Aug 04, 2022 07:05 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutokan mjini Tehran. Tuna furaha kujiunga nanyi tena katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kama mnavyojua huzungumzia sifa na fadhila za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) ambao si wengine bali ni Imam Hassan na Hussein (as).

Uislamu ni dini kamilifu na inayokamilisha dini na masuala mengine. Imekamilisha maadili bora, sheria na hukumu, imesahihisha imani na itikadi, imetabiri yatakayotokea baadaye, ili watu – ndugu wapenzi – wapate kujua vyema mambo yanayowahusu maishani, na ili mtihani wa Mwenyezi Mungu uwe ni wa kiadilifu kutokana na kuwa tayari ametupa hoja za kutosha na hivyo kutenganisha ukweli na batili.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) – ndugu zetu watukufu – na kwa msingi wa mafundisho ya Qur’ani Tukufu, alikuwa na habari za kutosha kuhusu umma wake, na hivyo akatangaza Uimamu baada yake na hata kuyataja majina ya maimamu hao kabla ya kuzaliwa kwao. Aliwausia watu washikamane na mafundisho ya Maimamu hao wa kizazi chake kama ambavyo aliwatahadharisha dhidi ya kuwaudhi seuze kupiga vita, kufanyiwa uadui na kuuliwa! Mtume Mtukufu aliyafanya hayo yote ili ukweli upate kubainika wazi na kujitenga na batili na ili watu wasije kusema baadaye: Laiti tungeletewa Mtume mwonyaji, na elimu inayoongoza, ili tuzifuate Ishara zake kabla hatujadhalilika na kufedheheka!

Sheikh as-Swadouq ananukuu katika kitabu chake cha Illal Al-Sharai' kwamba Mtume Mtukufu (saw) alimwambia Amirul-Muuminina Ali (as): “Andika ninayokwambia……Waandikie washirika wako.” Nikauliza: Ni nani hao washirika wangu, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Ni Maimamu wanaotokana na kizazi chako, ambao kwa baraka zao umma wangu utakatiwa kiu kwa kujaaliwa mvua, dua zao kujibiwa, Mwenyezi Mungu atauondolea balaa na kuuteremshia rehema kutoka mbinguni. Kisha alimuashiria Imam Hassan (as) kwa mkono wake na kusema: Huyu ndiye wa kwanza wao - na kisha akamuashiria Hussein (as) na kusema: “Maimamu (waliosalia) watatokana na kizazi chake."

Al-Swadouq pia ananukuu riwaya nyingine katika kitabu chake cha Ikmaal al-Deen wa Itmaam an-Ni'ma kutoka kwa Imam Swadiq (as), akisema: "Wakati Fatwimah (as), alipopata ujauzito wa Imam Hussein (as), Mtume Mtukufu (saw) alimwambia: Mwenyezi Mungu Mtukufu amekupa mtoto wa kiume anayeitwa Hussein, na ambaye Umma wangu utamuua. Fatwimah akasema: Sina haja naye: Mtume (saw) akasema: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ameniahidi jambo. Fatwima akamuuliza: Ni nini hicho alichokuahidi? Akasema Mtume (saw): Ameniahidi kwamba ataujaalia Uimamu baada yake katika kizazi chake. Akasema Fatwimah (as): Basi nimeridhia."

***********

 

Ndugu wasikilizaji, hivi ndivyo Mtume Mtukufu (saw) alivyohubiri kuufahamisha umma wake kuhusu suala zima la Uimamu na Maimamu, na kuwatabiria jinsi suala hilo lingechukuliwa katika jamii.

Nam, jambo la kusikitisha ni kwamba mara tu baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw), ukhalifa na Uimamu ulipokonywa kizazi chake, watu wakarejea nyumba na kupuuza mafundisho ya dini na amri za Mtume, kizazi chake kikavunjiwa heshima, kikateswa, kikauawa, kikapokonywa urithi kilioachiwa na Mtume (saw) na kubaidishwa. Kuna hadithi na riwaya nyingi ambazo zinathibitisha kwamba Mtume Mtukufu aliyabashiri hayo yote kabla ya kuaga kwake. Miongoni mwa Hadithi hizo ni kauli yake akimwambia mwanawe Al-Hussein (as): "Kipenzi changu Jibril alinijia na kuniambia kuwa nyinyi mtauawa, na makaburi yenu kutawanyika sehemu mbalimbali!"

Imepokelewa kutoka kwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), akisema: “Babu yangu mpendwa, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), aliniambia kuwa jambo hilo (Uimamu) litamilikiwa na watu kumi na wawili kutoka katika familia yake teule. Sote tutauawa ima (kwa kupigwa upanga) au kupewa sumu."

Hayo ndiyo waliyoambiwa Waislamu na Mtume (saw), ambapo alitabiri kuuawa mawasii wake mmoja baada ya mwingine.

Allama al-Majlisi ananukuu katika kitabu chake cha Bihar al-Anwaar Hadithi inayohusiana na kuuawa shahidi Imam Ali (as) kwa kusema: Mwenyezi Mungu atampokea shihidi akiwa ameuawa kwa upanga….. atazikwa katika eneo linalojulikana kama al-Ghariyy.. Kisha atakayechukua Uimamu baada yake ni mwanawe al-Hassan…. Atauawa kwa kupewa sumu na kuzikwa katika eneo zuri linalojulikana kama Baqee. Kisha baada yake atakuja al-Hussein, Imam mwadilifu…. Utauawa kwa upanga katika ufuo wa Mto Furati katika siku safi (tukufu)... Atazikwa Karbala, kaburi lake litakuwa nuru na mwangaza kwa watu..", hadi mwisho wa Hadithi.

Wasomi waliokuja kabla ya Uislamu pia walithibitisha jambo hilo ambapo as-Swadouq anasema katika kitabu chake cha Aamali akimnukuu Abdullah bin Sulaiman akisema: "Nilisoma katika Injili ikibainisha sifa za Mtume (saw) kwamba ana watoto wachache, lakini kizazi chake kitatokana na mwanamke aliyebarikiwa ambaye ana nyumba Peponi.. Ana vifaranga wawili (Hassan na Hussein) waliouawa shahidi."

Nam ndugu wapendwa, bishara za kinabii ziliendelea kutaja na kutabiri yale yote ambayo yangewapata Ahlu Bayt wake wote, yaani kwamba wangeuawa shahidi kwa namna tofauti. Baadhi ya Hadithi hata zimebainisha suala hilo ni kana kwamba matukio ya kuuawa shahidi watukufu hao tayari yalikuwa yamekwishatokea huko nyuma. Mfano wa hilo ni kama Qur'ani Tukufu inavyobainisha Siku ya Kiyama ni kana kwamba tayari imekwishatokea, yaani inazungumzia suala hilo kwa swigha na kitendo cha wakati uliopita.  Inasema katika Aya ya 1 ya Surat an-Nahl:  Imefika amri ya Mwenyezi Mungu, msiifanyie haraka. Wafasiri wa Qur'ani Tukufu wanasema: Maana yake ni, imekuja amri ya Mwenyezi Mungu iliyoahidiwa, nayo ni Siku ya Kiyama. Imeelezea jambo hilo kwa kitendo cha wakati uliopita kutokana na kutimia kwake katika ujuzi na elimu ya Mungu Mwenyezi.

Kadhalika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) alikuwa tayari anayajua yale ambayo yangetokea na kuisibu Ahlu Bayt yake, hivyo akasema (saw): "Hakika katika wanangu hao kuna yule aliyenijia hali ya kuwa ameuawa kwa sumu, na mwingine ameuwa kwa upanga!''

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni moja kwa moja kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka Tehran. Ni matumaini yetu kuwa tumenufaika sote kwa pamoja na yale tuliyoyasikia katika kipindi hiki. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena katika kipindi kijacho cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.