Aug 04, 2022 06:43 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni katoka mjini Tehran. Karibuni kusikilizaji sehemu ya 40 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambavyo huangazia fadhila na sifa za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) ambao ni Imamain Hassan na Hussein, wajuu ambao walipendwa sana na Mtume na ambaye aliwausia Waislamu wote wawapende, waheshimu utukufu wao na kuwalinda kutokana na madhara.

Kama tulivyotangulia kusikia katika vipindi vilivyopita, watukufu hao na kizazi chote cha Nyumba ya Mtume (saw) ndio viumbe bora na wenye fadhila nyingi zaidi kati ya viumbe wote wa Mwenyezi Mungu. Babu yao ambaye ni Mtume Mtukufu (saw), baba yao ambaye ni mrithi na Kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume, mama yao ambaye ni mbora wa wanawake wa ulimwengu na Maimamu wote tisa waliotokana na kizazi cha cha Imam Hussein (as). Ni watukufu katika ulimwengu huu na katika Akhera kwa kuwa wao ndio mabwana wa vijana wa peponi.

Uongozi ni jambo lililothibitishiwa Ahlu Bait wa Mtume Mtukufu (saw), tokea Mtume mwenyewe Muhammad al-Mustafa (saw), hadi kufikia Imam wa Zama Imam Mahdi (af), anayesubiriwa kwa hamu kubwa na Waislamu.

Wapenzi wasikilizaji iwapo tunataka kuzungumzia sifa na fadhila za Maimamu wawili watukufu Hassan na Hussein (as), ni wazi kuwa tutalazimika kupitia vitabu vingi ambavyo vimeandikwa na Waislamu wa madhehebu zote za Kiislamu na ambavyo vimezungumzia kwa marefu na mapana sifa na fadhila hizo.

*********

Wajuzi na wasomi wa Hadithi na historia wanasema kuwa Mtume Muhammad alithibitisha kizazi halisi cha useyyid (usharifu) katika Uislamu kupitia mjukuu wake Mtukufu Hassan (as). Hii ni kutokana na ukweli kuwa Imam huyo alitokana na kizazi bora zaidi cha wanadamu duniani kwa sababu babu na wazazi wake wawili ndio viumbe bora zaidi katika kizazi cha mwanadamu duniani. Kwa maneno mengine ni kuwa hakuna mtu aliye na babu bora duniani mfano wa Muhammad al-Mustafa (saw) wala aliye na wazazi wawili bora zaidi kama Imamu huyo kwa sababu baba na mama wazazi wake ni Imam Ali na Bibi Fatwimah (as). Kwa maelezo hayo Imam Hassan al-Mujtaba (as) ndiye Sayyid wa kwanza katika sifa na fadhila zake, imani, akhlaqi, takwa, misimamo na Uimamu wake. Waislamu wote wameafikiana na kukubali usayyid wake na wa ndugu yake Imam Hussein (as). Ibn Sa'd anasema katika kitabu cha Tabakaat al-Kubra kupitia Abu Bakra kwamba alisema: 'Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akiwa juu ya mimbar huku Hassan (as) bin Ali akiwa pembeni yake. Alikuwa akawajia watu wakati mmoja, na mwingine akienda kwa Hassan na kusema: “Hakika mwanangu huyu ni sayyid (bwana), huenda Mwenyezi Mungu akasuluhisha baina ya makundi mawili ya Waislamu kupitia kwake.” Na katika riwaya nyingine bali katika riwaya kadhaa ni kuwa Mtume Mtukufu (saw) alisema: “Huyu mwanangu ni bwana, na hakika Mwenyezi Mungu atayarekebisha makundi mawili ya Waislamu kupitia kwake.” Na katika riwaya nyingine: “Na huenda Mwenyezi Mungu akarekebisha kupitia mikononi mwake makundi makubwa mawili ya Waislamu.''

Hadithi hii pia imepokelewa kwa wingi ndugu wasikilizaji katika vitabu vingine vingi vya Hadithi katika mlango wa sifa na fadhila za Imam Hassan (as) na vilevile katika vitabu vya historia kikiwemo kitabu cha Maqtal al-Hussein (as) cha Khawarazmi al-Hanafi katika mlango wa fadhila za Hassan na Hussein (as). Ama kuhusu ubwana na usayyid (kizazi cha Mtume) wa Imam Hussein (as) ndugu wasikilizaji, vitabu vya Kifayatul Athar cha al- Khazzaz, Uyun Akhbar ar-Ridha cha Swadouq, Maqtal al-Hussein cha Khawarazmi, Bihar al-Anwar cha Sheikh al-Majlisi na vingine vingi vinanukuu Hadithi ambayo inasema kwamba siku moja Salman Farsi, sahaba mashuhuri wa Mtume alikwenda kwa Mtume (saw) ambapo alimkuta akiwa anawapa chakula wajukuu wake wawili Hassan na Hussein. Alikuwa akiweka tonge la chakula wakati mmoja katika kinywa cha al-Hassan, na wakati mwingine katika kinywa cha al-Husayn. Tulipomaliza kula, Mtume alimbeba Hassan begani kwake na kumuweka Hussein juu ya paja lake, kisha akasema: “Ewe Salman! Unawapenda hawa?” Salman akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Vipi nisiwapende ilihali mahali pao kwako ni mahala pao. Akasema Mtume (saw): ''Ewe Salman! Yeyote anayewapenda huwa amenipenda mimi, na anayenipenda mimi huwa amempenda Mwenyezi Mungu''.

Kisha Mtume (saw), alibusu macho na mdogo wa Hussein na kuweka mkono wake juu ya bega lake na kumwambia: “Ewe Hussein! Wewe ni bwana (sayyid-kizazi cha Mtume), mwana wa Sayyid na baba wa Masayyid, wewe ni Imamu, mtoto wa Imam, na baba wa Maimamu. Wewe ni Hujjah mwana wa Hujjah na baba wa Mahujja tisa watakaotokana na kizazi chako ambao ni Maimamu wema, walinda-amana maasumu (ambao hawatendi dhambi), wa tisa ni Qa’im wao. Hivyo basi, heri wale wanaowapenda, na ole wao wanaowachukia).''

************

Na sasa ndugu wasikilizaji ni vyema tufahamu zaidi usayyid wa Maimam Hassan na Hussein (as) usayyid ambao Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu (saw) aliukariri na kuwasisitizia Waislamu mara nyingi mno, jambo ambalo bila shaka limezungumziwa na kujadiliwa kwa mapana na marefu na wanahistoria, wasomi na wataalamu wa Hadithi za Kiislamu. Je, jambo hili haliashirii kwamba usayyid ni baadhi ya sifa zinazoonyesha na kuthibitisha ubora wao juu ya watu wengine katika kuchukua nafasi ya ukhalifa na uongozi wa umma wa Kiislamu baada ya Mtume (saw)? Huu ni ukweli wa wazi ambao akili, uadilifu na elimu sahihi inakubaliana nao. Dini tukufu ya Uislamu pia inakubaliana nao katika misingi na matawi yake ya dini. Pia Ahlul Bait wenyewe wa Mtume (saw) wamekubali na kuthibitisha jambo hili lenye umuhimu mkubwa. Imam Hassan al-Mujtaba (as) anasema: "Enyi watu, anayenijua mimi basi amenijua, na asiyenijua, mimi ni Hassan bin Ali bin Abi Talib binamu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu, ambaye ni Mwislamu wa kwanza. Mama yangu ni Fatima, binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Babu yangu ni Muhammad bin Abdullah, Mtume wa rehema. Mimi ni mtoto wa anayebashiria habari njema, mimi ni mtoto wa mwonyaji, mimi ni mtoto wa taa yenye nuru, mimi ni mtoto wa aliyetumwa kuwa rehema kwa walimwengu... Mimi ni mtoto wa mwenye kujibiwa dua yake, mimi ni mtoto wa muombezi mtiifu.

Mimi ninatokana na moja ya makabila bora kabisa, na baba zangu ni watukufu zaidi kati ya Waarabu. Wakati wa kuhesabiwa, fahari, nasaba bora na uungwana (utu) ni wetu. Sisi tunatokana na mti bora zaidi unaotesha matawi yanayonawiri, matunda safi na miili madhubuti inayosalia, ambamo humo mna chimbuko la Uislamu na elimu ya utume…. Fahari inapofika (inapojadiliwa) sisi ndio huwa wa kwanza kwa ubora na tunapozuiwa kufikia ubora wetu, sisi huutafuta ubora huo. Sisi ni bahari zenye kina kirefu, zilizojaa na ambazo hazijawahi kuwa tupu, na milima madhubuti ambayo haiwezi kushindwa.

Enyi watu! Lau mngetafuta kilicho baina ya hivi na hivi, mngemkuta mtu ambaye babu yake ni Nabii, wala hamtampata ila mimi na ndugu yangu."

Naam, wasikilizaji wapenzi haya ndiyo maneneo aliyoyatamka Imam Hassan al-Muhtaba kuhusu sehemu ndogo tu ya sifa na fashila za Ahlul Bait wa Mtume (sa). Anaashiria sehemu ndogo tu ya fadhila na sifa ambazo anazo yeye pamoja na ndugu yake Imam Hassan (as) na kwa ufupi Maimamu wengine wote watoharifu ambao wanatokana na chimbuko moja la utukufu wa mbinguni.

 Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana nanyi tena katika kiupindi kingine juma lijalo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.