Jun 07, 2016 08:33 UTC

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachozungumzia maadi na safari ya mja kurejea kwa Mola Muumba. Katika baadhi ya vipindi vilivyopita tulisema kuwa, itikadi ya kuwepo ulimwengu wa milele ni itikadi ya kifitra na kimaumbile.

Pamoja na hayo tulisema, baadhi ya watu wanauliza swali kwamba, kama kweli mwanadamu ana maisha ya milele katika ulimwengu mwingine na kwamba roho yake haitoweki na kutokomea baada ya kutengana na mwili, kwa nini basi wanadamu wengi wanaogopa kifo? Katika kipindi cha wiki iliyopita tulijibu sehemu moja ya swali hili na leo tutakamilisha jibu lake. Tafadhalini endeleeni kuwa nasi hadi mwisho wa makala yetu ya leo.     

<<<<   >>>>

Katika kipindi cha wiki iliyopita tulisema kuwa watu wengi wanaogopa kifo na hukiona kama zimwi la kutisha linalowaandama muda wote. Tulisema kuwa kuna sababu kadhaa zinazowafanya wanadamu waogope kifo na mauti na lakini tulitoa sababu mbili kuu miongoni mwao. Sababu ya kwanza ni ujahili na kutojua kifo ni nini. Kifo kama tulivyoashiria katika vipindi vilivyopita, ni kuzaliwa upya mwanadamu lakini katika ulimwengu mwingine sawa kabisa na jua linalozama katika sehemu moja ya dunia na kuchomoza katika dunia na ulimwengu mwingine. Mauti kwa muumini ni sawa na hamamu na bafu ambayo humsafisha na machafu yote. Machafu yaliyosababishwa na madhambi ya duniani na ambayo bado hayajafutwa, hufutika na kuondolewa na kifo.

Kuna baadhi ya watu wanaoogopa kifo japokuwa wanaamini kwamba kufariki dunia si mwisho wa maisha ya mwanadamu. Watu hawa ni wale wanaoiashiki na kuipenda sana dunia na vilivyomo. Watu wa aina hii kama tulivyosema ni mithili ya gundi inayonata katika sehemu yenye manyoya au nywele nyingi ya mwili wa mwandamu, huwa vigumu sana kuiondoa mahala hapo, na kuiondoa kwake husababisha maumivu makubwa. Vivyo hivyo mwanadamu anayeiashiki, kuipenda na kuikumbatia sana dunia, kama gundi inavyonata kwenye kiungo chenye manyoya; huwa vigumu sana kwake kutengana na dunia.  

Wakati mwingine mwanadamu huogopa kifo na mauti hutokana na madhambi na dhulma alizozifanya hapa duniani. Hii ina maana kwamba, si watu wote wanaoamini kuwa mauti ni dirisha na njia ya kuelekea kwenye ulimwengu mwingine wa Akhera huwa na utulivu na huyapokea mauti kwa mikono miwili. La hasha, bali wapo watu ambao licha ya kuamini ufufuo na maisha ya baada ya kifo, lakini huyaogopa sana mauti na kifo kutokana na madhambi na matendo yao maovu. Wanadamu hawa wanaelewa kwamba, baada ya kufariki dunia wataingia katika ulimwengu mwingine ambako watalazimika kujibu na kutoa maelezo kuhusu matendo, mwenendo, maneno na mali zao, na kwa kuwa walitenda madhambi hapa duniani, wanaogopa kifo na suala la kwenda kutoa maelezo na majibu ya maswali kuhusu amali na matendo yao katika ulimwengu mwingine wa baada ya dunia hii.

Imepokewa kwamba, bwana mmoja aliyekuwa miongoni mwa wapenzi wa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib (as) ambaye alikuwa mcheshi na mwenye kupenda utani, alimtembelea mtukufu huyo. Imam Hassan (as) alimuuliza hali yake na bwana yule alisema: Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ninapitisha siku zangu kinyume na aliyoyataka Mwenyezi Mungu na kinyume na anayotaka shetani, bali hata kinyume na ninayoyataka mimi mwenyewe. Imam Hassan al Mujtaba (as) alitabasamu na kuuliza: Vipi? Bwana yule alisema: Mwenyezi Mungu anataka nimtii daima na nisifanye madhambi kamwe, lakini mimi siko hivyo. Katika upande mwingine shetani anataka nimuasi Mwenyezi Mungu daima na nisimtii kabisa, na mimi siko hivyo. Mimi mwenyewe pia nataka nibakie hai daima na nisife, hili pia haliwezekani"!

Wakati huo huo mtu mwingine aliyekuwa kati ya hadhirina aliuliza: Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kwa nini sisi tunayachukia mauti na hatupendi kifo? Imam Hassan alisema: Kwa sababu mumeijenga na kuitengeneza dunia yenu na kuharibu Akhera yenu. Hivyo ni jambo la kawaida kwamba hampendi kuondoka sehemu mliyoijenga na kuistawisha na kuhamia kwenye magofu na uharibifu". (Biharul Anwar-Juzuu ya 6)

<<<<<    >>>>>

Iwapo tutayatambua mauti na kifo kuwa ni mwanzo wa maisha mapya, uhai wa milele na dirisha au lango la kuelekea kwenye ulimwengu mkubwa na mpana zaidi- kwa sharti la kutenda mema-, basi hapana shaka kuwa si tu kwamba mwanadamu hatayaogopa bali pia atayapokea kwa mikono miwili. Hii ni kwa sababu, mauti kwa maana hiyo ni sawa na kuvunja tundu finyu la dunia hii, kuwa huru roho ya mwanadamu na kukata minyororo na pingu zote za kimaada zilizokuwa zikiishikilia roho na nafsi yake. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana watu adhimu na wema waliyaona mauti na kifo kuwa ni lango na daraja la kuwahamisha kuelekea kwenye ulimwengu mwingine na waliyakaribisha kwa utulivu na moyo mkunjufu. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema katika hotuba ya 5 ya Nahjul Balagha kwamba: "Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kuwa hamu ya mwana wa Abi Twalib kwa mauti ni kubwa zaidi kuliko hamu ya mtoto mdogo anayenyonya kwa ziwa la mama yake…"

Mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) pia aliwaambia masahaba zake siku ya Ashura alipokuwa akipambana na jeshi la mtawala dhalimu Yazid bin Muawiya kwamba: Kuweni na subira enyi wana wa watu adhimu! Kifo ndio daraja pekee litakalowahamisheni kutoka kwenye mashaka na maumivu kuelekea kwenye mabustani makubwa ya Pepo na neema za kudumu milele. Nani kati yenu asiyependa kuhama kutoka kwenye jela na kuelekea kwenye kasri? Mauti kwa maadui zenu ni mithili ya mtu anayehama kutoka kwenye kasri kwenda jela na adhabu kali. Baba yangu amenukuu kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba amesema: Dunia ni jela ya muumini na Pepo ya kafiri, na mauti ni daraja la muumini kuelekea peponi na daraja la makafiri kuelekea kwenye moto wa Jahannam".

Kwa msingi huo muumini anayetarajia rehma zisizo na kikomo za Mwenyezi Mungu na anayetekeleza vyema wajibu wake na kujiepusha na makatazo ya Allah na kutubia madhambi yake si tu kwamba haogopi kifo na mauti, bali huyaashiki na kuyakaribisha yanapomjia. Hii ni kutokana na hamu yake kubwa ya kukutana na Mola Karima, Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu huko katika ulimwengu wa Akhera. Watu wanaotambua mauti na kifo kuwa ni njia ya kuelekea kwenye uhai wa milele na wanaoamini kuwa, rehma na maghufira ya Mwenyezi Mungu hayana mpaka wala mwisho, huwa na matumaini ya rehma na huruma Yake na wala hawaogopi kifo na mauti. Na pale wanapofanya madhambi na makosa huharakia kutubu wakitaradhia rehma za Mola Muumba. Watu hawa huosha madhambi yao kwa maji ya toba kwa sababu watu wanaotubu ni habibu na vipenzi vya Mola Karima. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 222 ya Suratul Baqara kwamba: Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojisafisha. 

Hivyo mtu anayependwa na Mwenyezi Mungu huwa haogopi kufariki dunia kwenda kukutana na kipenzi na mahabubu wake.

<<<<<<   >>>  

 

 

Tags