Aug 04, 2022 07:23 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Hiki ni kipindi cha 50 na cha mwisho katika mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambavyo vimekuwa vikijaili na kuzungumzia sifa na fadhila za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu ambao ni Imam Hassan na Imam Hussein (as) wajukuu ambao walipendwa sana na Mtume (saw) ambaye pia aliwataka Waislamu wote wawapende, wawaheshimu na kuwakinga na madh

Lakini pamoja na hayo Waislamu walipuuza wito huo wa Mtume kuhusiana na wajukuu wake hao na wakawa wamewatelekeza na mwishowe wakapelekea kuuawa kwao mikononi mwa maadui waliotawaliwa na uchu wa madaraka na ambao walitumia vibaya Uislamu kwa ajili ya kufikia malengo yao binafsi ya humu duiani.

Ili kusikiliza tuliyokuandalieni katika kipindi hiki cha mwisho katika mfululizo huu wa vipindi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi tunakukaribisheni muwe pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

*********

Waislamu wa kawaida na maswahaba waaminifu waliokuwa karibu na Mtume (saw), walikuwa hawajawahi kusikia maneno makali kutoka kwa mtukufu huyo ya kumlaani muuaji wa Maimamu wa uongofu kama walivyoyasikia kutoka kwake (saw) akimlaani muuaji wa Abu Abdillah al-Hussein (as). Hivyo wasomi na wafuasi waaminifu wa Mtume wakakisia kwamba bila shaka muuaji wa Imam Hussein (as) hangetosheka kwa kumuua mjukuu huyo wa Mtume (saw) bali angefanya kitendo cha kinyama ambacho kingewashangaza wengi na kuwaacha vinywa wazi. Walikisia kwamba kwa mauaji hayo muuaji huyo asiye na huruma angefanya ukatili wa kushtua kwa kumvunjia heshima mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) na hivyo kumvunjia heshima Mtume, Maimamu na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ujumla. Kitendo hicho bila shaka kingekuwa ni cha kinyama, cha kupindukia na ambacho kingekuwa hakijawahi kushuhudiwa tena katika historia ya mwanadamu.

Nam, ndugu wasikilizaji, ukatili huo ulikuwa mkubwa na wa kupindukia kiasi kwamba hata Imam Hussein alipomtembelea kaka yake Hassan (as) alipokaribia kukata roho kutokana na sumu aliyopewa na maaadui wa Uislamu, Imam Hassan al-Mujtaba (as) alimuomboleza ndugu yake Hussein (as) kwa kusema: "Kile kitakachoniua ni sumu watakayoninywesha, lakini hakuna siku (ya msiba mkubwa) itakayokuwa kama siku (ya msiba) yako ewe Aba Abdillah! Siku hiyo utazingirwa na watu elfu thelathini ambao watadai kuwa ni katika Umma wa babu yetu Muhammad (saw) na kuwa ni Waislamu. Wote watakusanyika kwa ajili ya kukuua na kumwaga damu yako, kukuvunjia heshima, kuwachukua mateka familia na wanawake wako pamoja na kupora mahema yako. Katika hali hiyo Mwenyezi Mungu atawalaani Bani Ummayyia na mbingu kunyesha damu na jivu. Kila kitu kitakulilia ikiwa ni pamoja na wanyama wa pori na samaki wa baharini."

Haya yameandikwa na Ibn Hasnawayh al-Mawsili al-Hanafi katika kitabu chake cha Durr Bahr al-Manaqib, katika hali ambayo al Khawarazmi al-Hanafi anasema katika kitabu cha Maqtal al-Hussein (as) kwamba: "La ajabu ni wale watu ambao Mwenyezi Mungu amewalaani, walimuua mmoja wao kwa sumu, na mwingine kwa upanga, nao ni watu wawili hao (Imam Hassan na Hussein)!

Al-Hafidh as-Suyuti as-Shafi' anasema katika maelezo chini ya anwani al-Alai al-Masnua kwa kumnukuu Talha, na vile vile al-Badakhshi katika kitabu cha Miftah Al-Najah, al-Khawarazmi katika al-Maqtal na Sheikh al-Swadouq katika Akhbar ar-Ridha (as) kwamba: "Musa bin Imran alimwomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika ndugu yangu Haroun amekufa, hivyo msamehe makosa yake. Mwenyezi Mungu akamwambia: Ewe Musa! Hata kama ungeniomba niwasamehe makosa yao wale wote waliotangulia na watakaokuja, ningefanya hivyo isipokuwa tu yule aliyemuua Hussein bin Abi Talib. Bila shaka nitamlipizia kisasi chake kwake!"

*********

Nam, ndugu wasikiliza, Mtume Mtukufu (saw) alitupasha habari ya msiba mkubwa na machungu ambayo yangempata kipenzi, mjukuu, ua na nuru ya moyo wake al-Imam al-Hussein (as) na hivyo kughubikwa na huzuni na majonzi makubwa. Huzuni na machungu hayo yamebainishwa kwa mapana na marefu katika hadithi nyingi zilizobainishwa na Mtume Mtukufu (saw) katika sehemu na matukio mbalimbali aliyopitia maishani. Baadhi ya Hadithi hizo ni ile iliyonukuliwa na as-Suyuti katika kitabu chake cha Taarikh al-Khulafaa akimnukuu Abi Dardaa ambaye anasema: "Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: Mtu wa kwanza atakayebadilisha suna yangu ni kutoka uko wa Bani Ummayyia anayeitwa Yazid."

Naye Muttaqi al-Hindi anasema kwenye kitabu cha Kanz al-Ummal kwamba Mtume (saw) alisema: "Mwenyezi Mungu asimbariki Yazid (akate kizazi chake) ambaye ni mwingi wa kuvunja heshima na anayelaani! Ambaye ataniulia mpendwa na kipenzi changu Hussein (as) na ambaye (Hussein) nimeletewa udongo wa sehemu atakayouawa shahidi na nikamwona muuaji wake!" Akasema Hadithi hii pia imenukuliwa na Ibn Asakir katika kitabu cha Tarikh ad-Dimashk.

Naye al-Haithami as-Shafi' amenukuu katika kitabu cha Majmau az-Zawaid Hadithi kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: Yazid! Mwenyezi Mungu asimbariki Yazid (amkatie kizazi)! Akatokwa na machozi na kisha akasema: Aliniulia Hussein na nikaletewa udongo (mchanga) wake, na kisha nikafahamishwa muuaji wake! Kisha akasema Mtume (saw): Mungu wangu! Nawasikitikia wanyonge na watoto wa Watu wa Nyumba ya Muhammad (saw) kutokana na shari watakayopitia mikononi mwa khalifa atakayetwa ukhalifa. Atakuwa dhalimu, mchafu, mwovu na mwenye kupenda anasa. Atamuua mrithi wangu na mrithi wa mrithi wangu baada yangu."

Na katika kitabu cha al-Futuh, Ibn A'tham al-Kufi anamnukuu Ibn Abbas akisema: "Siku moja Mtume (saw) alitoka kwenda safarini na alipokuwa njiani alisimama ghafla na kusema: Hakika sote tunatoka kwa Mwenyezi Mungu na hakika kwake tutarejea! Alitokwa na machozi na kuulizwa sababu ya hilo naye akasema: Huyu hapa Malaika Jibril ananipasha habari kuhusiana na yatakayojiri katika ukingo wa Mto Furati sehemu inayoitwa Karbala, ambapo atauawa hapo mwanangu al-Hussein mtoto wa Fatwimah." Mtu mmoja akauliza: Je, ni nani huyo atakayemuua, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!? Akasema: Ni mtu anayeitwa Yazid. Mwenyezi Mungu asimbariki maishani. Ninaona sehemu atakayouawa na kuzikwa. Watakata kichwa chake na kumpelekea Yazid kama zawadi! Ninaapa kwa jina la Mwenyzi Mungu! Kila mtu atakayekitazama kichwa cha mwanangu kilichokatwa na kisha kufurahia jambo hilo, bila shaka atakuwa amempinga Mwenyezi Mungu."

Na katika riwaya iliyonukuliwa na Ibn Quluwayh katika kitabu cha Kamil al-Ziyarat Imam Jaffar al-Swadiq (as) ananukuliwa akisema kwamba siku moja Imam Hussein (as) alikuwa amebebwa na mama yake ambapo Mtume (saw) alimchukua na kisha kumwambia: "Mwenyezi Mungu awalaani watakaokuua, Mwenyezi Mungu awalaani watakaokujeruhi, Mwenyezi Mungu awalaani watakaokusaliti na Mwenyezi Mungu awauwe wale wote waliosaidiana dhidi yako."

Nam ndugu wasikilizaji, ni huzuni kubwa iliyoje aliyokuwa nayo Mtume Mtukufu (saw) hadi akawa anazungumza kwa uchungu kuhusiana na mauaji na msiba mkubwa ambao ungempata mjukuu wake Imam Hussein (as) na kuamua kuwalaani waovu ambao wangemsaliti na kumuua kinyama katika ardhi ya Karbala huko Iraq?!

Khatib al-Baghdadi ameandika katika kitabu cha Tarikh Baghdad akimnukuu Jabir bin Abdullah al-Ansari kwamba alisema: "Nilimwona Mtume (saw) akiwa anacheza na Hussein huku akisema: 'Mwenyezi Mungu amlaani atakayekuua!' Jabir akasema: Nikamuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, ni nani atakayemuua?! Akasema: Ni mtu anayetoka kwenye Umma wangu ambaye anawachukia Aali zangu. Shufaa yangu isimfikie! Ni kana kwamba ninamwona akiungua kwenye matabaka ya moto huku akirukaruka juu chini hali ya kuwa sauti ya moto mkali inasikika ndani ya mwili wake.' Riwaya hii pia imenukuliwa na Ibn Hajar al-Askalani as-Shafi' katika Lisan al-Mizaan na Ibn Asakir katika Tarikh ad-Dimashk.

Naye al-Khawarazmi anasema katika kitabu cha Maqtal al-Hussein (as) akimnukuu Imam Ali (as) kwamba alisema: "Mtume Mtukufu (saw) alisema: Binti yangu Fatwimah atafufuliwa Siku ya Kiama huku akiwa amebeba nguo iliyojaa damu. Kisha ataegemea moja ya nguzo za Arshi (Kiti cha Enzi) ya Mwenyezi Mungu na kusema: Ewe Uadilifu (Mwadilifu/Mwenye Hekima)! Hukumu baina yangu na muuaji wa mwanangu. Mtume (saw) akasema: Ninaapa kwa jina la Mwenye Kaaba kwamba, Mwenyezi Mungu atahukumu kwa mslahi ya binti yangu."

Riwaya hii pia imenukuliwa na Ibn al-Maghazili as-Shafi' katika kitabu cha Manaqib Ali, ad-Dailami katika Firdous al-Akhbar, al-Badakhshi katika Miftah ad-Dujah fi Manaqib Aal al-Aba na al-Qandouzi al-Hanafi katika Yanabiul Mawaddah.  

************

Na Mtume (saw) hakutosheka na hayo tu bali aliendelea kuukemea umma ambao ungemwacha pekee yake mpendwa wake al-Imam al-Hussein mbele ya maadui wa Uislamu ili wamkatekate kwa mapanga na kumdunga kwa mikuki na mishale! Aliwaambia na kuwatahadharisha kuhusu yale yote ambayo yangempata mjukuu wake huyo mpendwa!

Tabarani anaandika katika kitabu cha Mu'jam na al-Muttaqi al-Hindi katika Kanz al-Ummal kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: "Ninaapa kwa jina la yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake! Atauawa (Imam Hussein) mikononi mwa kaumu ambayo haitamsaidia (kumtetea). Na katika riwaya nyingine: Kaumu ambayo haitamnusuru. Mwenyezi Mungu aweke hitilafu kati ya nyoyo na ndimi zao. Na katika Riwaya nyingine: Mwenyezi Mungu atawaadhibu wote."

Na Riwaya ya Ibn Abbas ambayo Ibn A'tham ameinukuu katika kitabu cha al-Futuh inaseme kwamba Mtume (saw) alisema: "Hakika Malaika Jibril amenipasha habari kwamba Umma wangu utamuua mwanangu Hussein katika ardhi ya Karbala… Mwenyezi Mungu amlaani na kumdhalilisha muuaji wake hadi mwisho wa Dunia!" Mtume (saw) pia amenukuliwa akisema: "Hakika aliyemuua Hussein yuko kwenye jeneza la moto, anapata nusu nzima ya adhabu ya watu wa motoni! Mikono na miguu yake imefungwa kwa nyororo za moto. Atatupwa motoni hadi atumbukie kwenye sakafu ya Jahannam. Atakuwa anatokwa na uvundo mkali ambao utawakera watu wa motoni kiasi cha kumwomba Muumba wao awaondolee uvundo huo. Na humo motoni atakaa milele huku akipata adhabu kali!"

Katika upande wa pili, Bwana wa Mashahidi na Vijana wa Peponi (Imam Hussein as) ana cheo na nafasi ya juu  na tukufu ambayo huwafanya wafuasi wake wajivunie na kuhisi kuwa wamebarikiwa kuwa karibu na mtukufu huyo. Ummu al-Mu'mineen Ummu Salama, amenukuliwa akisema kwamba Mtume Mtukufu (saw) alimpasha habari binti yake Fatwimah (as) kuhusu kuuawa kwa mwanae Imam Hussein (as) na kisha kumfariji na kumpa bishara kwa kusema: "Atauawa katika ardhi inayoitwa Karbala ambayo ni ngeni na iliyo mbali na watu wake. Kuna kundi litakalomzuru ewe Fatwimah! Huku likiwa na nia ya kunitendea wema na kuwa na mfungamano nami. Mimi pia siku ya Kiama nitawaendea na kushika mikono yao na kisha kuwaokoa kutokana na mfadhaiko na mashaka makubwa ya siku hiyo."

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio tunafikia mwisho wa mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambavyo tunatumai vimetunufaisha sote kwa pamoja. Basi hadi wakati mwingine, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.