Jul 14, 2022 09:58 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Hiki ni kipindi cha 30 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kama vilivyokuwa vipindi vilivyopita kinazungumzia sifa na fadhila za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) ambao si wengine bali ni Imam Hassan na Hussein (as). Hawa ni wajukuu ambao kama tulivyoona katika vipindi vilivyopita walipendwa sana na Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume wake (saw) ambaye alitaja na kufafanua sifa na fadhila zao nyingi kupitia hadithi nyingi ambazo zimenukuliwa katika vitabu vingi vya Waislamu, na kuwataka pia wawapende na kuwafuata katika masuala yao ya kidini na kimaisha.

Jambo tunalopasa kufahamu na kulitambua vyema ni kwamba hali ya kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ni maasumu, yaani mtu asiyetenda kosa wala dhambi inatufanya sisi Waislamu tupate yakini kuwa Mtume hampendi mtu yoyote ila kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na wala hampendi mtu ila mtu huyo huwa amependwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Huwa hakengeuki mipaka katika kumsifu yeyote na kwa hivyo maneno yake huwa ni sunna ambayo huambatana kikamilifu na ukweli wa mambo ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu huwa ameuridhia.

Hivyo basi iwapo Mtume alibainisha na kufafanua sifa za Maimamu Hassan na Hussein (as), bila shaka alifanya hivyo kwa msingi wa aliyoyataka Mwenyezi Mungu na yaliyomridhisha. Ni wazi kuwa kwa kufanya hivyo, Mtume alitekeleza wajibu aliopewa na kuamrishwa na Mwenyezi Mungu autekeleze kisheria na kivitendo. Suala hili lina umuhimu mkubwa sana kwetu sisi Waislamu. Hii ni kwa sababu jambo hili huimarisha itikadi zetu kidini na kutufanya tufuate amri ya Mwenyezi Mungu, ya kupenda na kufuata Ahlu Bait wa Mtume wake (saw), suala ambalo bila shaka ni ushindi na mafanikio makubwa kwetu kwa kuwa litatuokoa na kutukinga na moto mkali wa Jahannam, Siku ya Kiama Inshaallah.

*********

Ndugu wasikilizaji, Sheikh Mufid (MA) ananukuu katika kitabu chake cha Ikhtisas kwamba Muawiyyah bin Abu Sufyan alimuandikia Imam Ali bi Abi Talib (as) barua ya vitisho, tuhuma na maneno makali naye Imam, akamjibu, baada ya kuanza kwa jila la Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kusema: 'Ewe Muawiyyah! Umesema uongo….. Mimi ni Ali bin Abi Talib na baba wa Hassan na Hussein…', hadi mwisho wa barua. Kuna ibara ya kuvutia sana katika barua hiyo nayo ni hatua ya Imam Ali (sa) ya kujisifu na kujifaharisha kutokana na kuwa ni baba wa Hassan na Hussein. Anajifaharisha na kujiarifisha kuwa ni baba wa wajukuu wawili hawa watukufu wa Mtume (as). Ni utukufu mkubwa ulioje walionao wajukuu hawa wa Mtume mbele ya Mwenyezi Mungu! Utukufu huo mkubwa ndio ulimfanya Amir al-Mu'mineen Ali (as) kujifaharisha na kujinasibisha kwa wajukuu hao kwa kuwa wana nafasi na fadhila kubwa mno mbele ya Mwenyezi Mungu.

Nam, hawa ndio wale wajuu wawili ambao Mtume aliwapenda sana na kuwasifia kwa maneno ya kuvutia ambayo yalikuwa hayajawahi kutamkwa tena na mtu mwingine yeyote.

Hafidh bin Asakir ad-Dimishki ash-Shafi' anasema katika kitabu chake mashuhuri cha Tarikh Madinat ad-Dimishk akimnukuu Hudhaifa bin al-Yamaan kwamba Mtume Mtukufu (saw) alimuuliza: 'Je, unajua nani alikuwa nami?! Hudhaifa akajibu: La. Akasema Mtume: Jibril amenikujia na kunibashiria kwamba hakika Hassan na Hussein ni Mabwana wa Vijana wa Peponi.'

Nam wapenzi wasikilizaji, huu ni wahyi alioteremshiwa Mtume (saw) kwa njia tofauti. Sio uteremsho wa Qur'ani bali ni Wahyi na habari ya Mwenyezi Mungu aliyoteremshiwa Mtume (saw) na kuizungumzia kwa njia tofauti sehemu nyingi katika jukumu lake la kuwafikishia wanadamu ujumbe kutoka kwa Muumba wao. Moja ya sehemu hizo ni ile ambayo imeashiriwa na Tabarani katika kitabu cha Akhbar al-Hassan bin al-Ali ambapo amemnukuu Omar bin al-Khattab kwamba Mtume (saw) alisema: 'Hassan na Hussein ni Mabwana wa Vijana wa Peponi.'

Vile vile Ibn Asakir anasema katika kitabu chake cha Tarikh ad-Dimishk, al-Haithami ash-Shafi' katika kitabu cha Maj'mau az-Zawaid na Tabarsi katika kitabu cha A'laam al-Warah bi A'laam al-Hudaa akimnukuu sahaba mwema Jabir al-Ansari kwamba Mtume Mtukufu (saw) aliwaambia sahaba zake: 'Mtu anayetaka kuwaona Mabwana wa Vijana wa Peponi basi na awatazame Hassan na Hussein.'

********

Wapenzi wasikilizaji hakuna shaka yoyote kwamba pepo ndiyo daraja na nafasi ya juu kabisa Akhera, na huko waumini ni vijana ambao ndio kwanza wako katika mwanzo wa ujana wao. Huko watafurahia kutokana na kwamba Mwenyezi Mungu amewaaneemesha na kuwapa radhi zake kwa kuwajalia kuwa miongoni mwa watu wa peponi. Hassan na Hussein ndio watakaokuwa mabwana wa vijana hao wa peponi ambapo moyo wa kila aliyeko kwenye pepo hiyo utafurahi na kuridhishwa kwa pambo la mabwana hao wa peponi.

Sheikh Majlisi anasema katika juzuu ya 43 ya kitabu chake cha Bihar al-Anwaar akimnukuu mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kisuni ambaye si mwingine bali ni Shiruyah Al-Dailami akisema katika kitabu chake cha Firdaus al-Akhbar akimnukuu Bibi Aisha kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: "Wakati watu wa Peponi watakapoingia humo, Pepo itamwambia Mwenyezi Mungu Mtukufu: Ewe Mwenyezi Mungu! Uliniahidi kunipamba kwa nguzo zako mbili. Hapo Mwenyezi Mungu ataijibu kwa kusema: Je, sikukupamba kwa Hassan na Hussein?"

Watukufu wawili hao wametajwa katika Hadithi nyingine maalumu kwamba wao ni pambo la Arshi ya Mwenyezi Mungu.

Sheikh Swadouq anasema katika kitabu chake cha Maani al-Akhbar akimnukuu Imam Ridha (as) katika Hadithi tukufu inayozungumzia kisa cha Nabii Adam na mkewe Hawaa (as) kwamba alisema: "Adam alipotukuzwa na Mwenyezi Mungu na Malaika kuamrishwa wamsujudie na kisha kuingizwa Peponi. Alijiuliza moyoni, je, kuna kiumbe mwingine ambaye Mwenyezi Mungu amemuumba na kumfanya kuwa bora kuniliko mimi? Hapo Mwenyezi Mungu alimwita na kumwambia: Ewe Adam! Inua kichwa chako na utazame misingi (miguu) ya Kiti changu cha Enzi (Arshi). Adam alipotazama misingi hiyo (miguu ya Kiti cha Enzi) aliona pameandikwa: La Ilaha Ila Allah, Muhammad Rusul Allah, Aliy ni Amir al-Mu'mineen, Fatwimah ni mbora wa wanawake wa ulimwengu na Hassan na Hussein ni Mabwana wa Vijana wa Peponi. Adam akauliza, je, hawa ni akina nani? Akaambiwa: Hawa ni katika kizazi chako na ni wabora kukuliko wewe na viumbe wangu wote na lau wasingekuwa wao, bila shaka nisingekuumba wewe, pepo, moto, mbingu wala ardhi."

Ndugu wasikilizaji, an-Nisaburi amendika katika kitabu chake cha Raudhat al-Waidhin kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: "Siku Kiama kitakapofika, Kiti cha Enzi (Arsh) cha Mwenyezi Mungu kitapambwa vilivyo na mimbari mbili zenye nuru na zilizo na urefu wa maili mia moja kuwekwa hapo, moja upande wa kulia na ya pili upande wa kushoto wa Arshi hiyo. Kisha Imam Hassan na Hussein (as) wataletwa na kuwekwa juu ya mimbari hizo. Mwenyezi Mungu atapamba Arshi yake kwa watukufu hao sawa na anavyofanya mwanamke kwa kujipamba kwa herini."

Au kama inavyoonekana katika Riwaya ya Sheikh al-Majlisi ambaye anamkukuu Abdallah bin Omar bin al-Khattab kwamba: "Kisha mimbari mbili zenye nuru na zilizo na urefu wa maili mia moja zitaletwa hapo. Moja itawekwa upande wa kulia na ya pili upande wa kushoto wa Arshi. Kisha Imam Hassan na Hussein (as) wataletwa, na Imam Hassan atasimamishwa upande mmoja wa mimbari naye Hussein upande wa pili wa mimbari hizo. Mwenyezi Mungu Mtukufu atapamba Arshi yake kwa watukufu hao kama anavyofanya mwanamke kwa kujipamba kwa herini."

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafika mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa leo. Ni matumaini yetu kwamba tumeweza kunufaika sote na yale tuliyokuandalieni kwenye kipindi hiki. Basi hadi tutakapojaaliwa tena kukutana katika kipindi kijacho, tunakuageni kwa kusema, kwaherini.