Nov 28, 2022 04:55 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (45)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 45 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaanza kuzungumzia na kuchambua "Akhlaqi za Kisiasa" na nafasi na umuhimu wake katika utamaduni wa kisiasa wa Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Mojawapo ya usuli na msingi unaohusu mada hii ni "mfungamano wa dini na siasa". Lakini kwa vile ulimwengu wa siasa umeiachia jamii ya mwanadamu kumbukumbu chungu, za kuumiza na zisizopendeza, kiumbe huyo hupitikiwa kila mara akilini mwake na suali kwamba, inawezekana kweli kuwepo uhusiano na mfungamano kati ya dini na siasa? Sababu ni kuwa, wakati mafunzo na mafundisho ya dini za mbinguni yametawaliwa na masuala ya maadili mema ya kiakhlaqi na thamani aali na tukufu za kiutu, katika ulimwengu wa siasa sio tu haionekani alama yoyote ya maadili ya kiakhlaqi na kiutu, bali tunachokishuhudia ndani yake ni hila na ghilba, dhulma na ukanyagaji haki, ubaguzi, maadili machafu, ubabe na uwashaji moto wa vita. Katika hali kama hiyo itawezekanaje kuleta mfungamano baina ya dini na siasa?

Hapana shaka yoyote kuwa, kutokana na ufahamu tulionao juu ya watawala madhalimu na madikteta tuwaonao, fikra ya kutenganisha dini na siasa itakuwa na mantiki na itakubalika kikamilifu; lakini kama tutautafakari ulimwengu wa siasa unaozungumziwa na Qur'ani na Uislamu wa asili, tutabaini kuwa mfungamano wa dini na siasa ni kitu kisichoweza na kisichopasa kutenganishwa. Kwa maana kwamba, ulimwengu wa siasa unaotokana na viwili hivyo unajengwa juu ya msingi wa uadilifu, uhuru wa kweli, udugu, usawa na upendo kwa watu. Ni ulimwengu ambao ndani yake, utamaduni wa waja safi na maadili mema ndivyo vinavyotawala katika jamii.

Abdullah Ibn Abbas anasimulia kuwa, katika zama za Ukhalifa wa Imam Ali (AS), ambapo hatamu za uongozi wa Ulimwengu wa Kiislamu zilikuwa mikononi mwa mtukufu huyo, siku moja alikwenda kwa Imam Ali akamkuta anashona kiatu chake kilichokuwa kimefumuka; akapigwa na mshangao kumuona anafanya hivyo. Amirul-Muuminin Ali AS akamuuliza Ibn Abbas: "Uonavyo wewe, kiatu hiki kina thamani gani?" Ibn Abbas akasema: Hakina thamani yoyote. Imam Ali akamwambia: "Thamani ya kiatu hiki kilichofumuka na kuchakaa ni kubwa zaidi kwangu mimi kuliko kuongoza utawala juu yenu, isipokuwa kama kwa kuongoza huko nitasimamisha uadilifu, nitatetea haki zilizoporwa au kuiondoa batili". (Nahjul-Balaghah, 33).

Lakini mbali na hilo, baada ya wale walioongoza mpango wa Saqifa, kumweka yeye kando ya nafasi yake halisi ya uongozi wa jamii na kuamua wao kushika hatamu za madaraka, ilipofika hatua ya akthari ya watu katika jamii ya Waislamu kuchoshwa na utendaji wa waliokuwa na uchu wa madaraka na wakaamua kumkimbilia yeye Ali AS na kum'bai, mtukufu huyo aliwatolea hotuba iliyobainisha na kuonyesha kwamba katika siasa za Uislamu wa asili suala la kugombea madaraka halina nafasi yoyote; na lengo kuu la mtu kukubali kubeba dhima ya uongozi na madaraka katika jamii ya Kiislamu ni kuwatumikia na kuwapigania haki zao wale wanaonyongeshwa. Katika hotuba yake hiyo, Imam Ali AS aliwaeleza watu sababu ya kukubali kubeba dhima ya uongozi wakati huo kwa kusema: "Kama isingelikuwa umati mkubwa wa watu waliohudhuria, na kujitokeza kwao kulikotimiza dhima kwangu, na kama ningekuwa na udhuru wa kutoa, na laiti isingekuwa kwamba Mwenyezi Mungu amechukua ahadi kwa maulamaa kwamba wasinyamazie ulafi wa madhalimu na kiu ya waonevu, ningeliziacha hatamu za ukhalifa na kujiweka kando kama siku ya mwanzo (nilipofumbia macho haki yangu ya kisheria kwa ajili ya kulinda Uislamu na umoja wa umma wa Kiislamu)". Nahjul-Balagha, khotuba 3.

Lakini licha ya utaalamishaji na ueleweshaji wote huo, kundi moja la watu waliokuwa na uono finyu na ukereketwa wa kijazba wa dini wakiamini kwamba dini na siasa hazitangamani. Wakitilia shaka ulazima wa kuunda utawala wa Kiislamu na wakidhani kwamba inawezekana kutekeleza sheria na hukumu za Kiislamu pasi na kuasisi utawala wa kidini. Katika kuwajibu watu hao na kuuvunja mtazamo wao potofu, Imam Ali AS aliwaambia: "Ni sawa kwamba utawala hasa ni wa Mwenyezi Mungu, lakini inapasa sheria za Mwenyezi Mungu zitekelezwe na waja wema. Na kwa upande mwingine, (akili inahukumu kuwa) watu wanahitaji kuwa na kiongozi, awe mzuri au mbaya; kwa sababu ni kwa kuwepo utawala ndipo aliye muumini na mshika dini huweza kufanya anayokusudia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, aliyekufuru naye hupata kufaidika na dunia yake, masuala ya jamii huweza kuendeshwa na utawala kwa kodi kukusanywa, kupambana na adui, na amani na haki ya mnyonge kupatikana na kuchukuliwa kwa mwenye nguvu mpaka wema wapate utulivu…Nahjul-Balagha Khutba 4.

Sifa nyingine ya kipekee ya siasa halisi ya Kiislamu na kidini ni kwamba, kinyume na wale ambao muelekeo wao ni wa kutowahesabia wananchi kuwa na haki yoyote na kuwafanya kama watumwa ili kuweza kulinda maslahi yao yaliyo dhidi ya ubinadamu, katika mfumo wa utawala wa Kiislamu, kuna haki za baina ya pande mbili, yaani wananchi na viongozi wa jamii, ambazo lazima zitekelezwe kwa manufaa ya pande hizo. Kuhusiana na nukta hii pia, Imam Ali AS amesema: "kila pale umma unapochunga haki za utawala; na utawala nao ukachunga haki za watu, hapo ndipo "haki" inapotawala katika jamii ya watu. Ni wakati huo ndipo misingi ya dini inapokuwa imara. Ni hapo ndipo ishara na athari za uadilifu zinapodhihiri na kuonekana bila upotoshaji wa aina yoyote; na ni katika hali hiyo ndipo mila na desturi zinapofuata mkondo wake sahihi, mazingira na zama zinapovutia na kupendeza na adui anapovunjika moyo na kupoteza matumaini kwa kutoitazama kwa uchu na tamaa jamii ya aina hiyo iliyo imara na madhubuti kwa kila hali". Nahjul Balagha, Khutba ya 216

Mojawapo ya mambo muhimu zaidi yanayotoa msukumo wa utekelezaji wa haki za baina wananchi na utawala ni viongozi kutolitazama suala la kushika madaraka kama fursa kwao; kwani wakiwa na mtazamo huo watakengeuka mkondo wa utekelezaji "haki", na haki za watu katika jamii zitapondwa na kukiukwa tu. Ni kwa sababu hiyo, ndio maana katika barua yake kwa Liwali wa Azerbaijan, Imam Ali AS aliandika hivi: "Usije ukadhani kama mamlaka uliyokabidhiwa ni mawindo uliyoyatia mkononi. Hiyo ni amana iliyokabidhiwa kwako na kwa walio juu yako inayotaka uchunge haki za watu na wala usiamiliane na watu kwa mabavu na kwa ubaya". Na kwa barua hiyo ya 5 ya Nahjul-Balagha, mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa sehemu ya 45 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 46 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/