Oct 30, 2022 05:33 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 2

Tunapasa kutambua kwamba fitna ni mbaya kuliko kuua kwa sababu fitna huzuia ustawi wa thamani za binadamu na wakati huo huo kuwanyima manufaa ya maisha yao ya humu duniani na ya huko Akhera.

Bismillahir Rahmanir Raheem.

...Fitina ni mbaya zaidi kuliko kuua.

Salamu ziwe juu ya wale wote wanaothamini dini, salamu ziwe juu ya watu ambao hata kama hawana dini lakini wako huru na nyoyo zao huchelea utu na thamani zake.

**********

Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba fikra za kijahili na tabia za kutumia mabavu za Makhawarij zilibakia katika kitovu cha historia ya Uislamu na cheche zake zilikuwa zikidhihiri mara kwa mara na kuudhuru Uislamu kwa njia moja au nyingine, jambo lililowafurahisha maadui wa dini hii tukufu na kuwafanya watafute na kubuni mbinu za kuchochea zaidi cheche hizo na hatimaye kuwasha moto mkubwa dhidi ya Uislamu na Waislamu. Baada ya kuaga dunia Ibn Taymiyya, cheche hizo za moto zilizimika na maadui wakapoteza kwa muda fursa ya kueneza uadui dhidi ya Uislamu. Takriban karne nne baada ya hapo yaani mwaka 1115 Hijiria sawa na 1703 ambapo Muhammad bin Abdul Wahhab alizaliwa katika jangwa la mbali katika kijiji cha Uyainah katika eneo la Najd, hakuna mtu aliyedhani kwamba mtoto huyo angekuwa misdaki na mfano halisi wa Hadithi inayohusiana na fitina za maadui dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Katika juzuu ya pili ya Sahihi Muslim ambacho ni kitabu chenye itibari na kinachoaminika sana mbele ya Ahlu Sunna, kuna hadithi ambayo imenukuliwa na Abdallah bin Omar, khalifa wa pili akisema kwamba Mtume (saw) alisikika akisema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Yabariki kwa wingi maeneo ya Sham na Yemen." Hapo kundi la Waimuni waliokuwa hapo walimwendea Mtume na kumuomba aliombee pia eneo la Najd ili lipate kunufaika na wingi wa baraka za Mwenyezi Mungu. Mtume hakulipa uzito ombi hilo bali waumini hao waliendelea kusisitiza aliombee eneo la Najd ili libarikiwe na Mwenyezi Mungu. Mtume (saw) akasema: "Hilo ni eneo la machafuko, fitina na zilzala na Pembe ya Shetani itadhihirikia huko." Wafasiri wanasema kuwa kusudio la Mtume kuhusu 'Pembe ya Shetani' ni umma au wafuasi wa shetani.

Baada ya kujuana na Hempher, jasusi wa Uingereza mjini Basra huko Iraq, Muhammad bin Abdul Wahhab ambaye alivutiwa sana na fikra za Ibn Taymiyya alishawishiwa na jasusi huyo abuni madhehebu mpya ili kwa madai yake apate kuunusuru Uislamu kutokana na upotevu. Alianza kusambaza na kueneza fikra zake potovu kuhusu Uislamu akiwa katika kijiji alikozaliwa yaani Uyainah lakini akafukuzwa kwenye kijiji hicho na wakazi na jamaa zake wa karibu kutokana na fikra hizo zilizokuwa zikishajiisha utumiaji mabavu na ukatili dhidi ya Waislamu. Baada ya kufukuzwa katika kijiji hicho Muhammad Bin Abdul Wahhab aliamua kuelekea katika kijiji kingine cha Dir'iyyah ambapo aliendelea kueneza fikra zake hizo potovu na zilizo kinyume na mafundisho ya Uislamu halisi. Akiwa huko alifuatwa na Hempher ambaye aliendelea kumshajiisha aendelee kueneza fikra hizo na hata kumuunganisha na Sheikh wa kijiji hicho. Mwaka 1744 ukoo wa Aal Saud ambao ndio waliokuwa wakitawala eneo hilo la Dir'iyya walimkaribisha na kuungana na Muhammad bin Abdul Wahhab. Muungano huo ambao ungalipo hadi leo ndio uliopelekea kubuniwa kwa harakati ya kisiasa na kimadhehebu ya Uwahabi. Wakati huo muungano huo ulipelekea kubuniwa kwa jeshi dogo la kijijini ambalo taratibu lilistawi na kuwa genge la mauaji  na ukatili katika pembe zote za Saudi Arabia. Baada ya muda genge hilo lilibadilika na kuwa tishio kubwa la usalama katika nchi hiyo.

Muhammad bin Abdul Wahhab akiwa na Muhammd Aal Saud

Haukupita muda mrefu kabla ya jeshi hilo la hofu kuanza kuyashambulia makabila, vijiji na miji ya karibu ambapo lilifanya mauaji makubwa na kupora mali za miji hiyo na kuwapa wakazi wa Dir'iyya. Mali hizo zilizoporwa zilikuwa ni za wakazi na Waislamu wa Najd ambao licha ya kuswali msikitini na kutekeleza ibada nyingine za dini lakini walituhumiwa na wafuasi wa Bin Wahhab kuwa ni makafiri na hivyo kuhalalisha mali na damu zao. Wanahistoria wameandika kuhusiana na mauaji na uporaji huo wa kutisha dhidi ya Wislamu na kusema kuwa ukatili uliofanywa dhidi yao ni mkubwa na kwamba hauwezi kubainishwa kwa maneno.

**********

Mwaka 1216 Hijiria sawa na 1802 Miladia jeshi la Saudi Arabia na la Kiwahabi liliushambulia mji mtakatifu wa Karbala. Lilishambulia haram tukufu ya Imam Hussein, mkujuu wa Mtume Mtukufu (saw) na kuua kinyama zaidi ya watu elfu nne wasio na hatia katika mji huo. Unyama na ukatili wa jeshi hilo la Kiwahabi la Saudia haukuelekezwa tu kwa Mashia bali mwaka mmoja baada ya mauaji hayo ya kutisha ya mjini Karbala, jeshi hilo pia lilifanya hujuma nyingine kama hiyo dhidi ya wakazi wa Taif nchini Saudia kwenyewe. Liliwakata vichwa kinyama watoto waliokuwa vifuani mwa mama zao na kuwachinja bila huruma kwa mapanga watu waliokuwa wakifundishwa Qur'ani kwenye madrasa. Lilishambulia misikiti, kuteketeza moto na kuchanachana vitabu vya dini ikiwemo Qur'ani Tukufu na nakala za vitabu vya Sahih Bukhari na Sahih Muslim, vilivyopatikana kwenye misikiti hiyo.

Baada ya kuuharibu mji wa Najd jeshi hilo lilielekea katika mji mtakatifu wa Makka, ambapo Mawahabi waliwaandikia barua viongozi wa mji huo wakiwataka wakubaliane na fikra na itikadi zao za kidini, lakini wanazuoni na mamufti wa mji wa madhehebu zote nne za Suni katika mji huo walikataa takwa hilo na kutoa fatwa ya kupigana jihadi dhidi yao.

Mwaka 1219 Hijiri Mawahabi waliuzingira mji mtakatifu wa Makka katika kila upande na kuzuia chakula cha dharura kuingizwa katika mji huo. Wakazi wa mji huo waliteseka na kakumbwa na baa la njaa kali kiasi kwamba hata hawakujali kula nyama ya paka na mbwa na ngozi zilizokauka za wanyama ilimuradi tu kuokoa maisha yao. Njaa ilikuwa kali na bei ya bidhaa za msingi kupanda kiasi kwamba watu walishindwa kumudu na kupelekea wengi wao kupoteza maisha. Miili ya walioaga dunia ilitapakaa mjini na idadi ya wakazi kupungua sana kiasi kwamba safu ya kwanza ya watu waliosimama kuswali katika Masjidul Haram haikuwa ikijaa.

**********

Vitendo vya ugaidi na utumiaji mabavu vilivyotekelezwa na jeshi la Mawahabi wa Saudi Arabia viliwakasirisha wengi dfuniani. Khalifa wa Kiuthmania aliyekuwa akitawala wakati huo kwa jina la Abdul Hamid wa Pili na ambaye alichukuliwa kuwa mtawala rasmi wa Bara Arabu alitoa amri ya jeshi la Misri kuvamia bara hilo kwa ajili ya kuliadhibu jedhi la kigaidi la Saudia na Mawahabi. Mwaka 1818 Miladia jeshi la Misri likiongozwa na Ibrahim Pasha, mwanaye mtawala huyo wa Misri lilishambulia magaidi hao wa kiwahabi na kutokomeza kabisa makao makuu yao ya jangwani katika eneo la Dir'iyya. Jeshi la Misri liliwakamata mateka kiongozi wa Mawahabi Abdallah Aal Saud na watu wengine wawili katika wafuasi wao na kuwahamishia Misri. Viongozi wengine wa magaidi katika ukoo wa Aal Saud na Mawahabi pia walipelekwa uhamishoni nchini Misri. Pamoja na hayo lakini huo haukuwa mwisho wa pote hilo potovu la Mawahabi na watawala wengine wenye uchu wa madaraka katika ukoo wa Aal Saud. Baada ya kunyongwa Abdalla Aal Saud huko Uturuki, mabaki ya Aal Saud na Mawahabi waliendelea kuwatazama Waislamu kuwa maadui wao na Waingereza na Magharibi kwa ujumla kuwa marafiki zao halisi.

Hatimaye kizazi cha Abdalla na waungaji mkono wake kilifanikiwa kuasisi utawala wake katika ardhi ya Bara Arabu, lakini pamoja na hayo malumbano ya kiukoo ndani ya ukoo wa Aal Saud kwa upande mmoja na nguvu ya ufalme wa Othamnia katika eneo kwa upande wa pili vilizuia kuasisiwa kwa dola la Wasaudia na Mawahabi lenye nguvu katika ardhi hiyo. Mwaka 1843 Faisal bin Turki alitoroka kutoka uhamishoni mjini Cairo na kurejea Riyadh. Suala hilo lilisadifiana na kuongezeka kwa siasa za kikoloni za Uingereza za kuimarisha ukoloni wake Mashariki ya Kati, suala lililochukuliwa kuwa fursa nzuri sana na ukoo wa Aal Saud na washirika wake katika eneo hilo.

************


Kanali Lewis Pelly

Mfalme Faisal ambaye katika kipindi hicho alikuwa amefanikiwa kuimarisha utawala wake kwa kiwango fulani mjini Riyadh alianzisha mashauriano ya ushirikiano na Uingereza, jambo lililoivutia nchi hiyo ya Magharibi na kuipelekea kumtuma mjumbe wake Kanali Lewis Kelly mjini humo mwaka 1865 kwa ajili ya kufuatilia suala hilo na kutiliana saini mkataba wa mapatano na watawala wa Saudia na Mawahabi.

Mwaka mmoja baadaye, Faisal alitiliana saini na Uingereza mkataba wa urafiki ambapo kwa mujibu wa mktaba huo, Saudia ilikubali kuisaidia Uingereza kueneza satwa yake ya ukoloni Mashariki ya Kati ambapo watawala wa ukoo wa Aal Saud na Mawahabi wangepewa fedha na silaha kutoka kwa serikali ya London. Mkataba huo wa urafiki kati ya watalawa hao na Uingereza uliamsha hasira kubwa ya Waarabu na Waislamu ndani na nje ya Bara Arabu. Jambo hilo lilipelekea mwaka 1891 utawala wa Othmania kuwashambulia watawala wa Aal Saud na Mawahabi kwa mara ya pili mjini Riyadh lakini kwa mara nyingine tena baadhi yao wakafanikiwa kukimbia. Walikimbilia Kuwait ambayo katika kipindi hicho lilikuwa koloni la Uingereza na kuiomba nchi hiyo ya Magharibi msaada kifedha na silaha kwa ajili ya kujiimarisha tena huko Bara Arabu.