Nov 24, 2022 02:22 UTC
  • Alkhamisi tarehe 24 Novemba 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Mfunguo Saba Rabiuthani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Novemba 2022.

Miaka 771 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Muhammad bin Ahmad Dhahabi, anayejulikana kwa lakabu la Shamsuddin, mpokeaji wa Hadithi za Mtume (saw) na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu. Dhahabi alikuwa akipenda sana kukusanya Hadithi na alifanya safari nyingi katika pembe mbalimbali duniani ili kukamilisha elimu hiyo. Muhammad bin Ahmad Dhahabi alisimuliwa Hadithi nyingi kutoka kwa wazee na maulamaa katika safari zake hizo. Dhahabi alifuatilia matukio ya historia ya Uislamu na watu mashuhuri ya kuanzia wakati wa kudhihiri Uislamu hadi mwaka 704 na kuandika habari na matukuio ya wataalamu wa Hadithi wa zama hizo. Matukio hayo aliyakusanya katika kitabu alichokipa jina la Historia ya Uislamu. Vitabu vingine vya msomi huyo ni pamoja na Tabaqatul Qurraa, al Muujamul Saghiir na al Muujamul Kabiir.

Siku kama ya leo miaka 390 iliyopita, alizaliwa Baruch de Spinoza mwanafalsafa na mtaalamu wa elimu jamii wa Uholanzi. Spinoza alisoma kwa bidii na kukwea daraja za kielimu. Hata hivyo ukosoaji wake wa dini ya Kiyahudi ulimfanya akabiliwe na chuki na uhasama wa maulama wa dini hiyo. Njia na fikra za kifalsafa za Spinoza zilikaribiana na itikadi za kisufi. Msomi huyo wa elimu ya falsafa wa Uholanzi ameandika pia vitabu kadhaa kama The Philosophy of Spinoza na The Road to Inner Freedom. Baruch de Spinoza alifariki dunia mwaka 1677.

Baruch de Spinoza

Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, Michael Faraday mwanafizikia stadi wa Kiingereza aligundua mkondo wa umeme unaojulikana kitaalamu kama ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Faraday alizaliwa mwaka 1791 na awali alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza vitabu. Ni kipindi hicho ndipo taratibu alipoanza kusoma vitabu mbalimbai na kuanza kuvutiwa na masuala ya kielimu. Miaka michache baadaye akawa msaidizi wa maabara. Akiwa katika maabara hiyo Faraday alifanya utafiti mwingi kuhusiana na jinsi ya kutengeneza balbu za umeme. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.

Michael Faraday

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mkubwa wa Ufaransa, Henri Toulouse Lautrec. Familia ya Lautrec ilikuwa ya kipato cha wastani na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi ya kimaisha, Lautrec alitokea kuwa miongoni mwa wasanii mashuhuri na hodari wa Ufaransa kutokana na kipawa chake kikubwa. Msanii huyo alifariki dunia mwaka 1901.

Henri Toulouse Lautrec

Miaka 116 iliyopita katika siku kama ya leo ambayo ni sawa na tarehe 3 Azar mwaka 1285 Hijria Shamsia, gazeti la 'Majlis' lililokuwa na kurasa 8 lilianza kuchapishwa nchini Iran. Mhariri Mkuu wa gazeti hilo alikuwa Adib al Mamalik Farahani ambaye alikuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa zama hizo. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri yaani Bunge la Iran.

Siku kama ya leo miaka 22 ilioyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani. Alizaliwa mwaka 1303 Hijria Shamsia katika familia ya kidini katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya masomo ya mwanzo alielekea Karbala nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Alifanya utafiti mkubwa kuhusu dini na madhehebu mbalimbali na kuwa gwiji katika taaluma hiyo. Wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Rouhani alikuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran katika mapambano yao dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah wakiongozwa na hayati Imam Khomeini. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya "Firqatus Salafiyyah", "Buhuth Ma'a Ahlisunnah Wassalafiyyah" na "Firaq wa Madhahibu Islamiyyah".

Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani

Na siku kama ya leo miaka 9 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi 6 zinazounda kundi la 5+1 zilitia saini makubaliano ya muda ya nyuklia mjini Geneva huko Uswisi. Kutiwa saini makubaliano hayo kulitayarisha uwanja mzuri na kufungua njia ya mazungumzo zaidi kati ya Iran na nchi hizo sita ambazo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Russia, China na Ujerumani kwa ajili ya kutia saini makubaliano kamili ya nyuklia na kuondoa hitilafu kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia hapa nchini, na mwishowe kufutwa vikwazo vya kidhalimu vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

 

Tags