Nov 10, 2022 17:39 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (44)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 44 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho maudhui yake ya leo itahusu umuhimu na udharura wa kuchunga akhlaqi za kiuchumi katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Mpendwa msikilizaji, katika mfululizo huu wa mwisho wa maudhui ya "Akhlaqi za Kiuchumi" katika Uislamu tutazungumzia suala muhimu sana la "kupambana na ufisadi wa kiuchumi". Ufisadi wa kiuchumi ni mithili ya mchwa wanaoweza kumomonyoa na kuangamiza kidogokidogo nguzo imara za kiuchumi za jamii na mfumo wowote ule; na kwa kusababisha changamoto na miparaganyiko isiyoweza kudhibitika, husambaratisha kikamilifu misingi mikuu ya mfumo wowote ule wa nchi.

Moja ya mambo muhimu zaidi yenye kusababisha ufisadi kwa mtazamo wa utamaduni wa Uislamu unaopiga vita ufisadi katika uga wa uchumi ni mwenendo mchafu wa "ulajiriba". Mlariba ni mtu ambaye ili aweze kujipatia utajiri wa harakaharaka, huwategea watu ambao, kutokana changamoto na dhiki za maisha hulazimika kumwendea yeye kwa ajili ya kutatua shida na matatizo yao ya kiuchumi; ambapo walariba wanaotafuta mwanya wa kujinufaisha, huitumia kikamilifu fursa hiyo ili kuwatimizia haja zao watu wenye shida, lakini mkabala wake, wao kujipatia faida nono. Na kwa kuendeleza mwenendo huo, kwa upande mmoja, hutajirika kwa kasi bila kufanya kazi ya uzalishaji au hata kujishughulisha na jambo lolote; na kwa upande mwingine, huwanakamisha na kuwaharibia maisha yao wadaiwa wao, ambao hawana uwezo wa kulipa mikopo na madeni yenye riba inayoongezeka siku baada ya siku.

Katika utamaduni wa kiuchumi wa Uislamu, upataji faida wa aina hii kwa njia ya dhulma na unyonyaji kupitia vyanzo vya kiuchumi umekosolewa na kukemewa vikali na dini hiyo, kufika hadi ya kufananishwa na kupigana vita na Mwenyezi Mungu, kama inavyoeleza aya ya 278 na 279 za Suratul-Baqarah ya kwamba:  Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe

Jambo jengine lenye madhara kwa mfumo wa uadilifu wa kiuchumi wa Uislamu ni walariba kujikurubisha na watawala na mahakimu wa mfumo wa mahakama ili waweze kutumia satua na ushawishi wao kuhodhi mali za watu bila ya haki na kujizidishia utajiri wao wa harakaharaka. Katika kukabiliana na kukataza njia hizo za kidhulma na kiuonevu, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya 188 ya Suratul-Baqarah: "Wala msiliane mali zenu kwa baat'ili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua".

Tunapotupia jicho kijuujuu mihimili ya nguvu na madaraka tokea zama zilizopita za historia hadi za sasa tunaukabili ukweli mchungu, nao ni kwamba, matajiri wenye tamaa na wanaoogolea kwenye raha na wasiofahamu shida ni kitu gani wamekuwa wakijiweka karibu na watawala wa kiimla wanaoishi raha mustarehe kwenye makasri na maghorofa waliyojijengea kwa kupora na kukomba maliasili na utajiri wa mataifa yao. Matajiri hao waliotajirika kwa njia za riba na unyonyaji huamua kuchota sehemu ya mali na utajiri wao kuwaneemesha watawala hao madhalimu, lakini kwa kufanya hivyo, huweza mkabala wake kupata mali na utajiri mkubwa zaidi na wa harakaharaka. Lakini katika mfumo wa uadilifu wa kiuchumi wa Uislamu, unakemewa vikali mwenendo wowote ule wa kujiweka karibu, kujipendekeza na kuwarubuni walioshika hatamu za madaraka ili kujipatia mali na utajiri haramu; na hakuna shaka yoyote kuwa wanaofanya hayo watafikwa na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu.

Inafaa kuashiria pia hapa kuwa, masuala ya uharibifu yanayoweza kuukengeusha mfumo wa kiuadilifu wa kiuchumi na kuuweka mbali na mkondo wake wa kidini na kiutu yanahitaji uhakiki na uchambuzi mpana, ambao hauwezi kufanywa katika muda mfupi wa mfululizo huu wa "Akhlaqi za Kiuchumi". Kwa kutoa mfano, katika ulimwengu wa uchumi, kuna mambo kadhaa haribifu kwa uchumi kama ubadhirifu, magendo ya bidhaa, madawa ya kulevya, uporaji vyanzo vya mafuta, uporaji maliasili na mengineyo yanayofanana na hayo, ambayo kila moja peke yake lina uwezo wa kuifanya mihimili mikuu ya wenye nguvu za utajiri na madaraka iimarike zaidi na kuyanakamisha mataifa yanayodhulumiwa na kunyongeshwa duniani kwa kuyazidishia madhila na ufukara. Lakini mbali na hayo, kama kuna kitu ambacho kinaonekana kwa uwazi zaidi katika mahusiano yote machafu na ya kidhulma ya kuchumi, ni utoaji na upokeaji rushwa au hongo.

Katika kulikemea ovu hilo, Bwana Mtune SAW amesema: "Mwenyezi Mungu amlaani mtoaji na mpokeaji rushwa na muunganishi baina ya wawili hao". (Kanzul-Ummal 150/80)

Kwa mtazamo wa Imam Ali AS, moja ya mambo yanayopelekea kuporomoka na kusambaratika mataifa na staarabu mbalimbali ni mwenendo huu muovu wa "rushwa", ambao mtukufu huyo ameuzungumzia kwa kusema: "kaumu za kabla yenu ziliangamia na kutoweka kwa sababu watu walinyimwa na kuzuiliwa haki zao na wakalazimika (kutoa rushwa) ili kupata haki (au mali) zao walizoporwa". (Nahjul-Balagha, Khutba 131).

Mbali na kusababisha madhara na mvurugiko wa kiuchumi na kijamii, moja ya athari mbaya za rushwa ni kupenya na kuathiri misingi ya kiitikadi pia, kwa sababu kwa mtazamo wa Uislamu, utoaji na upokeaji rushwa ni haramu na kwa hiyo unafungua njia katika jamii ya upataji na ulaji chumo la haramu ambao una madhara makubwa kwa akhera pia. Kuhusiana na ubaya mkubwa wa rushwa, Bwana Mtume SAW amesema: "Jiwekeni mbali na jiepusheni na upokeaji rushwa, kwani hapana shaka ni kukufuru hasa; na mchukuaji rushwa hataisikia hata harufu ya Pepo". (Biharul-Anwar 274/104)

Katika hitimisho la mazungumzo yetu haya kuhusu "Akhlaqi za Kiuchumi" katika Uislamu tueleze hapa kwamba, endapo watu watajichunga ipasavyo na kujiepusha na mambo yote yenye madhara na yaliyo haribifu kwa mfumo wa uchumi, jamii itabaki salama kwa kufutwa aina zote za ubaguzi na upendeleo na ufa wa kidhalimu wa matabaka; na haitasalia athari yoyote ya upokaji na ukanyagaji wa haki za watu katika jamii. Na kwa maelezo hayo basi mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa sehemu ya 44 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 45 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/

 

 

Tags