Aug 04, 2022 06:52 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tuna furaha kujiunga nanyi tena katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho tunatumai kitatunufaisha sote baada ya kusikiliza kwa makini yale tuliyokuandalieni kwa juma hili, karibuni.

Ni wazi kuwa Maimamu wawili Hassan na Hussein (as) walitunukiwa na Mwenyezi Mungu baraka na utukufu mkubwa kwa kujaaliwa kuwa na wazazi watukufu ambao ni Fatwimah (as) binti ya Mtume Mtukufu (saw) na Ali bin Abi Talib (as) ambao kama tunavyojua sote ana sifa na fadhila nyingi zisizohesabika katika Uislamu. Babu ya Maimamu wawili hao si mwingine bali ni Mtume Mtukufu mwenyewe Muhammad al-Mustafa (saw) ambaye ni mmbora wa viumbe wote. Licha ya utukufu wa Maimamu hao lakini jambo la kusikitisha ni kwamba maadui wa Uislamu hawakuwapa fursa ya kuishi kwa amani na furaha bali waliwatesa, kuwatenga kuwaudhi na kuwasababishia kila aina ya mahangaiko na mashaka na hii ni katika hali ambayo Mtume mwenyewe na kwa amri ya Mwenyezi Mungu alikuwa amewasihi na kuwataka Waislamu wawaheshimu, wawalinde na kutowasababishia matatizo na madhara ya aina yoyote ile kwa sababu hilo ni jambo linalomchukiza Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw).

*********

Wapenzi wasikilizaji Mtume hakuaga dunia ila baada ya kuwaarifishia Waislamu Ahlu Bayt wake watukufu kwa njia iliyo wazi kabisa na kuwataka Waislamu wote wafuate mafundisho yao na kutahadharisha dhidi ya kuwaasi na kuwatendea mabaya watukufu hao, kama tunavyosoma katika Hadithi na Riwaya nyingi za Kiislamu.

Imepokelewa katika kitabu at-Tarf cha Sayyid Ibn Tawous, Kanz al-Fawa’id cha al-Karajki, na Bihar al-Anwar cha Sheikh al-Majlisi kwamba katika ule usiku ambao Mtume aliaga dunia asubuhi yake, aliwaita Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein(as), na akamuomba Fatwimah amkaribie na hapo akaanza kumnong'onezea mambo fulani. Wake wa Mtume (saw) walipomwona Ali na wanawe wawili, wanatoka nje walimuuliza nini Mtume alikuwa akimnong'oneza binti yake, naye akajibu kwamba alikuwa anamwambia yale yangetokea baada yake.

Kisha ugonjwa wa Mtume (saw) alimzidia hapo Zahrah (as) akawa anamwita Ali ambaye aliingia chumbani huku akiwa ameandamana na wanawe wawili Hassan na Hussein. Hapo Mtume na Ahlu Bayt wake hao wakawa wanalia. Kichwa cha Mtume kilikuwa kifuani kwa binti yake Fatwimah (as) nao wajukuu wake Hassan na Hussein wakiwa wanambusu miguu yake huku wakiwa wanalia kwa sauti kubwa.

Mtume (saw) aliwatuliza na kuwausia kwa maneno ya kuwapa moyo na kuwatabiria heri kwa kuwaambia kwamba Siku ya Kiama Mwenyezi Mungu Mtukufu atautaka Moto wa Jahannam utulie na kupoa hadi Fatwimah na wanawe wawili Hassan na Hussein (as) wapite na kuingia Peponi. Hapo Fatwimah (as) ataingia Peponi huku Hassan akiwa upande wake wa kulia naye Hussein upande wake wa kushoto.

Na tunasoma katika kitabu cha Kashf al-Ghumma cha al-Arb'Ali, ndugu wasikilizaji kwamba, ilipotimia siku ya Jumanne tarehe 28 katika mwezi wa Swafar, Mtume hakuenda mbali wala kuachana na Ahlu Bait wake (as) ambapo aliweka kichwa chake kwenye mapaja ya Imam Ali (as). Mtume alimwomba Imam Ali (as) amsaidie kuketi na alipomketisha Mtume (saw) alimwomba Bilal amwitie wajukuu zake wawili Hassan na Hussein. Alitoka nje kuwaita na muda sio mrefu akawa amewaleta kwa Mtume (saw). Mtume aliwakumbatia kifuani kwake huku akiwa anawabusu. Alipoona hivyo Imam Ali alienda kuwatoa kifuani kwa Mtume ili wasimuumize katika hali yake ya ugonjwa na hapo Mtume (saw) akawa amemwambia Ali (as): "Achana nao wanibusu nami nipate kuwabusu, wanufaike nami nami pia nipate kunufaika nao. Hii ni kwa sababu watakabiliwa na misukosuko na dhulma kubwa baada yangu na watapitia mambo magumu na matatizo mengi. Mwenyezi Mungu awalaani wale wote watakaowadhulumu wanangu wawili hawa."

*********

Wapenzi wasikilizaji tunaendelea kusimulia hali aliyokuwa nayo Mtume Mtukufu (saw) wakati alipokuwa amezidiwa na ugonjwa huku akiwa anawaaga Ahlu Bayt wake watukufu ambapo aliwausia sana Waislamu wawalinde Ahlu Bayt hao na kutowaudhi au kuwadhuru kwa njia yoyote ile.

Ibn Nema al-Hilli ameandika katika kitabu chake chenye jina Muthirul al-Ahzan kwamba Mtume Mtukufu (saw) alimkumbatia Hussein kifuani kwake huku akiwa anatokwa na jasho ambalo lilimdondokea mwanaye huyo na kusema (saw): "Vipi huyu Yazid, Mwenyezi Mungu asimjaalie heri, Allahumma mlaani Yazid"! Kisha Mtume akawa amezidiwa na kupoteza fahamu kwa muda na alipopata fahamu alianza kumbusu Hussein huku akiwa anatokwa na machozi. Alimwambia Hussein: Bila shaka mimi na muuaji wako tutasimama mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu (nitamuwajibisha)."

Alipokuwa amelala kwenye kitanda cha mauti huku akiwa amezungukwa na Ahlu Bayt wake waliokuwa na huzuni kubwa, Mtume (saw) aliwabashiria Pepo na heri Ahlu Bayt hao pamoja na wafuasi na waungaji mkono wao ambao waliwafuata kwa wema na kuwataii katika yale yote waliyoamrisha na kuyakataza na wakata huo huo kuwaonya na kuwatahadharisha na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiama wale waliowatendea mabaya, kuwapinga na kuwadhulumu humu duniani.

Muda mfupi kabla ya kuingia adhuhuri, Bibi Fatwima alifika mbele ya Mtume akiwa ameandamana na watoto wake wawili Hassan na Hussein na kusema (as): "Hawa ni watoto wako wawili basi warithishe. Mtume (saw) akasema: Ama Hassan ana hadhi na heshima yangu, na kuhusu Hussein ana ujasiri na ukarimu wangu."

Naye Ibn Shahrashub anaansika katika kitabu cha Manaqib Aali Abi Talib kwamba ilipofika adhuhuru siku ya Jumanne na kifo cha Mtume kukaribia, Malaika wa Mauti alimwomba idhini Mtume naye akawa amekusanya Ahlu Bayt wake, Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein (as) na kuwaomba watu wengine waondoke chumbani hapo na kumtaka Ummu Salama asimame mlangoni ili asiingie humo mtu. Kisha aliunyanyua mkono wa binti yake Fatwimah na kuuweka katika kifua chake kitukufu na akaushika mkono wa Ali kwa mkono wake mwingine. Alipotaka kuzungumza Mtume (saw), alishindwa kufanya hivyo kutokana na maumivu ya ugonjwa aliokuwanao, jambo lililomfanya Fatwimah alie kwa uchungu na kumbusu baba yake usoni. Ali, Hassan na Hussein nao pia walilia sana baada ya kumwona Mtume akilia. Kisha wakaanguka na kuukumbatia uso wake. Baada ya hapo Mtume alimuusia Ali jambo fulani kuhusiana na Fatwimah na akataja baadhi ya fadhila zake. Kisha alizungumzia yale ambayo yangewapata baada ya yeye kuaga dunia. Aliwakumbatia wote Fatwima, Ali, Hassan na Hussein huku akibusu, kunusa na kuwanyonya Hassan na Hussein. Aliwapasha habari kwamba wangedhulumiwa na kuuawa kinyama baada yake. Alilaani wauaji wao na kumuusia Imam Ali awachunge. Muda si mrefu Mtume alikata roho na hivyo kuhitimisha maisha yake matukufu humu duniani akiwa mikononi mwa Imam Ali (as). Hapo Imam Ali akasema: "Sote ni wa Mungu na kwake tutarejea. Ni msiba ulioje uliowapata Ahlul Bayt mahsusi na Waumini kwa ujumla!

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.