Aug 04, 2022 06:17 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hiki ni kipidi cha 31 katika mfululizo wa vipindi vya Sibtain ambavyo kama mnavyojua hujadili na kuzungumzia utukufu na fadhila za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) ambao ni Maimamu Hassan na Hussein (as) kwa msingi wa kitabu kitakatifu cha Qur'ani na Hadithi za Kiislamu.

Kuna mambo mawili ambayo yamezingatiwa na kujadiliwa kwa kina na wanahistoria na watafiti wengi wa masuala ya Kiislamu. Moja ni kuhusu Hadithi nyingi ambazo zimepokelewa kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) katika kusifu na kuwatukuza Ahlu Beit wake (as). Alibainisha na kufafanua fadhila, nafasi, vyeo na utukufu wao mbele ya Mwenyezi Mungu na kusisitiza ubora na Uimamu wao na hata kufungamanisha wokovu wa wanadamu na ufuasi wao (as). Al-Fital an-Nisaburi amesema katika kitabu chake cha Raudhat al-Waidheen na pia Ibn Shahrashub as-Sarwi katika kitabu cha Manaqib Aal Abi Talib kwamba Mtume Mukufu (saw) alisema: Anayetaka kupanda safina ya wokovu, kukamata kishikio madhubuti na kushikamana na Kamba imara ya Mwenyezi maungu, basi na ampende (amfuate) Ali baada yangu, amchukie adui yake na afuate Maimamu waongofu katika kizazi chake, kwani wao ndio makhalifa na mawasii wangu na hoja ya Mwenyezi Mungu katika viumbe baada yangu. Wao ndio mabwana wa Umma wangu wanaowaongoza wenye takwa kuelekea peponi. Kundi lao ni kundi langu na kundi langu ni kundi la Mwenyezi Mungu na kundi la maadui wao ni kundi la shetani.

Na huu wasikilizaji wapendwa ni wito wa wazi na wa moja kwa moja kwa ajili ya wanadamu kuwafuata Maimamu hawa wa haki na wongofu. Maimamu hao si wengine bali ni Ali, Hassan na Hussein na wengine tisa katika kizazi cha Imam Hussein (as). Hili ni jambo la kwanza. La pili ni kwamba kuna ishara ya wazi na isiyo na shaka yoyote katika wito ulioko kwenye Hadithi hii tukufu kuwa Mwenyezi Mungu anawataka waumini walioitwa kwenye njia hii wawafuate watukufu hawa ambao ni makhalifa na mawasii wa Mwenyezi Mungu na wakati huo huo hoja ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake duniani baada ya Mtume Mtukufu (saw). Wao ni viongozi wa waumini wenye takwa na wabora wa kundi la Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). Ni wazi kuwa kundi la maadau wao ni kundi la shetani.

Wapenzi wasikilizaji, je, kuna dalili nyingine iliyo wazi na ya moja kwa moja kuliko hii inayoashiria Uimamu wa Amir al-Mu'mineen na wanawe wawili al-Hassan na al-Hussein (as)?

Jambo jingine ambalo limewashangaza watafiti na wasomi wengi na kuwafanya walizingatie kwa makini katika Hadithi tukufu zilizopokelewa kutokwa kwa Mtume Mtukufu (saw) ni kuinukia katika ujana wake hali ya kuwa ni maasumu na aliyekingwa na matamamio na upotofu, jambo linalothibitisha sifa za utukufu na ukamilifu wake. Jambo hilo lilimfanya ajifaharishe kuwa baba wa wajukuu wake al-Hassan na al-Hussein (as) kama anavyoashiria mwanazuoni mashuhuri wa madhehebu ya Shafi, as-Sheikh Abdul ar-Rahman as-Swafuri al-Baghdadi kwa kusema: Niliona katika kitabu cha ad-Durr at-Thameen fi Khasais as-Swadiq al-Ameen, yaani Mtume (saw) kwamba alisema:  'Nitafufuliwa mimi na Manabii wengine katika kundi moja. Hapo mnadi atanadi: Enyi Manabii! Jivunieni baba wa watoto. Hapo nitajifaharisha mimi na watoto wangu wawili al-Hassan na al-Hussein."

Swali hili linajitokeza hapa wapenzi wasikilizaji kwamba je, Waislamu walipasa kuwachukulia vipi watukufu wawili hawa ambao Mtume Mtukufu ambaye ni kiumbe bora zaidi duniani alijifaharisha nao? Walipasa kuelekea wapi ili wapate kunufaika na uongozi bora wa mbinguni baada ya kuaga na kuondoka duniani Mtume Mtukufu (saw)? Bila shaka wajukuu wawili hawa ni miongoni mwa viongozi wa mbinguni ambao ni watukufu na wabora zaidi miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu. Wako karibu zaidi na Mwenyezi Mungu na walishabiaha zaidi na babu yao ambaye ni Mtume Mtukufu (saw) na bila shaka walikuwa wajuzi zaidi wa mafundisho ya dini na makatazo pamoja na maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Muungu Muumba alipawa fadhila na utukufu mkubwa wa kuwawezesha kuwaongoza wanadamu kwenye njia nyoofu na isiyo na upotofu. Wajukuu wawili hawa walifanana sana katika sifa nyingi na babu yao Mtume Mtukufu. Huenda moja ya sababu za Mwenyezi Mungu kuwashabihisha na Mtume ni kuwa alitaka wanadamu na Waislamu wakumbuke, wazingatie na kuhuisha thamani na matukufu ya kidini ya Mtume Mtukufu kupitia wajukuu wake hao wema ambao waliumbwa kutokana na nuru moja ya utukufu wa Mtume kupitia wazazi wao wawili Bibi Fatwima binti yake Mtume na Imam Ali (as) ambaye ni mtoto wa ami yake (saw). Hiyo ndio maana Mwenyezi Mungu alitaka wajukuu wawili hawa wa Mtume waenziwe, watukuzwe na kuheshimiwa kwa kufuatwa katika masuala ya kidini kama Maimamu.

Al-Muttaqi al-Hindi anasema katika kitabu cha Kanzul Ummal, Tabarani katika al-Mu'jam na Ibn Naeem katika Hilyat al-Auliyaa kwamba Ali Amir al-Mu'mineen alisema: 'Anayetaka kumuona mtu anayefanana zaidi na Mtume tokea shingoni hadi kwenye uso wake na amtazame Hassan bin Ali na anayetaka kumuona mtu anayefanana zaidi na Mtume (saw)  kimaumbile na kirangi tokea kwenye shingo hadi kwenye visigino (miguuni) vyake basi na amtazame Hussein bin Ali (as).'

Ndugu wasikilizaji, Ibn Hajar al-Askalani as-Shafi' anasema katika kitabu chake cha al-Iswabatu fi Tamyeeez as-Swahaba kwamba Anas bin Malik alisema: Hassan na Hussein ndio waliofanana zaidi na Mtume (saw), kati yao (masahaba). Tirmidhi anasisitiza katika kitabu chake cha Swahih, Ibn Hambal katika Musnad, Ibn Hubban katika Swahih yake, ad-Dulabi katika ad-Dhuriyyat at-Tayyiba, Ibn Abd al-Birr katika al-Istia'ab na wengineo katika vitabu vyao maalumu kwamba Hassan na Hussein walishabihiana sana na Mtume katika maumbile na sifa zake za kimwili seuze katika tabia na maadili yake kadiri kwamba Hani bin Hani alimnukuu Imam Ali (as) akisema: 'Hassan alishabihiana sana na Mtume (saw) tokea kwenye kifua hadi kichwani kwake naye Hussein alishabihiana naye sana tokea hapo kwenda chini.'

Kuna dalili nyingi zinazothibitisha kwamba kushabihiana huko kwa Mtume na wajukuu wake wawili hao ilikuwa hoja tosha kwa Waislamu ili wapate kuwalinda, kuwaheshimu na kufuata uongozi wao katika masuala ya kidini.

Moja ya dalili hizo ni ile iliyonukuliwa na Bukhari katika kitabu cha Swahih, na vile at-Tirmidhi, Ahmad bin Hambal, al-Mutaqqi al-Hindi, Abu Naeem na wengineo katika vitabu vyao maalumu. Wote hao ni wanazuoni mashuhuri wa Kisuni ambao walibobea katika masuala ya hadithi za Kiislamu. Wote wamemnukuu Anas bin Malik akisema: 'Abaidullah bin Ziad alikuja akiwa amebeba kichwa cha Hussein bin Ali kwenye jibakuli na hapo akawa anakikejeli lakini pamoja na hayo akasema wema fulani kumuhusu. Alisema: Na Hussein alifanana zaidi na Mtume wa Mwenyezi Mungu kuliko wengine wote na alikuwa mcheshi sana.'

Na riwaya ya pili wapenzi wasikilizaji, imenukuliwa na Sheikh Swadouq (Mwenyezi Mungu ainue nafasi yake) katika kitabu chake muhimu cha Ilal as-Sharaye' kuhusu sababu ya Ashura kuchukuliwa kuwa siku yenye huzuni na msiba mkubwa zaidi katika umma wa Kiislamu. Imam Swadiq (sa) aliulizwa swali kuhusiana na suala hilo naye akajibu kwa kusema: 'Hilo linatokana na kuwa Ahlul Kisaa (Watu wa Shuka) ambao walikuwa viumbe watukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu walikuwa watano. Mtume (saw) alipoaga dunia, Amir al-Mu'mineen, Fatwimah, Hassan na Hussein (as) walibakia miongoni mwa watu na hivyo kuwa faraja na tulizo la moyo kwao. Fatwimah (as) alipoaga dunia, Amir al-Mu'mineem Hassan na Hussein (as) waliachwa nyuma na hivyo kuwa faraja na tulizo la moyo kwa watu. Amir al-Mu'mineen (as) alipoaga dunia, Hassan na Hussein ndio waliobakia na hivyo kuwa faraja na tulizo la moyo kwa watu. Hassan (as) alipoaga dunia watu waliendelea kupata faraja na tulizo la moyo kutoka kwa Hussein (as). Lakini alipouawa Hussein (as) hakukubakia tena mtu mwingine miongoni mwa Ahlul Kisaa ambaye angewapa watu faraja na tulizo la moyo. Hivyo kuaga kwake dunia kulikuwa mfano wa kuaga dunia Ahlul Kisaa wote kama ambavyo kuwepo kwake kulikuwa sawa na kuwepo Ahlul Kisaa wote. Hivyo kuaga kwake dunia ulikuwa msiba mkubwa zaidi (kwa Waislamu duniani).

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa juma hili. Basi hadi wakati mwingine panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alayukum Warahmatullahi Wabarakatuh.