Jan 20, 2023 17:27 UTC
  • Ustawi wa Iran katika teknolojia za nyuklia na anga za mbali

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya taarifa na mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ametangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejitosheleza katika uga wa teknolojia ya nyuklia.

Teknolojia ya nyuklia ni moja ya teknolojia za msingi ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya teknolojia mpya na maendeleo ya viwanda vipya. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imegeukia matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia kwa kutegemea uwezo wa wataalamu wa ndani na imethibitisha kwa nia njema kwamba haina malengo mengine isipokuwa matumizi ya amani na viwanda ya nishati hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni, wanasayansi wa masuala ya nyuklia wa Iran wamefanikiwa kuzalisha aina mbalimbali za bidhaa za matumizi zinazohitajika na vituo vya kisayansi na utafiti nchini; Kwa mfano, wanasayansi wa Iran wamefanya uvumbuzi muhimu katika uwanja wa uchunguzi na matibabu ya saratani, ambayo itaingia katika hatua ya majaribio ya kliniki. Iran ni miongoni mwa nchi 5 bora duniani katika eneo hili.

Katika suala hili na kwa mujibu wa IRNA; Mohammed Eslami, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, aliyasema Januari 11 katika hafla ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuuawa shahidi wanasayansi wa nyuklia wa Iran, kwamba Iran imejitosheleza katika kutoa vifaa vilivyokuwa chini ya vikwazo na sasa ina uwezo wa kusafirisha nje bidhaa hizo." Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo imekuwa nchi yenye uwezo kamili katika uga wa teknolojia ya nyuklia na imeweza kupata mafanikio makubwa kwa kutegemea nguvu za ndani."

Akizungumzia uwezo wa dawa za radiopharmaceuticals, Eslami amebainisha kuwa: "Uwezo tulionao katika dawa hizi za radiopharmaceutical umeifanya Iran kuwa moja ya nchi za kwanza duniani katika sekta hii."

Akizungumzia matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika kutibu saratani, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amebaini kuwa: "Athari za matibabu ya plasma ni kuzuia seli za saratani kutekeleza hujuma mwilini, na bila athari za chemotherapy, tiba ya plasma inaweza kukusanya na kusambaratisha seli zinazohusika katika kueneza saratani na hii ni hatua kubwa katika matibabu."

Ustawi wa teknolojia ya anga za mbali Iran

Shirika la anga za mbali la Iran hivi karibuni limefanya kikao chake cha kwanza rasmi cha utekelezaji wa mpango wa miaka kumi ya anga za mbali na hivyo kuanza kivitendo utekelezaji wa mpango huo wa kimkakati.

Kwa mujibu wa mpango huo, mnamo miaka kumi ijayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itabadilika kuwa kitovu cha maendeleo ya teknolojia ya anga za mbali na utoaji huduma za upelekaji vyombo katika anga za mbali katika ukanda huu. Lengo hilo limepangwa kufikiwa wakati Iran imewekewa vikwazo na litafanikishwa kwa kutegemea uwezo wa ndani na utaalamu wa wanasayansi na wataalamu wa humu humu nchini.

Sekta ya anga za mbali inahesabiwa kuwa moja ya vipengee vinavyoakisi nguvu na uwezo wa nchi yoyote ile; na kwa upande wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika miaka ya karibuni, imepiga hatua kubwa na za mtawalia katika uga wa teknolojia ya makombora na anga za mbali.

Katika ramani ya mpango mkuu wa kisayansi nchini, uga wa anga za mbali umezingatiwa kuwa moja ya nyanja kuu za teknolojia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi na hata kupewa kipaumbele kikuu katika teknolojia za kisasa. Kuhusiana na suala hili, upelekaji mtu na utumaji satalaiti za mawasiliano ya simu katika anga za mbali ni suala lililotiliwa mkazo maalumu.

Tofauti ya mpango wa anga za mbali wa Iran na nchi zingine za ukanda huu wa Asia Magharibi ni kwamba, Iran imetegemea uwezo wake wa ndani na imeweza kupiga hatua kutokana na ubunifu wa wasomi na wanasayansi wa humu humu nchini.

Tunaweza kuitathmini teknolojia ya anga za mbali ya Iran kwa mitazamo miwili ya ndani na kimataifa. Kwa mtazamo wa ndani, mpaka kipindi cha kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilikuwa na antena na vyombo vichache tu vya kupokelea mawimbi ya satalaiti; na kwa upande wa maalumati ya kiufundi kuhusiana na satalaiti zenyewe, ujuzi wake ulikuwa wa kiwango cha sifuri. Kwa hivyo ilikuwa na uwezo wa kupokea baadhi tu ya mawimbi yanayorushwa kutoka nchi zingine. Lakini kuanzia kipindi cha vita vya miaka minane, Iran ilianza kujitutumua na kupiga hatua za kujiendeleza katika teknolojia ya anga za mbali kwa ajili ya ulinzi wa nchi; na kwa muktadha huo, vyuo vya anga za mbali vilianzishwa; na kuimarisha uwezo wa nchi katika uga wa anga za mbali ukazingatiwa na kupewa umuhimu maalumu.

Inakadiriwa kuwa, ifikapo mwishoni mwa utekelezaji wa mpango huo wa miaka kumi, mifumo 30 itakuwa imeshaanzishwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa vyombo vya serikali na wajasiriamali hapa nchini.

Hivi sasa, tayari kuna mifumo kumi inayotumika kwa ajili ya shughuli hizo au iko kwenye awamu ya ukamilishaji, lengo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran likiwa ni kuongeza idadi yake. Na hayo yanafanyika wakati maadui, kwa kutumia kila aina ya vikwazo, wamejaribu hadi sasa kuiwekea vizuizi Iran isiweze kupiga hatua kiuchumi na kielimu, ikiwemo katika sekta ya anga za mbali. Lakini pamoja na kuwekewa vizuizi na mashinikizo yote hayo, sasa hivi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inamiliki teknolojia mbalimbali za anga za mbali na zinazohusiana na masuala ya anga.

 

Uganda yatokomoeza Ebola

 

Uganda imetangaza habari ya kudhibitiwa na kutokomezwa mlipuko wa Ebola ambao umeua makumi ya watu nchini humo tangu Septemba mwaka uliomalizika 2022.

Tangazo hilo lilitolewa Jumatano Januari 11 na Jane Ruth Aceng, Waziri wa Afya wa Uganda katika hafla ya kuadhimisha mwisho wa mlipuko wa maradh hayo hatarishi.

Dakta Aceng amebainisha kuwa, 'Tumefanikiwa kudhibiti msambao wa Ebola nchini Uganda." Tangazo hilo limekuja baada ya Uganda kutoripoti kesi yoyote mpya ya ugonjwa huo ndani ya siku 42 kabla ya 11 Januari, kwa kuzingatia miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus ameipongeza Uganda kwa kufanikiwa kuudhbiti mlipuko wa Ebola. Uganda imetokomeza Ebola pasi na kuwepo chanjo iliyoidhinishwa kwa ajili ya spishi ya maradhi hayo iliyoripotiwa katika mlipuko wa sasa.

Takwimu za Wizara ya Afya ya Uganda zinaonesha kuwa, watu 55 wamefariki dunia kwa maradhi hayo katika mlipuko huu ulioisha, wakiwemo wahudumu sita wa afya; huku kesi 143 zikinakiliwa katika muda huo wa miezi minne.

Hapo awali Ahmed Ogwell Ouma, Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (AFRICA CDC) aliipongeza serikali ya Uganda kwa jinsi ilivyochukua hatua bora za kuzuia kuenea kwa virusi hivyo, akisema ilichukua takriban siku 70 kudhibiti hali hiyo.

China yazindua kituo cha afya Afrika

Na Waziri wa mambo ya nje wa China Qin Gang amesema China itatoa mchango mkubwa zaidi kwenye sekta ya afya ya Afrika na kwa maslahi ya watu wake.

Qin amesema hayo hivi karibuni kwenye sherehe ya kukamilika kwa mradi wa makao makuu ya Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Maradhi cha Afrika (Africa CDC) kwenye kitongoji cha kusini cha Addis Ababa.

Qin amesema ujenzi wa makao makuu ya Africa CDC ni mradi muhimu wa ushirikiano uliotangazwa na Rais Xi Jinping wa China kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika mwaka 2018 mjini Beijing, na pia ni mradi mwingine mkubwa kwa ushirikiano wa China na Afrika kufuatia Kituo cha Mikutano cha Umoja wa Afrika.

Qin ameeleza imani yake kuwa kutokana na juhudi za pamoja za China na Afrika, Africa CDC itatoa mchango mkubwa zaidi kwenye sekta ya afya na maslahi ya watu wa Afrika, na kuandika ukurasa mpya kwenye historia ya uhusiano kati ya pande hizo mbili.

 

Tags