Hakika ya Uwahabi 12
Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba Mawahabi na matakfiri hudai kuwa wao ni Masalafi yaani kuwa ni wafuasi wa watu wema waliotangulia katika historia ya Uislamu na ambao kimsingi ni masahaba na wafuasi wa masahaba wa Mtume Mtukufu (saw). Pamoja na amadai hayo lakini ukweli wa mambo unathibitisha kinyume chake ambapo tunaona kwamba Mawahabi wametoka nje kabisa ya itikadi na suna za Mtume na kufanya mambo kwa msingi wa itikadi za Makhawarij.
Katika ulimwengu wa leo tunaona kwamba kuna makundi mengi yanayodai kuwa ni ya Masalafi lakini hayafuati itikadi na mienendo kama ya Mawahabi wa kitakfiri. Leo tutazungumzia moja ya makundi hayo.
Bismillahir Rahmanir Rahiim. Tunaanza kwa jina la Mwenyezi Mungu wa wanaotenda mema, ambao hushindana katika kutenda yaliyo mema.
Hamjambo wapenzi wasikilizaji.
Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba Mawahabi na matakfiri hudai kuwa wao ni Masalafi yaani kuwa ni wafuasi wa watu wema waliotangulia katika historia ya Uislamu na ambao kimsingi ni masahaba na wafuasi wa masahaba wa Mtume Mtukufu (saw). Pamoja na amadai hayo lakini ukweli wa mambo unathibitisha kinyume chake ambapo tunaona kwamba Mawahabi wametoka nje kabisa ya itikadi na suna za Mtume na kufanya mambo kwa msingi wa itikadi za Makhawarij.
Katika ulimwengu wa leo tunaona kwamba kuna makundi mengi yanayodai kuwa ni ya Masalafi lakini hayafuati itikadi na mienendo kama ya Mawahabi wa kitakfiri. Leo tutazungumzia moja ya makundi hayo.
************
Mwaka 1324 Hijiria sawa na 1906 Miladia, takriban miaka 10 baada ya kuaga dunia au kwa mujibu wa baadhi ya kauli, baada ya kuuawa shahidi Jamal ad-Deen Asad Abadi, mtoto alizaliwa katika moja ya vijiji vya Misri, ambaye baadaye alifuata njia ya Seyyed Jamal Deen katika mapambano dhidi ya ukoloni, ubeberu na udikteta na kuanzisha umoja wa Kiislamu. Hassan al-Banna aliweka nyuma kipindi cha utotoni mapema sana ambapo akiwa na umri wa miaka 16 tu aliingia katika uwanja wa harakati za kijamii. Akiwa katika umri huo mdogo alishughulishwa sana na jinsi ya kukuza na kueneza fikra za kidini katika jamii, kuwafanya watu wafurahie maisha na kupigana dhidi ya fikra za kimaada na kidunia. Harakati hizo zilimpelekea aanzishe jumuiya ya Ikhwanul Muslimeen mwaka 1346 Hijiria (1927 Miladia) alipokuwa na umri wa miaka ishirini na mbili pekee, Jumuiya ambayo mwanzo ilikuwa na wanachama sita tu. Jumuiya hiyo ilipata haraka wanachama wengi nchini Misri na ikawa mojawapo ya harakati muhimu zaidi katika nchi hiyo. Katika maisha yake yote ya kijamii, Hassan al-Banna alijaribu kuufanya Uislamu wenye nguvu na hai kuwa msingi wa harakati na mawazo yake na daima aliepuka misimamo ya kufurutu ada na kupindukia mipaka katika dini. Aliuchukulia Uislamu kuwa dini isiyo na fikra za mgando wala kujitenga kijamii na wakati huo huo kujiweka mbali na fikra za kuwakufurisha Waislamu na utumiaji mabavu.
Mojawapo ya misingi muhimu ambayo Ikhwanul Muslimeen iliundwa juu yake ni kuepuka mifarakano na kusisitiza umoja wa Kiislamu. Fikra hii, ambayo lilibuniwa na Muhammad Abduh na Seyyed Jamaluddin Asadabadi, imelindwa katika misimamo na shughuli zote za Ikhwanul Muslimeen hadi leo. Ili kufikia lengo hilo, Muhammad Abduh, ambaye alikuwa mwanachuoni wa Kisunni, aliandika na kutoa maelezo juu ya kitabu mashuhuri cha Nahj al-Balaghah na kuanza kukifundisha katika vyuo tofauti vya Kisuni. Kwa mtazamo wake, watu wote wanaozungumza Kiarabu na Waislamu wanaamini kwamba maneno ya Imam Ali (as) ndiyo maneno matukufu, yenye ufasaha, yenye maana ya kina na yenye kupambanua zaidi baada ya Qur'ani Tukufu na maneno ya Mtume Mtukufu (saw).
Imani nyingine ya Ikhwanul Muslimeen ni kwamba hakuna mgongano au tofauti yoyote iliyopo kati ya Uislamu na taaluma nyinginezo au sayansi. Waislamu wanapaswa kujishughulisha na uzalishaji mali ili kuinua hali zao za maisha na za watu wengine, na wakati huo huo kuweka misingi ya uadilifu wa kijamii ili watu wote wapate fursa sawa za kijamii. Hassan al-Banna aliyachukulia malengo hayo yote kuwa yaliyotokana na thamani za kidini na sunna za "watangulizi wema" au kwa maneno mengine Salaf Swaleh, na ndio maana akajiita yeye na wafuasi wake kuwa "Masalafi". Alisema katika moja ya hotuba zake: "Unaweza kusema kwamba Ikhwanul Muslimeen ni harakati ya Kisalafi, harakati ambayo imetokana na Sunna, na hakuna yeyote anayeweza kukuzuia kuwa na itikadi hiyo."
Bila shaka, kwa maelezo hayo mafupi ambayo tumeyapata kuhusu itikadi ya Ikhwanul Muslimeen, ni wazi kwamba fikra za Usalafi za Hassan al-Banna zinatofautiana sana na za Usalafi wa Mawahabi. Hassan al-Banna hakuunga mkono hata kidogo mbinu za kutumia mavabu na mauaji dhidi ya Waislamu, na hata alipinga vikali kuuawa kigaidi wapinzani wake. Aliamini kuwa mabavu na ugaidi si katika mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Hatimaye, alipokuwa na umri wa miaka 44 tu, Hassan al-Banna aliuawa shahidi na serikali ya Ufalme wa Misri kwa njia hiyo hiyo isiyo ya Kiislamu. Baada ya kuuawa shahidi Hassan al-Banna, jumuiya ya Ikhwanul Muslimeen imeendelea kuwepo na ndiyo jumuiya ya Kiislamu yenye ushawishi mkubwa zaidi katika vipindi vyote vya utawala wa kisiasa nchini Misri. Jumuiya hiyo daima imekuwa ikifuatilia kuanzishwa nchini serikali ya Kiislamu na kujitenga serikali za kifalme na kijeshi zinazotawala nchini humo. Wanachama wa Ikhwanul Muslimeen daima wamekuwa na uhusiano mzuri na Mashia ulimwenguni na hata wakati fulani waliunga mkono wazi wazi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuitaja kuwa nchi pekee ya Kishia duniani. Baada ya Hizbullah ya Lebanon kushinda vita vya siku 33 dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, Jumuiya ya Ikhwanul Muslimeen licha ya kuwepo mashinikizo makubwa ya kisiasa na kijeshi, iliandaa sherehe za ushindi na kiongozi wao akawahutubia wapiganaji wa Hizbullah na kusema: “Mumeyaletea fahari kubwa mataifa yote ya Kiarabu na Kiislamu...” Jumuiya ya Ikhwanul Muslimeen inajumuika na Waislamu wengine wote pamoja na wapigania uhuru ulimwenguni katika njia ya mapambano ya kuikomboa Palestina. Lengo la jumuiya hiyo ni kufikiwa uhuru wa nchi za Kiislamu na kukombolewa kutoka kwenye makucha ya ukoloni, ubeberu na udikteta, lengo ambalo ingali inaendelea kulipigania hadi leo.
Baada ya kujua harakati ya Ikhwanul Muslimeen na kutambua kwa nuhtasari malengo, sera, itikadi na mienendo yake na kuwa inatofautiana sana na ya Masalafi wa kitakfiri, tunaelewa vyema kwamba kuenezwa fikra za kukufurishwa Waislamu na kushajiishwa vitendo vya mabavu na ugaidi dhidi yao sio tu si katika matendo ya Salaf Swaleh bali ni mkungeuko na uzushi katika dini au hata ni njama kubwa inayoendeshwa dhidi ya Uislamu na Waislamu. Njama ambayo, kwa upande mmoja, kwa kuibua mgawanyiko, inalenga kuwaangamiza Waislamu kutokea ndani kwa kutumia machafuko, vurugu na ugaidi, na kwa upande mwingine, inalenga kuiweka dunia mbali na ukweli wa mafundisho halisi ya Uislamu safi ulioletwa na Mtume Muhammad (saw), kwa kuwasilisha sura potovu ya Uislamu kwa kudai kuwa ni dini inayoshajiisha vitendo vya mabavu na ugaidi. Ukweli wa njama hii unatudhihirikia wazi tunapochunguza kwa makini zaidi utendaji wa Mawahabi wa kitakfiri kuhusiana na malengo matukufu ya Waislamu kuhusu kadhia ya ukombozi wa Palestina. Nyaraka za kihistoria zinatuonyesha kuwa mwanzoni mwa kuundwa utawala wa Mawahabi wa kitakfiri huko Saudi Arabia, ukoo wa Al Saud ulitia saini makubaliano na serikali ya Uingereza, ambapo Abdul Aziz aliandika chini ya makubaliano hayo maneno yafuatayo: "Mimi, Mfalme Abdul Aziz bin Abdul Rahman as-Saud, ninakiri mara elfu kwamba kwa maoni yangu, kwenda na kuja Percy Cox, mwakilishi wa Uingereza Kubwa, na pia kupeanwa Palestina kwa Wayahudi au wengine kama inavyotaka Uingereza na kwa maoni yake, hadi siku ya Kiama, hakuna tatizo lolote.”
Mwanzoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, serikali ya Aal Saud ilitangaza kutoegemea upande wowote katika vita hivyo, lakini Marekani ilipoingia vitani na Waitifaki wakahitaji mafuta, utawala huo ulishirikiana na kukubali matakwa yao moja kwa moja. Msaada wa Aal Saud haukuishia tu katika kuuza mafuta, bali Mawahabi waliwaruhusu Wamarekani kuanzisha kituo cha anga huko Dhahran, Saudia na ili kuonyesha zaidi 'ukarimu' wao, waliruhusu bandari zao zote kutumiwa na manowari za Uingereza na Marekani. Sasa kwa hatua hiyo Abdul Aziz angeweza kusema kwa yakini kwamba alikuwa ametimiza ahadi zake zote kwa Wamagharibi. Moja ya matukio muhimu yaliyofuatia ushindi wa Waitifaki katika vita hivyo ni kwamba Palestina ilikabidhiwa kwa Mayahudi wa Kizayuni, na hiyo ikawa moja ya khiana kubwa za kihistoria kuwahi kufanywa na Mawahabi dhidi ya Waislamu. Huduma za Abd al-Aziz kwa Uingereza zilimfanya Churchill, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza kusema katika mojawapo ya matamshi yake kwamba: "Yeye (Abdu al-Aziz) ni rafiki mwaminifu katika mashaka na shida, na kama isingekuwa yeye, Mayahudi wasingeweza kupata hata haki yao ndogo kabisa."
Hata kama utawala wa Aal Saud umejaribu kila uwezalo katika miaka yote hii kuficha nafasi yake katika usaliti huu mkubwa dhidi ya umma wa Kiislamu, lakini nyaraka za kihistoria zilizoachwa nyuma tangu wakati huo zinaonyesha wazi ukweli kwamba Mawahabi wamekuwa wakishirikiana bega kwa bega na wakoloni pamoja na Wazayuni ambao ni maadui waliojitangaza wazi dhidi ya Uislamu.
Wapenzi wasikilizaji, tutaendelea kuchambua zaidi suala hili la ushirikiano wa Mawahabi na wakoloni na maadui namba moja wa Uislamu katika kipindi kijacho panapo majaaliwa. Basi hadi wakati huo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.