Sura ya Ash-Shuura, aya ya 11-14 (Darsa ya 887)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 887 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 11 na 12 za sura hiyo ambazo zinasema:
فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ۖ يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ
Muumba mbingu na ardhi, amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu, na katika wanyama hoa dume na jike, anakuzidishieni namna hii. Hakuna chochote kilicho mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
لَهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ
Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila kitu.
Katika darsa iliyopita tulieleza kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye walii na mstahiki wa kuwatawalia waja wake mambo yao, lakini baadhi ya watu hawako tayari kuukubali utawala na uwalii wa Allah na kutii sharia na maamrisho yake. Katika mwendelezo wa maudhui hiyo, aya tulizosoma zinasema: Ni Yeye Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi; na ndiye anayeendesha mfumo unaotawala viwili hivyo. Moja ya alama za tadbiri na hekima ya uumbaji wa Mola Mwenye Enzi ni kuwaumbia wanadamu wenza watokanao na wao wenyewe, ambao kwa upande mmoja wanawafanya wapate utulivu wa roho na nyoyo; na kwa upande mwingine ni sababu ya kuendelea kuwepo na kubaki kizazi chao. Lakini mbali na wanadamu, Mwenyezi Mungu ameweka utaratibu na mfumo huo wa uumbaji wa jozi za dume na jike kwa nyama hoa, yaani wanyama wa miguu minne pamoja na viumbe wengine hai ili vizazi vya viumbe hivyo pia viendelee kubaki. Basi je, kuna mtu yeyote duniani umjuaye mwenye ujuzi na uwezo kama huo? Na hii ni pamoja na kwamba, hakuna yeyote wala chochote katika ulimwengu kinachoshabihiana Naye au kilicho mfano wa Yeye; Naye ametakasika na kila kasoro na upungufu wa vingine vyote vilivyoko. Kwa masikitiko ni kwamba baadhi ya watu wanaitakidi kuwa, hata kama Mungu atakuwepo, basi baada ya uumbaji, amewaachia wanadamu wajiendeshee mambo yao wenyewe; na sasa hana nafasi yoyote katika masuala ya ulimwengu huu. Qur'ani tukufu inaupinga vikali mtazamo huu potofu na kueleza kwamba Yeye Allah SWT ndiye Muumbaji na ndiye pia Mwendeshaji wa masuala ya ulimwengu; tena ni msikiaji na mwonaji wa kila kitu. Katika lahadha hii, anayashuhudia yasemwayo na yaonekanwayo na funguo za hazina zote za mbingu na ardhi ziko mikononi mwake Yeye. Riziki za viumbe vyote, nazo pia ziko kwenye mamlaka yake. Na kwa kuzingatia maslaha yalivyo, humkunjulia riziki amtakaye; na kwa kuzingatia maslaha pia humkadiria amtakaye. Yote hayo yanafanyika kwa ujuzi na hekima yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kubaki kwa kizazi cha wanadamu kumefungamana na ndoa; tab'an ni ndoa baina ya mwanamke na mwanamme, si ndoa ya watu wa jinsia moja; uchafu ambao kwa masikitiko unaendelea kuzagaa siku hizi katika baadhi ya jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mwenyezi Mungu hana aliye mfano wake na si mhitaji wa mwenza kama walivyo wanadamu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Allah SWT hakuviacha viumbe vyake kama vilivyo na kuvisabilia mambo yao baada ya kuviumba; bali muda wote Yu mwenye kufuatilia na kusimamia mambo yao. Aya hizi zinatutaka tuelewe pia kuwa, kukunjuliwa au kukadiriwa riziki kuko mikononi mwa Allah, na wala hakumaanishi kurehemewa au kughadhibikiwa mtu na Yeye Mola. Kwani si hasha makafiri wakawa matajiri na wenye uneemevu, na waumini wakawa masikini na wenye dhiki ya maisha; kama inavyoweza kuwa pia kinyume chake.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 13 ambayo inasema:
شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ ۚ كَبُرَ عَلَى الْمُشْرِكِينَ مَا تَدْعُوهُمْ إِلَيْهِ ۚ اللَّهُ يَجْتَبِي إِلَيْهِ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَن يُنِيبُ
Amekupeni sharia ya Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayo waitia. Mwenyezi Mungu humteua kwake amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye.
Aya hii inaashiria moja ya misingi ya wito wa Mitume na kueleza kwamba, kubaathiwa na kutumwa Nabii Muhammad SAW ni mwendelezo wa ujumbe uliolinganiwa na Mitume wengine katika zama zote za historia na kwamba wito wa tauhidi na kumwabudu Mola mmoja pekee si jambo jipya. Analowalingania watu Bwana Mtume SAW ndilo lile lile ambalo Mitume waliokuja kabla yake yeye pia waliwalingania watu wao. Mitume wote wa Allah wamekuja kuwaambia watu kwamba, ishikeni dini ya Mwenyezi Mungu na mtekeleze hukumu na maamrisho yake; acheni kufanya mambo kwa kufuata matashi yenu ambayo yanatokana na hawaa na matamanio ya nafsi zenu na zitiini amri za Mola wenu. Katika aya hii ya 13, neno dini limetajwa katika hali ya umoja, ikimaanisha kwamba chimbuko na asili ya dini ya Mwenyezi Mungu ni moja. Hata hivyo kutokana na mageuko kamilifu ya jamii ya mwanadamu, sharia na hukumu zilizoletwa na Mitume imebidi zipanuliwe na kustawishwa ili ziendane na mageuko hayo ya ukamilifu ya wanadamu katika zama mbalimbali za historia hadi kufikia marhala na awamu ya mwisho ya ukamilifu huo. Dini ya Uislamu, ambayo ni dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu imekuja na maandiko jumuishi na yaliyokamilika zaidi ya sharia za Mola kwa ajili ya walimwengu. Bahati mbaya akthari ya dini za mbinguni zilizotangulia zimeharibiwa kutokana na watu kufarikiana na kugawanyika matapo na mapote kutokana na ufahamu usio sahihi wa baadhi ya misingi ya dini au kwa sababu ya kuingiza kwenye dini matashi na mtakwa ya watu binafsi au ya makundi. Kwa hiyo Quráni tukufu inawatahadharisha wafuasi wa dini wajihadhari na balaa hilo kubwa la mfarakano katika dini. Nukta nyingine iliyoashiriwa katika aya hii ni kwamba, kuukubali wito wa tauhidi na wa imani ya Mungu mmoja asiye na mshirika ni jambo gumu na zito kwa washirikina. Sababu ni kwamba fikra batili za kishirki zimepenya na kujikita ndani ya nafsi zao kiasi kwamba wito wa tauhidi huwatia hofu na kiwewe. Kisha aya inaendelea kuashiria na kutilia mkazo nukta moja muhimu ya kwamba, uteuzi wa Mitume hauko mikononi mwa watu; ni Allah SWT Mwenyewe, kulingana na ujuzi na hikma yake amemteua kwa jambo hilo yule aliyemuona kuwa na ustahiki na kumkabidhi jukumu la kuwaelekeza watu kwenye uongofu. Ni wazi kwamba kila atakayemwamini Allah, anajiandalia mazingira ya kupata rehma zake na kunufaika na nuru ya uongofu wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, msingi wa wito wa Mitume wote ulikuwa mmoja: kushikamana na dini ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na kila aina ya mifarakano. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Nabii Nuh (as) alikuwa Mtume wa mwanzo aliyeteremshiwa mwongozo kamili wa sharia; na Bwana Mtume Muhammad SAW ni Mtume wa mwisho aliyeteremshiwa mwongozo kamili wa sharia. Na kwa kuwa Uislamu ndio dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu na unajumuisha ndani yake mafundisho ya Mitume wote waliotangulia, una sharia jumuishi zaidi na zilizokamilika zaidi. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kwamba, ikhtilafu na mifarakano ni mambo yanayoharibu dini na kuzuia mafundisho yake kutekelezwa kwa usahihi katika jamii. Wa aidha aya hii inatutaka tuelewe kuwa, uteuzi wa Mitume unafanywa na Mwenyezi Mungu Mwenyewe; Naye amewateua na kuwapa cheo hicho waja wake wastahiki, walio wasafi na watakasifu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 14 ambayo inasema:
وَمَا تَفَرَّقُوا إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى لَّقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۚ وَإِنَّ الَّذِينَ أُورِثُوا الْكِتَابَ مِن بَعْدِهِمْ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مُرِيبٍ
Na hawakufarikiana ila baada ya kuwajia ilimu kwa sababu ya husuda iliyo kuwa baina yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli kutoka kwa Mola wako Mlezi ya kuakhirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka palingeli hukumiwa baina yao. Na hakika walio rithishwa Kitabu baada yao wanakitilia shaka inayo wahangaisha.
Katika aya iliyotangulia tumeona kuwa, Mitume wote waliwatahadharisha watu na mifarakano katika dini, kwa sababu misingi ya dini zote za tauhidi ni mimoja; na haileti maana katika wakati mmoja ziwepo sharia na dini kadhaa za Mwenyezi Mungu kwa watu. Baada ya kuja Mtume yeyote mpya, watu wa zama zake wana wajibu wa kuupokea wito wake, na si kusema sisi tunafuata dini ya Mtume aliyepita, kwa hivyo watu wanaoamini na kufuata dini mpya ni makafiri. Kama maneno hayo yatasemwa ilhali watu wanaujua ukweli kuhusu Mtume mpya aliyewajia, basi yatakuwa hayatokani na sababu nyingine zaidi ya taasubi na husda. Mtazamo huu potofu ndio uliowafanya wafuasi wa baadhi ya dini kama Ukristo na Uyahudi katika zama zetu, wakatae kuufuata Uislamu. La kusikitisha ni kwamba, baadhi ya viongozi wa dini hizo na kwa sababu ya kutaka waendelee kubakiwa na wafuasi, kila siku hutumia nyenzo mbalimbali, hususan vyombo vya habari vya umma, kueneza shaka na upotoshaji kuhusu ukweli wa Uislamu na Quráni. Kwa kueneza kauli za ubabaishaji na utatanishi, wanawakosesha wafuasi wa dini hizo neema ya kuwa Waislamu itakayowafanya wale wote wanaomwabudu Mungu Mmoja wafuate dini moja na sheria moja. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba, kama ingekuwa Mwenyezi Mungu hakukata shauri kwamba makafiri watabaki hai na kuwa huru hadi muda maalum waliopangiwa, angehukumu baina yao kwa kuwaangamiza wafuasi wa batili na kuwapa ushindi wafuasi wa dini ya haki. Kwa kumalizia, aya inaashiria kundi la warithi wa vitabu vya mbinguni, ambao waliitilia shaka haki na wakakataa kuiamini. Kwa kuzingatia kwamba shaka yao hiyo inatokana na ukaidi na dhana mbaya kwa hivyo hawawezi kubainikiwa na ukweli. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, dini ya Allah ni moja; na mambo kama husda, taasubi na uadui ndiyo yanayosababisha mfarakano baina ya dini za mbinguni. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, maulamaa na wanazuoni wa dini wana jukumu la kufanya hima na bidii ya kuwaunganisha wafuasi wa dini zao, na si wao kuwa chanzo cha mfarakano. Vile vile aya hii inatuelimisha kwamba, kuwapa muhula wakosaji na wafanya madhambi ni moja ya kaida na utaratibu thabiti aliouweka Allah SWT. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa, kama shaka itatokana na sababu za kawaida, basi itaweza kumuondokea mtu kwa kuchunguza na kutafiti. Lakini kama chanzo chake ni ukaidi, taasubi na dhana mbaya, itamkosesha mtu fursa ya kuubaini na kuukubali ukweli na haki. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 887 ya Quráni imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki kama ilivyo na atupe taufiki ya kuifuata, na atuonyeshe batili kama ilivyo, na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/