Jul 14, 2022 09:48 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Asslaama Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza kipindi kingine katika mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi, ambavyo vinawazungumzia wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) al-Hassan na al-Hussein (as).

Fadhila na utukufu wa Maimamu wawili hawa wapenzi wasikilizaji, umezungumziwa katika Aya kadhaa za Qur'ani Tukufu zikiwemo za Mawadda, Mubahala na Tat'hir. Fashila zao nyingine zimetajwa na kuzungumziwa kwa marefu na mapana katika Hadithi za Mtume Mtukufu (saw), ambaye aliwapenda sana na kuwaonyesha huruma na upendo wa hali ya juu huku akiwataka Waislamu wawapende pia na kuwalinda kutokana na mabaya. Hadithi hizo pia zinabainisha wazi namna Mtume (saw) alivyosifu na kufafanua fadhila zao nyingi katika Uislamu. Mtume amenukuliwa katika Hadithi nyingi namna alivyokuwa na upendo mkubwa kwa watukufu wawili hao na akimwomba Mwenyezi Mungu awapende na kuwachukia wale wote waliokuwa na chuki na uadui nao. Amenukuliwa akisema: 'Ninawapenda wawili hawa, hivyo nakuomba uwapende', au kama ilivyo katika riwaya nyingine: 'Wawili hawa ni wanangu na wana wa binti yangu. Allahumma! Ninawapenda, hivyo ninakuomba uwapende na umpende kila anayewapenda.'

Anas bin Malik amenukuliwa akisema Mtume (saw) aliulizwa: 'Je, ni Ahlul gani unaowapenda zaidi? Akajibu: 'Ni Hassan na Hussein.'

Anas anaendelea kusema: 'Mtume alikuwa akimwambia binti yake Fatwimah: 'Niitie wanangu wawili, na walipofika mbele yake alikuwa akiwashumu na kuwakumbatia.'

Hadithi hii imenukuliwa na Tirmidhi katika Sunan yake, Ibn Asakir katika kitabu cha Taarikh Dimashk, Ahmad bin Hambal katika Sunan yake, al-Haithami as-Shafi' katika Majmaul Bayyan na wengine wengi. Wote hao akiwemo an-Nasai wanasema kwamba Buraida ambaye ni sahaba mashuhuri amenukuliwa akisema: 'Siku moja Mtume (saw) alikuwa akihutubia, ambapo Hassan na Hussein walifika mahala hapo huku wakiwa wanatembea wakichechemea. Mtume aliteremka mara moja kutoka kwenye mimbar na kwenda kuwabeba. Aliwabeba mikononi ni kisha akasema: Niliwatazama watoto wawili hawa wakiwa wanatembea wakichechemea, lakini sikuweza kusubiri na ndipo nikakatiza hutuba yangu kwenda kuwabeba.'

**********

Nam wapenzi wasikilizaji, hivi ndivyo Mtume (saw) ambaye ni maasumu yaani amekingwa na Mwenyezi Mungu kufanya makosa na dhambi katika matendo yake yote ya kihisia na kidhahiri, alivyokuwa akionyesha mapenzi na upendo mkubwa kwa wajukuu wake hao watukufu. Je, Mtume alitosheka tu kwa kuwaonyesha huruma na mapenzi hayo hadharani? La hasha, bali daima alikuwa akiwaombea dua na kuwataka wafuasi wake na Waislamu wote wawapende akama livyokuwa akifanya yeye. Si hayo tu bali alikuwa akiwaombea dua za ushindi na kuwalaani wale wote waliowachukia, kuwadhulumu na kuwaua.

Hebu na tupitie hapa baadhi ya maneno ya mtukufu Mtume (saw) ambaye kitabu kitakatifu cha Qur'ani kinasema wazi kwamba hasemi lolote kutokana na matamanio yake bali ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kuwahusu wajukuu wake hao. Amepokelewa katika vitabu vingi vya Kiislamu vya madhehebu zote mbili kuu za Kiislamu akisema: 'Anayenipenda mimi na wawili hawa (yaani Hassan na Hussein) pamoja na baba na mama yao, atakuwa pamoja nami kwenye daraja langu siku ya Kiama.'

Hivi ndivyo anavyonukuu Asakir ad-Dimashki katika kitabu chake cha Tarikh ad-Dimashk. Naye Tabari ash-Shafi' anasema katika kitabu chake mashuhuri cha Dhakhair al-Uqba fi Manaqib Dhawil Qurba kwamba, Mtume Mtukufu (saw) alisema kuwahusu Hassan na Hussein: 'Mimi ninawapenda, hivyo wapendeni pia enyi watu! Na Mtume (saw) aliyasema hayo baada ya kuwashumu, ambapo walimkumbatia naye akawa amewakumbatia.'

***********

Ndugu wasikilizaji, Mtume Mtukufu ni Mtume wa rehema na huruma ambaye aliteuliwa na kutumwa kwa wanadamu na mwenyezi Mungu na bila shaka matendo na suna zake ni hoja kwetu sisi kwa ajili ya kuzitekeleza na kuzifuata kikamilifu. Watu wanapasa kutambua kwamba suna hizo ni wasia na matakwa ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Matamshi na maneno hayo ya Mtume yanaashiria na kubainisha wazi daraja ya juu ya utukufu walionao wajukumuu wawili hawa wa Mtume Imam Hassan na Hussein (as). Maneno hayo pia yanaweka wazi wajibu na ulazima wa kuwapenda na uharamu wa kuwapinga na kuwachukia.

Tabari anasema katika kitabu cha Dhakhair al-Uqba kwamba Mtume (saw) alisema kuwahusu watukufu wawili hawa (as): 'Wawili hawa ni  maua yangu mawili duniani, hivyo anayenipenda mimi na awapende pia.' Muttaqi al-Hindi anasema katika Kanzul Ummal kwamba Mtume (saw) alisema kuwahusu: 'Anayewapenda wawili hawa mimi humpenda na ninayempenda mimi, hupendwa na Mwenyezi Mungu na anayependwa na Mwenyezi Mungu, humuingiza kwenye Pepo ya Amani, na anayewachukia, mimi pia humchukia na ninayemchukia mimi huchukiwa pia na Mwenyezi Mungu na anayemchukiwa na Mwenyezi Mungu humuingiza kwenye Jahannam naye huko atapata adhabu kali!'

Wapenzi wasikilizaji, si ni wazi kwamba wokovu wa wanadamu na hasa Waislamu unapatikana katika kupenda na kuwafuata watukufu wawili hawa?! Na hasa tukiongezea hapa riwaya hii iliyonukuliwa na Sayyid Walii bin Ni'matullah al-Husseini katika kitabu chake cha Majmaul Bahrain fi Manaqib as-Sibtain ambapo Mtume amenukuliwa akinasihi na kuwashauri wafuasi wake kwa kusema: 'Anayetaka kushikamana na kishikio madhubuti, kisichovunjika cha Mwenyezi Mungu ambacho amekizungumzia katika kitabu chake kitakatifu basi na awafuate Ali bin Talib, na Hassan na Hussein kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu anawapenda kwenye Arshi yake.'

Al-Juwaini as-Shafi' anasema kwenye kitabu chake cha Faid as-Simtain fi Fadhail al-Murtadha Walbatul Walhussein kwamba mtu mmoja alifika mbele ya Mtume Mtukufu (saw) na kumwambia: 'Hakika mimi ninakupenda sana Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mtume akamuuliza: Je, unanipenda mimi tu?! Akajibu: Ndio ninakupenda wewe tu. Mtume (saw) akamtahadharisha kwa kusema: Hakika haunipenda mpaka unipende kupitia Ahlul Bait wangu.'

Ni kweli kabisa! Hii ni kwa sababu watukufu wawili hawa Imam Hassan na Hussein (as) ni vipenzi wa Allah na Mtume wake (saw). Ni uongo mtupu kwa mtu kudai kwamba anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) ilihali hawapendi watukufu wawili hao (as). Hii ni kwa sababu Mtume amesema sehemu nyingine: 'Msiingie kwenye nyumba ya watu nisiowapenda', akikusudia wawili hao! Az-Zarandi al-Hanafi anasema katika kitabu chake cha Nadhm Durar as-Simtain kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema wazi wazi kwamba: 'Mtu anayempenda Hassan na Hussein ataingia Peponi na anayewachukia ataingia Motoni.'

Salamu za Mwenyezi Mungu zimuendee Muhammad (saw) na Ali zake watoharifu (as).