May 28, 2022 03:25 UTC
  • Jumamosi, 28 Mei 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria sawa na tarehe 28 Mei 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 170 iliyopita, alifariki dunia Eugène Burnouf, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufaransa. Burnouf alizaliwa Paris mwaka 1801 na kuhitimu somo la sheria. Hata hivyo hamu yake kubwa ya kusomea lugha na fasihi sambamba na kuvutiwa na masuala ya Mashariki ya Kati, vilimfanya ajifunze lugha za Sanskrit na Iran ya kale. Eugène Burnouf pia alijifunza utamaduni wa nchi za Iran na India. Miongoni mwa kazi zilizozifanya msomi huyo ni pamoja na kufasiri sehemu za kitabu cha Avesta. Vitabu vya ‘Dondoo za Yasna’ ‘Historia ya dini ya Mabudha’ na ‘Babr Bayan’ ni miongoni mwa vitabu vya Eugène Burnouf. ****

Eugène Burnouf

 

Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilitangaza kuanzishwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) ambayo mwanzoni ilijumuisha harakati nane za mapambano pamoja na idadi kubwa ya taasisi za kielimu, kijamii, kitiba, kiutamaduni na kifedha. Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la PLO la a Fat'h ambalo lilikuwa na wanachama 10,000 lilianzisha shughuli za kupigania ukombozi wa Palestina. Mwaka 1974, PLO ilikubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa na hadi mwaka 1982 ilikuwa imeanzisha uhusiano rasmi na zaidi ya nchi 100 za dunia. Taratibu PLO ilianza kupoteza mwelekeo wake wa kupambana kijeshi na utawala ghasibu wa Israel na mwaka 1993, ikiongozwa na Yassir Arafat, harakati hiyo ilikubali kuutambua rasmi utawala haramu wa Israel kwa kutia saini mapatano ya Oslo. ***

Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO)

 

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, yaani tarehe saba Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsia duru ya kwanza ya Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (bunge) ilianza. Kufunguliwa duru hiyo ya Majlisi ya kutunga sheria ilikuwa hatua muhimu katika historia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jukumu la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ni kutunga sheria na kusimamia kwa njia ya moja kwa moja utendaji kazi wa rais wa nchi na baraza lake la mawaziri. Hivi sasa Majlisi ina wajumbe 290 ambao huchaguliwa moja kwa moja na wananchi. Kila eneo hupata mbunge kwa kutegemea idadi ya watu wa eneo hilo. Idadi ya wafuasi wa dini za wachache hapa nchini, ingawa haiwezi kufikia kiwango kinachohitajika kwa ajili ya kutengewa mbunge, lakini katiba ya nchi inawapa fursa ya kuwachagua wawakilishi wao bungeni.  Vikao vya wazi vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu hutangazwa moja kwa moja kwa njia ya redio na vile vile magazeti ya nchini hutoa ripoti kuhusu vikao hivyo. ***

Bunge la Iran

 

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita sawa na tarehe 28 Mei 1991, utawala wa kikomunisti wa Mengistu Haile Mariam ulisambaratika nchini Ethiopia na kupelekea mtawala huyo dikteta kukimbia nchi. Ethiopia ni moja ya nchi kongwe zaidi barani Afrika na wakati mmoja ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Misri ya kale. Tokea karne ya 16 wakoloni wa Ureno, Uingereza na Italia walifanya juhudi kubwa za kuikoloni nchi hiyo kwa lengo la kupora utajiri wake lakini bila mafanikio makubwa. Italia iliishambulia Ethiopia mara mbili. Shambulio la kwanza likifanyika mwaka 1896 ambapo ilishindwa kufikia malengo yake, na la pili likafanyika mwaka 1936 ambapo iliikalia kwa mabavu Ethiopia kwa muda wa miaka mitano. Mfalme wa mwisho kuitawala Ethiopia alikuwa Haile Selassie ambaye aliitawala nchi hiyo tangu mwaka 1930 hadi 1974 na akapinduliwa na watawala wa kikomunisti, ambao nao baadaye walikabiliwa na upinzani mkubwa wa ndani kutokana na majanga ya njaa na matatizo mengine yaliyotokana na utawala mbaya. ***

Mengistu Haile Mariam

 

Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Mei 1998, kwa mara ya kwanza Pakistan ilifanya majaribio matano ya makombora ya nyuklia. Majaribio hayo yalifanyika zikiwa zimepita wiki mbili tu tangu hasimu wake, yaani India, ifanye majaribio ya kombora la nyuklia. Baada ya hapo nchi hizo mbili zimekuwa zikifanya kwa zamu majaribio yao ya makombora ya nyuklia. Majaribio ya nyuklia ya Pakistan, kinyume na yale yanayofanywa na India,  yamekuwa yakizikasirisha mno nchi za Magharibi za Marekani na Ulaya, na kufikia hatua ya kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi. ***

Majaribio ya nyuklia

 

Tags