Sibtain katika Qur'ani na Hadithi
Bismillahir Rahmanir Raheem. Assalam Aalikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni wakati mwingine wa kukutana nanyi tena wapenzi wasikilizaji katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambapo kipindi cha leo ni cha ishirini na nane katika mfululizo wa vipindi hivi, karibuni muwe nasi hadi mwisho wa kipindi.
Si katika tabia na maadili ya Mitume kujikalifisha na kuona uzito katika utekelezaji wa majukumu yao, kivitendo na kwa maneno kwa sababu hayo ndiyo maumbile yao ambayo hufungamana na ukweli na umaasumu kwa Baraka za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa maneno mengine ni kuwa maumbile yao safi yanatokana na kiwango cha juu cha imani, takwa na maarifa.
Na wazi kuwa Mtume Mtukufu (saw) aliamiliana na Ahlu Bait wake kwa huruma na mapenzi makubwa si tu kwa kuwa walikuwa Watu wa Nyumba yake bali pia walikuwa viongozi na mawalii wa Mwenyezi Mungu na pia wapendwa wake watukufu waliojitolea kulinda dini yake. Hao ni watukufu wenye ikhlasi kubwa ambao walijitolea na kutoa kila walichokuwanacho, wawe ni wapendwa au mali zao kwa ajili ya kutumikia dini ya Muumba wao. Tutazungumzia japo hili kwa urefu kidogo hivi punde, endeleeni kuwa nasi.
**********
Ndugu wasikilizaji, Tunasoma katika vitabu vya Dhakhair al-Uqba cha Tabari, Usud al-Ghaba cha Ibn Athir na vile vile Sahih Ibn Maja, Mustadrak cha Hakim Naishaburi as-Shafi' na vingine vingi katika marejeo ya Kisunni na Kishia kwamba, Ummul Fadhl, mkewe Abbas bin Abdul Muttalib ambaye ni ami yake Mtume (saw) alimwambia Mtume: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niliona kwenye ndoto kwamba moja ya viungo vyako kipo nyumbani kwangu! Mtume akamwambia: Umeota ndoto nzuri kwani hivi karibuni binti yangu Fatwimah atajifungua mtoto wa kiume na wewe utamnyonyesha maziwa ya Quthm ( ambaye ni mtoto wa kiume wa Ummul Fadhl), na hivyo atakuwa ni ndugu yake wa kunyonya.' Ummul Fadhl akasema: Fatwimah akawa amejifungua Hassan nami nikamyonyesha maziwa ya Quthm.
Naye Sheikh Swaduq ananukuu katika kitabu chake cha Aamali na Majlisi katika kitabu cha al-Bihar Hadithi kutoka kwa Imam Jaffar Swadiq (as) akisema kwamba Ummu Aiman hakupata usingizi katika moja ya nyusiku kutokana na kilio kilichompata. Hivyo Mtume (saw) akawa ameomba aitwe na kufikishwa mbele yake naye akamuuliza sababu ya kilio hicho. Alimwambia: "Nimeona usiku huu ni kana kwamba baadhi ya viungo vyako vimeanguka nyumbani kwangu! Mtume (saw) akamwambia: Lala bila ya kuwa na wasi wasi wowote kwa sababu Fatwimah atajifungua Hussein na wewe utamlea. Hivyo baadhi ya viungo vyangu vitakuwa nyumbani kwako."
Ndugu wasikilizaji, je, tunajifunza nini kutokana na Hadithi hii, iwapo kweli tunataka kuwa na maarifa sahihi kuhusu masuala ya kiakhlaki na kiitikadi katika dini? Je, si Hadithi hii inatwambia wazi wazi kwamba Imam Hassan na Hussein (as) wanatokana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) moja kwa moja? Na kutokana na ukweli kwamba Mtume (saw) ndiye mbora, mtukufu na mtoharifu wa viumbe vyote, si wawili hao nao pia ni hivyo hivyo kwa dalili kuwa wanatokana moja kwa moja na Mtume na kwamba wao ni sehemu ya mwili wa Mtume? Je, si maneno haya ya Mtume yana maana kwamba kufanyiwa uadui na kuchukiwa watukufu wawili hawa ambao ni wajukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ni kufanyiwa uadui na kuchukiwa Mtume mwenyewe kwa sababu wanatokana naye moja kwa moja? Ni wazi kuwa Mtume (saw) amenukuliwa sehemu nyingi akisema wazi wazi kwamba kuudhiwa wawili hawa ni sawa na kumuudhi yeye Mtume na kwamba kuwapenda wao ni sawa na kumpenda Mtume mwenyewe (saw).
Ahmad bin Hambal anasema katika kitabu chake cha Musnad, Suyuti katika ad-Durr al-Manthur na Tabarani katika Akhbar al-Hassan bin Ali kwamba Mtume (saw) huku akiwa ameshika pande mbili za mlango wa Fatwimah (as) aliwaambia Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein: Mimi ni salama kwa anayekuwa salama kwenu na mpiga vita anayekupigeni vita. Hadithi hii imepokelewa na Zaid bin Arqam ambapo pia imepokelewa na Abu Huraira ambaye anasema kwamba Mtume (saw) aliwaambia watukufu hao (as): 'Mimi ni mpiga vita anayekupigeni vita na ni salama kwa anayekuwa salama kwenu.'
************
Ndugu wasikilizaji hii ni moja ya hadithi mashuhuri ambazo zimezoeleka kusikika mara kwa mara katika Umma na jamii za Waislamu. Wakati huo huo kuna habari mashuhuri za kihistoria katika upande wa pili zinazotwambia kwa masikitiko makubwa jinsi baadhi ya watu waovu walivyompiga vita Imam Hassan (as), kumtenga na kumfungia nyumbani kwake na kisha kumuua kwa sumu huku wakiwa wanatambua vyema kwamba ni mjukuu wa Mtume (saw) aliyependwa sana na mtukufu huyo. Kadhalika kuna habari nyingi za kuaminika kihistoria zinazotufahamisha namna jeshi la Sham lilishirikiana na baadhi ya watu waovu katika mji wa Kufa nchini Iraq ya leo na kutuma askari wapatao elfu thelathini kwa ajili ya kwenda kumpiga vita mjukuu mwingine mpendwa wa Mtume, Imam Hussein (as) na kisha kumuua kinyama yeye pamoja na watoto, jamaa na masahaba zake. Hawakutosheka na hayo tu bali walikata kichwa chake kitakatifu na kisha kukitundika kwenye mkuki na kukitembeza kwa kejeli katika maeneo mengi, kutokana na chuki na uadui mkubwa waliokuwa nao dhidi ya familia na Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw).
Jambo hili lina maana gani wapenzi wasikilizaji? Tutauarifisha vipi msimamo wa Muawiyya, Yazid bin Muawiyya, Banu Umayyia na wasaliti wa Kufa isipokuwa kuuchukulia kuwa ulikuwa msimamo wa uadui na chuki dhidi ya Mtume Mtukufu (saw) pamoja na kumpiga vita yeye pamoja na Watu wa Nyumba yake? Bila shaka kama tulivyosama katika Hadithi tulizotangulia kusoma, Mtume na wajukuu wake wawili watukufu yaani Imam Hassan na Hussein (as) wanawapiga vita na kuwachukia wale wote waliowadhulumu na kuwaua kikatili, na daima wanamwomba Mwenyezi Mungu apate kuwahilikisha.
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Hadithi na Qur'ani ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kwamba mmepata kunufaika na yale tuliokuandalieni katika kipindi cha juma hili. Basi hadi wiki ijayo panapo majaaliwa yake Mwenye Mungu, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.