Aug 04, 2022 06:48 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiwahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran na karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ni na Hadithi, ambacho huzungumzia sifa na fadhila za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) al-Hassan na al-Hussein kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na Hadithi za kuaminika za Kiislamu.

Wasikilizaji wapendwa, Imam Hassan na Hussein (as) wana sifa na fadhila za kipekee kinasaba ambazo si rahisi kupatikana kwa mtu mwingine yeyote. Ya Kwanza ni kuwa wao ni wajukuu wa kiumbe bora zaidi duniani amabye si mwingine bali ni Mtukufu Mtume wa Uislamu Muhammad al-Mustafa (saw), baba yao ni Ali lango la elimu na kipimo cha haki na batili na mama yao ni mbora wa wanawake wa dunia waliotangulia na waliokuja baada yake (as). Kwa kuzingtatia hilo, inakuwa vigumu kwa mtu kubainisha kwa haki sifa zote za watukufu hawa ambao wanatokana na kizazi safi cha Mtukufu Mtume (saw).

Pamoja na hayo yote wapenzi wasikilizaji na licha ya sifa na fadhila zote waliozukuwa nazo watukufu hao wa Nyumba ya Mtume (saw), lakini iliwapata misiba, mateso na masaibu makubwa ya kutisha ambayo Mtume alikuwa akiyahofia kutoka kwa umma huu. Mtume alionya na kutahadharisha sana kuhusiana na suala hili lakini watawala waliotwa kwa nguvu uongozi wa umma wa Kiislamu baada yake waliyapuuza hayo yote na kuwafanyia watukufu hao ukatili na maovu makubwa.

Kumeandikwa katika kitabu cha al-Mustadrak cha al-Hakim al-Nishaburi al-Shafi', al-Irshad cha Sheikh Mufid na Bihar Al-Anwar cha Sheikh Al-Majlisi kwamba Mtume Mtukufu (saw) siku moja alienda kumtembelea binti na kipenzi chake, Fatwimah al-Zahra (as) nyumbani kwake ambapo alikaa na kuzungukwa na binamu na wasii wake Ali pamoja na wajukuu wake wawili, Hasan na Hussein (as), na akala chakula pamoja nao.

Alipomaliza kula, Imam Ali (as) alinyanyuka na kummiminia maji mikononi mwake, naye akawa amefurahi na kuridhishwa sana nao. Akiwa katika hali hiyo, Malaika Jibril aliteremka na kumpasha habari fulani. Mtume (saw) akawa amehuzunika sana, akainuka na kutawadha na kisha akatazama upande wa kibla na kuswali rakaa kadhaa pamoja na kuomba dua, na alipokuwa katika sajda yake ya mwisho alilia sana na kuirefusha sajda hiyo. Machozi yalimtoka kwa wingi, kisha akainua kichwa na kumvuta Hussein kwake, huku akibusu mahali ambapo angepigwa panga na maadui wa Uislamu na kulia sana. Hakuna aliyethubutu kumuuliza juu ya hilo isipokuwa Hussein(as). Alipanda juu ya mapaja ya Mtume, na kukiweka kichwa chake kifuani kwake, akakiweka kidevu chake juu ya kichwa cha babu yake na kumuuliza: Eeh Baba! Nimekuona ukifanya jambo ambalo nilikuwa sijawahi kukuona ukilifanya. Uliingia nyumbani kwetu, nasi tukawa tumefurahi sana kiwango ambacho tulikuwa hatujawahi kukifurahia tena, kisha ukalia kwa huzuni kubwa. Je, ni nini kilikufanya ulie? Akasema (saw): "Mwanangu! Nilikutazameni leo nami nikawa nimefurahishwa sana nanyi furaha ambayo nilikuwa sijawahi kuwa nayo tena kukuhusuni. Muda si muda kipenzi changu Jibril aliteremka na kunipasha habari kwamba mtauawa na makaburi yenu kutawanyika. Hilo lilinihuzunisha lakini nikasmhukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo, kisha nikamwomba akujaalieni heri."

Siku moja Mtume Mtukufu (saw) alikuwa ameketi pembeni ya Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein (as). Kisha Mtume (saw) aliwatazama na kusema: "Mtafanya nini mtakapoaga dunia na kuzikwa hali ya kuwa makaburi yenu yametawanyika kila upande? Imam Hassan (as) akauliza: Je, Tutakufa kifo cha kawaida au tutauawa? Mtume (saw) akamjibu: Eeh mwanangu! Wewe utauawa kidhalimu kwa sumu naye ndugu yako (Hussein) atauawa shahidi hali ya kuwa na kiu kikali. Baba yako pia atauawa kidhulma na watoto wenu kutawanyika katika pembe tofauti za dunia. Imam Hussein (as) akauliza: Je, ni nani hao watakaotuua? Mtume (saw) akajibu: Watu waovu zaidi duniani. Imam Hussein akauliza tena: Je, kuna watu watakaotuzuru? Mtume (saw) akajibu: Ndio, kundi moja katika umma wangu litanifanyia wema na ihsani mimi kwa kukuzuruni nyinyi. Siku ya Kiama itakapofika nitaenda upande wao na kuwanusuru kutokana na woga na hofu ya siku hiyo."

Nam, Mtume Mtukufu (saw) alimjibu kuhusu wale watakaozuru makaburi yao, wakayachunga na kuyakarabati licha ya kutawanyika sehemu tofauti kwa kusema: "Eeh mwanangu! Wao ni kundi katika umma wangu ambao wananitakia wema na kutaka kujiunga nami. Kwa kufanya hivyo watakuwa wanatafuta baraka na wala hakuna atakayefanikiwa kunizuru mimi, baba yako, kaka yako na wewe mwenyewe isipokuwa wakweli katika umma wangu."

Kisha Hussein (as) akamuuliza: "Eeh baba! Je, ni malipo gani atakayoyapata mtu anayekuzuru? Mtume (saw) akajibu: Eeh mwanangu! Mtu anayenitembelea nikiwa hai au maiti- yaani siku za uhai wangu au nitakapokuwa nimeaga dunia – atapata Pepo, anayemzuru baba yako atapata Pepo, anayemzuru kaka yako atapata Pepo na atakayekuzuru wewe baada ya kuaga kwako dunia atapata Pepo. Utakuwa wajibu wangu kumzuru Siku ya Kiama katika eneo watakalosimamishwa watu na kumshika mkono ili kumnusuru kutokana na mafadhaiko na mashaka ya siku hiyo pamoja na kumuondolea madhambi yake."

Nam, ndugu wapenzi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) hakuondoka humu duniani ila baada ya kuiaga familia yake kwa uchangamfu na wakati huo huo akiwa na huzuni kubwa. Hata aliwatabiria kile ambacho kingetokea baada ya yeye kuaga dunia na ndio maana aliwausia Waislamu kufuata na kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na suala zima la uimamu na ukhaifa baada yake.

Kati ya mambo aliyoyaandika an-Nu'mani katika kitabu chake cha al-Ghaiba na kunukuliwa na Allama al-Majlisi katika kitabu cha Bihar al-Anwar ni kuwa Imam Ali Amir al-Mu'mineen (as) alisema katika kusimulia yale yaliyotokea baada ya Mtume (saw) kuzuiwa kuandika yale aliyotaka kuyaandika na ambayo aliyataja kuwa dhamana ya kutopotea umma wake baada ya yeye kuondoka duniani: "Na masahaba wa Mtume (saw) walipoondoka, Mtume aliniambia kile alichotaka kuandika na kuwajulisha watu wote. Alisema kwamba Malaika Jibril alimfahamisha kwamba Mwenyezi Mungu alitambua vizuri kuwa umma ungetofautiana na kutawanyika baada ya Mtume kuaga dunia. Kisha Mtume aliitisha kitabu na kuniandikia humo aliyotaka kuyaandika na kuwaita watu watatu kuwa mashahidi nao ni Salman al-Farisi, Abudhar na Miqdad. Kisha aliwataja Maimamu wote wa wongofu na ambao aliwaamuru Waislamu kuwafuata na kuwatii hadi Siku ya Kiama. Alinitaja mimi kuwa wa kwanza wao kisha mwangu huyu Hassan na kisha mwanangu Hussein na kisha wengine tisa watakaotokana na mwanangu huyu Hussein."

Nam ndugu wasikilizaji, Mtume Mtukufu alionyesha rehema na upendo mkubwa kwa umma wake kiasi cha kuonyesha na kuwachagulia, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Maimamu wema ambao wangewashika mkono na kuwaongoza kwenye njia nyoofu ya matendo yanayomridhisha Muumba wao na ambayo inawaelekeza kwenye neema zake za milele. Aliwachagulia Ahlu Bait wake (as) kuwa viongozi wao kwa sababu wao ndio chimbuko la saada na kufuzu kwao katika maisha ya milele huko Akhera. Wao ndio njia ya haki, ukweli na heri kwa waja wa Mwenyezi Mungu. Katika hutuba yake aliyotoa siku ya Ijumaa ya tarehe 25 Swafar, yaani siku tatu kabla ya kuaga kwake dunia, Mtume Mtukufu (saw) aliwahutubia Waislamu kwa kuwaambia: "Enyi watu! Nitaondoka hivi karibuni na kuelekea machweo. Ninakuusieni muwatendee wema Ahlu Bayt wangu. Msiwapinge, msigombane nao, wala msiwapuuze na kuwatenga... Enyi watu! Anayelikosa jua basi na ashikamane na mwezi, na atakayeukosa mwezi basi na ashikamane na Farqad mbili (Hassan na Hussein), na mkikosa hizo mbili shikamaneni na nyota zinazong'aa…."

Alipoteremka kutoka kwenye mimbar yake (saw) Salman al-Farisi alimfuata na kumuuliza maana ya maneno aliyoyatamka naye akamjibu kwa kusema: "Mimi ndio Jua na Ali ni mwezi. Mkinikosa mimi basi shikamaneni naye (Ali). Ama Farqad mbili ni Hassan na Hussein. Hivyo iwapo mtaukosa mwezi shikamaneni na Farqad mbili hizo. Ama nyota zinazong'ara ni Maimamu tisa wanaotokana na kizazi cha Hussein ambapo wa tisa wao ni Qaim wao (Imam Mahdi -af-)…Wa kwanza na bwana wao ni Ali bin Abi Talib, wa baada yake ni wanawe wawili na baada yao ni Ali bin al-Hussein Zain an-Abideen, baada yake ni Muhammad al-Baqir al-Elm, baada yake ni Jaffar as-Swadiq, kisha Musa al-Kadhim ambaye alipewa jina la Nabii Musa bin Imraan na ambaye atauawa kwa kupewa sumu katika ardhi geni kutokana na dini na imani yake, kisha baada yake ni mwanawe Ali bin Musa ar-Ridha, kisha mwanaye Muhammad bin al-Jawad na kisha as-Swadiqan (wakweli wawili) Ali na Hassan na kisha wa mwisho ni Hujjat al-Qaim Anayesubiriwa. Wao ni itra, nyama, damu, ubongo, mifupa na mishipa yangu na ambao elimu yao ni elimu yangu na hukumu yao ni hukumu yangu. Hivyo yeyote atakayeniudhi kuhusiana nao basi hatapata shufaa yangu mbele ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiama."

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa siku ya leo, kipindi ambacho kimekujieni moja kwa moja kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana nanyi tena katika kipindi kingine juma lijalo Inshaallah, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaama Alaykum Warajmatullahi Wabarakatuh.