijria Shamsia na alikuwa miongoni mwa wanachuo wa kwanza wa Iran kupata shahada ya uzamivu ya somo la fizikia ndani ya Iran. Alitunukiwa tuzo ya Tamasha ya Kimataifa ya Kharazmi mwaka 1386 Hijria Shamsia na kushika nafasi ya pili katika utafiti wa masuala ya kimsingi. Wapinzani wa miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran baada ya kushindwa kusimamisha miradi hiyo kwa hatua za kisiasa na vikwazo vya kiuchumi walikhitari kutumia njia za kigaidi na kuwaua wasomi wa nyuklia wa Iran. Magaidi waliomuua msomi huyo wa Iran walitiwa nguvuni na kukiri kwamba walikuwa wakishirikiana na utawala haramu wa Israel.

Dokta Massoud Ali-Mohammadi

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta ilitokea huko Haiti katika bahari ya Caribbean. Zilzala hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea duniani katika miongo kadhaa iliyopita na iliua watu karibu laki tatu na kujeruhi wengine wengi. Mtetemeko huo wa ardhi ulioikumba Haiti uliharibu kabisa miundo mbinu na nyumba nyingi za nchi hiyo. Aidha ulipelekea mamia ya maelfu ya raia kuwa wakimbizi.