Aug 04, 2022 06:35 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahilim Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 36 ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho huwa kinazungumzia sifa, fadhila na utukufu wa wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu ambao si wengine bali ni Imamain al-Hassan na al-Hussein (as). Ni matumaini yetu kuwa kama vilivyokuwa vipindi vilivyopita, kipindi hiki pia kitatunufaisha zote kutokana na yale tutakayoyasikia humu, kari

Wajukuu wawili hawa walipendwa sana na Mtume (saw) na kunufaika pakubwa na upendo wake mtakatifu wa kinabii, kwa sababu yeye ni maasumu katika hali na vipaji vyake vyote vya kielimu, kiakili, kimaarifa, na katika roho, nafsi, ibada na miamala yake na watu. Haikutoka kwake ila haki na heri na matendo yake yote matukufu yalikuwa kwa ajili ya utiifu na kupata radhi za Mwenyezi Mungu, Mtukufu.

Wapenzi wasikilizaji, huyu ndiye Mtume mwongozaji (saw) ambaye aliwapenda sana wanawe Hassan na Hussein kwa sababu walikuwa nuru na mwanga wa Mwenyezi Mungu, na waliotokana na binti yake mtoharifu Fatwimat az-Zahra na mwana wa ami yake, ndugu, walii, mrithi na nafsi yake Mtume al-Imam Ali (as), kama inavyoashiria wazi ukweli huo Aya ya al-Mubahala. Wajukuu wawili hao walimrith babu yao katika sifa zake zote njema na toharifu na vilevile katika uimamu na uwasii ambao ni uongozi wa umma wa Kiislamu baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw). Je, ni vipi Mtume wa Allah (swt), mwenye hisia takatifu na laini zaidi, atakosa kuwa na shauku juu ya mawili hao wema (as)?

Sheikh at-Tarihi anamnukuu katika kitabu cha al-Muntakhab Umm al-Mu'mineen Ummu Salama akisema kwamba siku moja alikuwa na Mtume (saw) ambapo Hussein ambaye wakati huo alikuwa mtoto wa miaka mitatu na miezi kadhaa alifika mahala hapo naye Mtume (saw) akamkaribisha kwa kusema: 'Karibu kipenzi changu na tunda la moyo wangu.'

Walipokuwa wakitembea Hussein alimrukia kifuani Mtume (saw) naye kidogo akawa amepunguza mwendo wake. Ummu Salama akahisi kwamba Mtume alikuwa amechoka na akaamua amtake Hussein ateremke kutoka kifuani kwa babu yake. Hapo Mtume akamwambia: Mwache ewe Umma Salama! Atateremka atakapotaka kufanya hivyo mwenyewe. Elewa kwamba mwenye kumdhuru hata unywele mmoja huwa amenidhuru mimi.'

Ibn Asakir ameandika katika kitabu cha Tarikh ad-Dimashq, Hakim Naisaburi katika Mustadrak ala Swahihain, Ibn Kathir katika al-Bidaya wa an-Nihaya na wasomi wengine kwamba Mtume alikuwa akiwatengea Hassan na Hussein (as) wakati maalumu wa kucheza nao. Hadithi kuhusiana na suala hili pia imenukuliwa na al-Khawarazmi al-Hanafi katika kitabu cha Maqtal al-Hussein (as) kupitia Abu Huraira. Abu Huraira anasema katika Hadithi hiyo kwamba Mtum alishika mikono ya Hassan na Hussein (as) na kuwaambia wapande juu. Walipopanda kwenye miguu yake mitakatifu (saw) Mtume aliwanyanyua hadi kifuani kwake na kisha kuwaambia wafungue midomo yao na kisha akaibusu huku akiwa anasema: 'Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika mimi ninawapenda wawili hawa hivyo wapende.'

Kuna Hadithi katika kitabu cha Durr al-Manthur cha Hafidh as-Suyuti as-Shafi', Swahih ar-Ramzi, Sunan Nasai na vingine vingi inayosema kuwa siku moja Mtume (saw) alikuwa akihutubu msikiti ghafla Hassan na Hussein (as) wakawa wameingia msikitini hapo huko wakiwa wanachechemea. Mtume alisikia kilio chao na kuteremka haraka kutoka kwenye mimbar kwenda kuwachukua ambapo aliwabeba na kuwapakata kisha akarudi nao kwenye mimbar na kuwahutubu watu kwa kusema: 'Enyi watu!...Niliwaona watoto hawa wakiwa wanatembea kwa kuchechemea nami sikuweza kusubiria hilo na nikakatisha hotuba yangu ili kwenda kuwabeba.' Kisha alisema: 'Watoto wetu ni maini yetu yanayotembea duniani.'

Na haya yote wapenzi wasikilizaji ni mambo yanayotoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye ni maasumu na aliyekingwa kufanya dhambi. Vitendo hivyo vyote vinathibitisha wazi kuwa wajukuu wawili hawa wa Mtume wana hadhi na nafasi muhimu na tukufu mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). Vinatuthibitishia kwamba Mwenyezi Mungu amewatengea nafasi ya juu kiuongozi ambayo inapaswa kuzingatiwa na kuheshimiwa na Waislamu wote. Je, kuna dalili yoyote ya kuthibitisha hilo?

Allama Majlisi anasema katika kitabu cha Bihar al-Anwar kutoka katika kitabu cha Kifayat al-Athar cha al-Khazzaz kwamba siku moja Hassan na Hussein waliugua naye Mtume (saw) akawa amehuzunishwa sana na hali yao. Aliamua kwenda kuwatembelea na baada ya kuwachukua na kuwabusu alinyanyua mbinguni mikono yake mitakatifu na kuwaombea dua ifuatayo ya kuwakinga na shari na mabaya:

'Ewe Mola Mlezi wa mbingu saba na vilivyo chini ya kivuli chake! Mola Mlezi wa pepo na vinavyopeperushwa nao! Ewe Mola Mlezi wa kila kitu! Wewe ndiye wa kwanza na hakuna kilichoko kabla yako, wewe ndiye wa batini (ndani/kina) na hakuna kilichoko ndani zaidi yako. Wewe ni Mola wa Jibril, Mikaeli na Israfil na Mungu wa Ibrahim, Is-haq na Yaaqub. Nakuomba uwape afya na salama yako, uwaweke chini ya ulinzi na usimamizi wako na uwaepushe na maovu na mabaya kwa baraka na rehema zako.'

Kisha Mtume (sa) aliweka mkono wake mtukufu juu ya bega la al-Hassan (as) na kumwambia: 'Wewe ni Imam na mtoto wa Walii wa Mwenyezi Mungu.' Kisha akaweka mkono wake mtukufu kwenye mgongo wa al-Hussein (as) na kumwambia: 'Wewe ni Imamu na baba wa Maimamu tisa wema watakaotokana na kizazi chako. Wa tisa wao ndiye atakayekuwa kiongozi wao wa mwisho (wa zama). Mwenye kushikamana na nyinyi na Maimamu katika kizazi chenu, atakuwa pamoja nasi Siku ya Kiama, na pamoja nasi Peponi katika safu zetu.'

Hivi ndivyo Mtume Mtukufu (saw) alivyojali, kulinda na kuwazingatia sana wajukuu wake wema al-Hassan na al-Hussein (as) ambao aliwachukulia na kuwataja kuwa maua mawili ya moyo wake mtukufu. Alijali na kuwazingatia sana pia kutokana na kuwa walikuwa mawalii na warithi wa ujumbe wake wa mbinguni baada ya baba yao mpendwa al-Imam Ali (as). Wao ndio waliobeba mzigo wa kueneza ujumbe wake wa mbinguni na kulinda dini tukufu ya Mwenyezi Mungu hadi walipouawa shahidi kwenye njia hiyo.

Sheikh Swadouq (Mwenyezi Mungu amrehemu) anasema katika kitabu chake cha Aamali kwamba kabla ya kuaga kwake dunia, Mtume (saw) alikutana na Ahlul Bayt wake yaani Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein na kusema: 'Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika wewe unajua kwamba hawa ndio Ahlul Bayt wangu, na ambao ndio watukufu zaidi kwangu. Hivyo mpenda mwenye kuwapenda, mchukie anayewachukia, wasaidie na kuwaunga mkono wale wanaowasaidia na kuwaunga mkono (wanaowatetea), kuwa adui wa wale wanaowafanyia uadui, wanusuru wanaowanusuru na watakase kutokana na uchafu wote, wakinge kutokana na dhambi na waimarishe kupitia roho yako takatifu.'

Kisha alimuusia Ali kuhusu Fatwima na watoto wake wawili kwa kusema: 'Ewe Ali! Fatwimah ni sehemu ya mwili wangu, nuru ya jicho langu na tunda la moyo wangu. Kinachomkasirisha yeye hunikasirisha mimi na kinachomfurahisha yeye hunifurahisha mimi pia……Ama Hassan na Hussein, wao ni watoto na maua yangu mawili. Wao ni mabwana wa vijana wa Peponi. Wanapasa kuwa mfano wa macho na masikio matukufu kwako.'

Kisha Mtume Mtukufu (saw) alinyanyua juu mikono yake na kusema: Allahumma! Shuhudia ya kwamba ninampenda anayewapenda, kumchukia anayewachukia, ni salama kwa anayekuwa salama kwao (anayewadhaminia usalama na amani), ntapiga vita anayewapiga vita, kuwa adui wa anayewafanyia uadui na kuwa rafiki wa anayewaonyesha urafiki.'

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho tunatumai kimekunufaisheni vya kutosha. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena juma lijalo, hatuna la ziada ila kukuageni nyote kwa kusema, kwaherini.