Jul 14, 2022 09:39 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, na karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi. Mwenyezi Mungu alipowaumba Manabii, Mitume na Maimamu waongofu kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu, aliwapa watukufu hao uwezo, fadhila na vipawa maalumu kwa ajili ya kufikia lengo hilo la kuwaongoza wanadamu kwenye njia nyoofu.

Al-Khawarazmi al-Hanafi anazungumzia suala hili katika kitabu chake cha 'Maqtal al-Hussein' (as) akimnukuu swahaba mwema na mwenye ikhlasi, Asmaa bint Umays, kwamba alimwambia Ali bin al-Hussein (as): 'Bibi (nyanya) yenu alipojifungua Hassan na Hussein mimi nilikuwa mkunga wake. Alisema: Alipojifungua Hassan, Mtume (saw) aliniambia: Niletee mwanangu. Nilimpelekea nikiwa nimemfunika kwenye shuka ya njano, naye Mtume (saw) akaitupa pembeni na kuniambia: Je, Asmaa, sikukwambieni msimfunike mtoto huyo kwa shuka ya njano?!' Akasema (Asmaa). Baada ya hapo nilimfunika kwa shuka nyeupe na kumpa Mtume ambaye alimuadhinia kwenye sikio lake la kulia na kumkimia kwenye sikio lake la kushoto. Akamuuliza Ali (as): Je, umemmpa jina gani? Akasema: Nisingeweza kumpa jina kabla yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume (saw) akasema: Na mimi pia siwezi kumtangulia Mola Mtukufu kumpa jina….. Hapo Malaika Jibril (as) akawa ameteremka kutoka mbinguni na kusema: Salamu ziwe juu yako ewe Muhammad! Mwenyezi Mungu aliye juu anakupa salamu na kusema: Ali kwako wewe ni kama alivyokuwa Harun kwa Musa na wala hakuna Mtume mwingine atakayekuja baada yako. Muite mtoto wako huyu jina la mtoto wa Harun…. Mtume akauliza: Na mtoto huyo alikuwa akiitwa nani? Jibril akajibu: Shubbar. Mtume akasema lakini lugha yangu mimi ni Kiarabu….. Jibril akasema muite Hassan. Asmaa akasema: Mtume akawa Amempa jina la Hassan na ilipofika siku ya saba alimfanyia Aqiiq kwa kumchinjia kondoo wawili wenye rangi nyeupe na nyeusi. Kisha alinyoa nywele yake na kutoa sadaka madini ya fedha iliyo na thamani ya wizani ya nywele hiyo.

********

Tunaendelea kuwa pamoja na Al-Khwarazmi ambaye anaendelea kutufafanulia riwaya ya Asmaa bin Umays ambaye anaikamilisha riwaya hiyo kwa kusema: Baada ya kupita mwaka mmoja baada ya kuzaliwa al-Hassan, Fatwimah alijifungua al-Hussein ambapo Mtume (saw) alifika mbele yangu na kuniambia: Ewe Asmaa! Niletee mwanangu….. nilimpa nikiwa nimemfunika shuka nyeupe ambapo alimuadhinia kwenye sikio lake la kulia na kumkimia kwenye sikio lake la kushoto. Kisha alimpakata na kulia. Asmaa akasema: Nilimwambia (Mtume), baba na mama yangu wawe fidia kwako! Ni nini kinachokuliza? Akasema: Ni mwanangu huyu…..Nikasema: Lakini amezaliwa hivi sasa tu…. Akasema: Ewe Asmaa! Atauliwa na kundi dhalimu. Mwenyezi Mungu asilijalie shafaa yangu! Kisha akasema: Ewe Asmaa! Usimwambie Fatwimah habari hii kwa sababu amejifungua hivi sasa tu. Kisha akamuuliza Ali: Umempa jina gani mwanagu? Akasema: Nisingelikutangulia kumpa jina, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mtume (saw) akasema: Na mimi sitamtangulia Mola wangu Mtukufu kumpa jina. Hapo Jibril (as) akawa ameteremka kutoka mbinguni na kusema: Salamu ziwe juu yako ewe Muhammad! Mwenyezi Mungu aliye juu anakupa salamu na kusema: Ali kwako wewe ni kama alivyokuwa Harun kwa Musa na wala hakuna Mtume mwingine atakayekuja baada yako. Muite mtoto wako huyu jina la mtoto wa Harun…. Mtume akauliza: Na mtoto huyo alikuwa akiitwa nani? Jibri akajibu: Shubair. Mtume akasema lakini mimi ni Mwarabu….. Jibril akasema muite Hussein. Asmaa akasema: Mtume akawa Amempa jina la Hussein na ilipofika siku ya saba alimfanyia Aqiiq kwa kumchinjia kondoo wawili wenye rangi nyeupe na nyeusi. Kisha alinyoa nywele yake na kutoa sadaka madini ya fedha iliyo na thamani ya wizani ya nywele hiyo."

Na hivi, wasikilizaji wapenzi, ndivyo alivyofanya juhudi kubwa Mtume Mtukufu (saw) katika kulinda, kujali na kuwalea wajukuu wake wawili hao watukufu tokea walipozaliwa na hata kabla ya kuzaliwa kwao hadi alipoaga dunia (saw). Hata baada ya kuaga kwake dunia (saw) aliwataka wafuasi wake walinde heshima yake kupitia kizazi chake hicho kitukufu kwa kuwaambia: ''Lindeni heshima yangu enyi Ansar kupitia Ahlu Beit wangu."

Hivi ndivyo anavyonukuu Ibn Tawous katika kitabu chake cha at-Tarf. Naye Idlibi ananukuu katika kitabu chake cha Kashf al-Ghumma kupitia Tumama kwamba Mtume (saw) alimwambia Bilal: 'Eeh Bilal! Niletee wanangu Hassan na Hussein. Bilal akaondoka na baadaye akawa amerejea nao. Mtume akawa amewabeba kifuani kwake huku akiwa anawashumu. Imam Ali (as) akasema: Nilienda kuwatoa kifuani kwa Mtume naye akasema: Waache wanishumu nami pia niwashumu, wafaidike kwa kuniona, nami pia nifaidike kwa kuwaona. Hii ni kwa sababu watakumbana na masaibu na dhulma kubwa baada yangu. Mwenyezi Mungu awalaani wale wote watakaowatia woga na hofu. Ewe Mwenyezi Mungu! Ninawaweka kwenye hifadhi yako wawili hawa pamoja na baba yao."

*********

Nam, ndugu wasikilizaji, na katika fadhila na utukufu wa Imam wawili hawa ni kwamba Mwenyezi Mungu aliwaandalia mapokezi makubwa ya mbinguni ambapo Malaika Jibril aliteremka na habari ya kuzaliwa kwao pamoja na majina yao kutoka mbinguni. Malaika huyo wa Nuru aliteremka na kuwabashiria pepo na vilevile Mtume kuwaandalia karamu na sherehe maalumu. Hivi ndivyo zinavyosema riwaya takatifu na maalumu za Uislamu.

Kwa mfano kuna hadithi hii ambayo inasema kwamba siku moja Alkhamisi jioni ikiwa ni usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa, tarehe 5 au 3 ya mwezi mtukufu wa Shaaban mwaka wa Nne Hijiaria, Bibi Fatwimah alipatwa na machungu ya uzazi huku Mtume (saw) akiwa amesimama nje ya mlango wake. Baada ya muda Bibi Fatwimat az-Zahraa (as) akawa amejifungua mwanae Hussein (as), kabla ya alfajiri. Hapo nuru ikawa imedhihiri nyumbani kwake na pembeni yake palikuwa pameandikwa maneno matukufu yanayosema: (Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na uadilifu. Hapana awezaye kuyabadilisha maneno yake)….. Na mara tu Imam Hussein (as) alipozaliwa, Mtume (saw) alisema: (Shangazi!) Nileteeni mwanangu: Shangazi yake, Swafiyya (binti yake Abdul Muttalib) akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Bado hatujamnadhifisha (kumsafisha/kumuosha). Mtume (saw) akajibu: Eeh Shangazi! Kwani ni wewe utakayemnadhifisha?! Tayari Mwenyezi Mungu Mtukufu amekwishamnadhifisha na kumsafisha."

Na siku hiyo, Riwaya zinasema wapenzi wasikilizaji kwamba Mwenyezi Mungu alimwambia Malaika anayesimamia Moto auzime moto huo kutokana na utukufu wa Mtume Muhammad (saw) kubarikiwa mtoto duniani. Pia aliwamuru malaika wa mbinguni wasimame kwenye safu huku wakiwa wanasifu, kuhimidi na kumtukuza Mwenyezi Mungu kutokana na uzawa huo mtukufu. Vile vile Mwenyezi Mungu alimuamuru Malaika Jibril ateremke duniani huku akiwa ameandamana na malaika wengine elfu moja waliojaa furaha na bashasha kwenda kwa Mtume (saw) ili kumpasha habari ya jina atakalopewa mtoto huyo aliyezaliwa, ambalo ni Hussein. Hali kama hiyo pia ilijitokeza alipozaliwa Imam Hassan (as) kabla yake.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain kwa juma hili. Ni matumaini yetu kuwa mmenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi cha leo. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena wiki ijayo, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.