Oct 09, 2022 11:58 UTC
  • Ndege za Russia kukarabatiwa Iran

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Ndege za abiria za Russia zinakarabatiwa nchini Iran huku uhusiano wa nchi hizi mbili jirani ukizidi kuimarika ili kukabiliana na vikwazo vya vya Marekani.

Waziri wa uchukuzi wa Iran Rostam Qassemi amesema Russia imeziagiza kampuni za huduma za uhandisi wa usafiri wa anga za Iran kuzifanyia ukarabati ndege zake.

Qassemi amesema kwamba tayari ndege tisa za abiria za Russia ziko Iran kwa ajili ya kupata matengenezo huku akipigia debe teknolojia iliyopo katika sekta ya usafiri wa anga ya Iran ambayo imewezesha ukarabati na ukaguzi wa aina mbalimbali za ndege za abiria.

"Tumekuwa katika nafasi nzuri katika miezi ya hivi karibuni katika suala la ukarabati wa ndege," amesema waziri bila kufafanua aina za ndege za Russia zinazokarabatiwa nchini Iran.

Tangazo hilo linakuja huku kukiwa na ripoti za ushirikiano wa karibu kati ya Iran na Russia ili kupunguza athari za vikwazo vya madola ya Magharibi.

Iran na Russia zimetia saini mikataba mikubwa katika miezi ya hivi karibuni ili kuimarisha ushirikiano wao katika nyuga za sayansi na teknolojia, uchumi na nishati.

Marekani iliiwekea Iran vikwazo shadidi mnamo 2018 baada ya Washington kujiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya kimataifa juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Marekani na washirika wake waliiwekea Russia vikwazo vikali zaidi mwezi Februari baada ya Moscow kuanzisha operesheni ya kijeshi nchini Ukraine.

Wataalamu wanasema vikwazo vya Marekani vilishindwa kufikia lengo kuu la kuilazimisha Iran kulegeza misimamo yake imara katika masuala ya kisiasa na kijeshi. Wanasisitiza kuwa marufuku hiyo hata iliipa Iran fursa ya kubuni misingi ya uchumi wake mbali na mapato ya mafuta ghafi na kutegemea zaidi rasilimali zake za ndani.

NANOTEKNOLOJIA NCHINI IRAN

Taarifa ya hivi karibuni ya Makao Makuu Maalum kwa ajili ya Maendeleo ya Nanoteknolojia nchini Iran imesema Bidhaa za "nanoteknolojia" za Iran sasa zitauzwa katika nchi 47 ambazo zimetuma maombi ya kupokea bidhaa hizo.

Taasisi hiyo imeongeza kuwa: Bidhaa na huduma za nanoteknolojia katika nyanja mbalimbali za ujenzi, optoelectroniki, dawa, afya na tiba, vitambaa na nyanja nyingine za teknolojia zinasafirishwa katika nchi 47 zilizoomba.

Iran ni miongoni mwa nchi tajika katika uga wa teknolojia ya nano katika ngazi ya kimataifa, na wanateknolojia Wairani wameweza kurekodi mafanikio muhimu katika uwanja huo.

Sekta hii, kwa msaada na uwezo wa wataalamu wa ndani ya nchi, imeweza kuharakisha njia yake ya maendeleo na kufanya bidhaa na huduma zake kuwa na ufanisi Iran na kimataifa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Makao Makuu Maalum kwa ajili ya Maendeleo ya Nanoteknolojia katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Sayansi na Teknolojia, bidhaa na huduma za nanoteknolojia za makampuni ya Iran yanayotumia maarifa katika nyanja mbalimbali za ujenzi, optoelectroniki, dawa, afya na tiba, nguo na teknolojia nyinginezo zimesafirishwa katika nchi 47 ambazo zimeomba bidhaa hizo. Kati ya na nchi zilizoomba bidhaa hizo ni pamoja na Uturuki, Iraq, Lebanon, Afghanistan, Georgia, Syria, Russia, Pakistan, Tajikistan, India na Kazakhstan.

Kiasi kikubwa zaidi cha mauzo ya nano ya Iran ni kwa Uturuki yenye thamani ya dola milioni 13, Iraq yenye thamani ya dola milioni 12 na Lebanon yenye thamani ya dola milioni 3.4 mtawalia. Afghanistan, Georgia na Syria ndizo zinazofuata.

Sehemu kubwa zaidi ya mauzo ya nje ya bidhaa za nano za Iran inahusiana na sekta ya ujenzi, ambayo inachukua asilimia 53%.

EBOLA NCHINI UGANDA

Nchini Uganda mamlaka za afya zimetangaza mlipuko wa Ebola katika wilaya ya Mubende katikati mwa nchi hiyo baada ya Taasisi ya utafiti wa virusi nchini humo kuthibitisha kuwa kifo cha mwanaume mmoja kimesababishwa na ugonjwa huo wa Ebola wa aina ya virusi kutoka Sudan au #EbolaSudan.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni kanda ya Afrika iliyotolewa Septembe 20 mjini Brazaville, Congo na Kampala, Uganda ilisema uchunguzi ulitokana pia na vifo vya watu 6 wilayani humo mwezi Agosti.

Hii ni mara ya kwanza kwa zaidi ya muongo mmoja, Uganda inapata aina hiyo ya Ebola, amesema Dkt. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO, kanda ya Afrika akisema “tunashirikiana kwa karibu na mamlaka za kitaifa za afya Uganda ili kuchunguza chanzo cha mlipuko huu na wakati huo huo tunasaidia harakati za kusambaza hatua za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.”

Amesema jambo linalotia moyo ni kwamba, Uganda si ngeni katika hatua fanisi za kudhibiti Ebola, “tunashukuru kwa utaalamu wake, hatua zimechukuliwa haraka kutambua virusi hivyo na tunategemea utaalamu na ufahamu huo katika kukomesha kusambaa zaidi.”

Tayari WHO imetuma timu za kusaidia kutoa huduma kwa wagonjwa. Kumekuweko milipuko saba ya aina hii ya Ebola ambapo minne imekuwa nchini Uganda na milipuko mitatu nchini Sudan. Mara ya mwisho Uganda iliripoti mlipuko huo mwaka 2021.

Mwaka 2019 Ebola yenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ikipatiwa jina #EBolaZaire ililipuka Uganda na virusi hivyo vilitokea DRC. Chanjo iliyoko ni ya EbolaZaire na si EbolaSudan.

Ingawa chanjo ya Ebola, imeonekana fanisi katika kudhibiti kuenea kwa Ebola, chanjo hiyo aina ya Ervebo (rVSV-ZEBOV) ina ufanisi katika kukabili EbolaZaire na si EbolaSudan.

Ebola ni ugonjwa hatari ambao unaweza kusababisha kifo na hupata binadamu na nyani. Ina aina sita ya virusi, ambavyo vitatu kati yavyo ni Bundibugyo, Sudan na Zaire na vimeshasababisha milipuko. 

Wakati huo huo, Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amethibitisha kifo cha daktari Muhammed Ali (37) raia wa Tanzania kilichotokana na ugonjwa wa Ebola huko nchini Uganda.

Mohammed ambaye alikuwa anasomea shahada ya pili nchini humo, anakuwa daktari wa pili kupoteza uhai kufuatia ugonjwa wa virusi vya Ebola vilivyozuka mwezi Septembe nchini Uganda.

TABIANCHI NA MARADHI YA SARATANI

Utafiti mpya uliosimamiwa na Taasisi ya Francis Crick huko London, mji mkuu wa Uingereza, umeongeza kwa kiasi kikubwa uelewa wa wanasayansi kuhusu jinsi uchafuzi wa hewa unavyoathiri ongezeko la maradhi ya saratani.

Taasisi ya Francis Crick ya London imetangaza kwamba matokeo ya utafiti mpya uliosimamiwa na taasisi hiyo yameleta mageuzi katika ujuzi na uelewa wa wanasayansi kuhusu jinsi ya kujitokea na kukua uvimbe wa saratani, na suala hilo linaweza kufungua njia ya kuzuia maradhi hayo.

Kulingana na Taasisi ya Francis Crick, utafiti huo mpya pia umesaidia kuelewa vyema uhusiano kati ya uchafuzi wa hewa na kuundika kwa uvimbe wa saratani.

Matokeo ya utafiti huo pia yanaonesha kuwa, ubora wa hewa unaendelea kuzorota duniani kote na kwamba viwango vya uchafuzi wa hali ya hewa unaotokana na kemikali na chembe chembe ndogo, vinachangia matatizo ya kupumua na vifo vinavyoweza kuzuilika duniani kote.

Mamilioni ya watu hupoteza maisha duniani kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa, mwaka 2012 pekee watu milioni 7 walifariki dunia kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa. Ripoti hiyo ya WHO ilisema kuwa: Kanda za Asia Mashariki na Kusini pamoja na Pasifiki Magharibi zimekuwa na kiwango kikubwa zaidi cha uchafuzi wa hewa ndani ya makazi na hata nje ya makazi ya watu na kwamba tatizo hilo linazihusu nchi tajiri na maskini.

 

Tags