May 24, 2023 09:46 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 890 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 24 ya sura hiyo ambayo inasema:

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّهِ كَذِبًا ۖ فَإِن يَشَإِ اللَّهُ يَخْتِمْ عَلَىٰ قَلْبِكَ ۗ وَيَمْحُ اللَّهُ الْبَاطِلَ وَيُحِقُّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ

Ati wanasema: Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Mwenyezi Mungu akipenda atapiga muhuri juu ya moyo wako. Na Mwenyezi Mungu anaufuta upotofu na anaithibitisha Haki kwa maneno yake. Hakika Yeye anayajua yaliyomo vifuani.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyozungumzia kuwapenda Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW kama malipo ya kimaanawi kwa ajili ya mjumbe huyo wa Allah. Aya hii tuliyosoma inasema: Pamoja na hayo, baadhi ya wanafiki wanamzulia uwongo Bwana Mtume kwa kudai kuwa, hayo ayasemayo yanatokana na yeye mwenyewe, lakini ameyanasibisha tu na Mwenyezi Mungu; na yale yeye anayosema kuhusu  Qur’ani, wahyi na mapenzi kwa Ahlul-Bayt, hayakuteremshwa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu akawajibu watu hao kwamba: Kama Mtume atafanya hivyo, Yeye Mola atapiga muhuri juu ya moyo wake na hataruhusu kunasibishiwa kitu ambacho hakumteremshia Mtume wake. Na sababu ni kwamba, ikiwa hatalizuia hilo, litasababisha watu kupotoka; na kutokea hayo hakuendani na hikma ya Mwenyezi Mungu ya kutaka watu wafuate uongofu. Ni kama ilivyoelezwa katika tarjumi ya aya ya 44 hadi 46 za Suratul-H’aaqqah ya kwamba: Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu, Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia, Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo! Sehemu inayofuatia ya aya hii inatilia mkazo nukta ya kwamba Mwenyezi Mungu anaifuta na kuifedhehesha batili; na haruhusu katu batili iingie ndani ya wahyi wake. Kwa maneno anayoyateremsha, Allah SWT anaifanya haki iwe thabiti na kusimama daima dawamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mtu muumini huwa anayaamini na kuyakubali yote yaliyoletwa na Bwana Mtume SAW kutoka kwa Mwenyezi Mungu; na si kuyakubali yale tu yapendwayo na nafsi yake na kuyapuuza au kuyakanusha yale isiyoyapenda. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Mwenyezi Mungu SWT hana mzaha na mtu yeyote. Kama ingetokezea hata Mtume wake kumnasibishia jambo lisilo sahihi, basi angemfedhehesha kwa kuuweka uongo wake hadharani na kumkatishia neema ya kupokea wahyi wake. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kwamba, kutawala haki na kutoweka batili ni ahadi ya hakika na isiyo na shaka ya Allah kwa waumini.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 25 na 26 ambazo zinasema:

وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ وَيَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ

Naye ndiye anaye pokea toba kwa waja wake, na anasamehe makosa, na anayajua mnayo yatenda. 

وَيَسْتَجِيبُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَيَزِيدُهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ وَالْكَافِرُونَ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ

Na anawaitikia wanao amini na wakatenda mema, na anawazidishia fadhila zake. Na makafiri watakuwa na adhabu kali.

Moja ya rehma na ukarimu mkubwa zaidi wa Allah SWT kwa wanadamu ni kwamba Yeye Mola ameuweka wazi muda wote na bila ya mpaka wowote mlango wa toba kwa waja wake wanaomkosea. Ni kinyume na sisi binadamu, ambao kwa kawaida mtu anapotufanyia dhulma na kutuomba radhi, lakini akarudia tena na tena kosa alilotutendea, hufika mahala tukakataa kuomba radhi kwake na wala hatuwi tayari tena kumsamehe. Lakini katika aya tulizosoma, Mwenyezi Mungu anasema, kila pale waja wangu watakapojuta kwa madhambi waliyofanya na wakaamua kutubia, wataukuta mlango wa toba uko wazi na nitawasamehe makosa yao. Hii ni pamoja na kwamba Yeye Mola ana habari za mambo yetu yote ya dhahiri na batini na hakuna chochote kinachofichika katika elimu na ujuzi wake. Uraufu na ukarimu wa Allah SWT kwa waja wake hauishii katika kuwasamehe madhambi yao tu, lakini pia kwa kuwatakabalia dua na maombi yao. Kwa maana kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu anayakubali maombi ya waja waliomwamini na wakafanya mema; lakini kubwa zaidi ya hayo, anawatunuku katika fadhila zake, yale ambayo hata hayajawapitikia katika fikra zao, na yaliyo bora zaidi ya vinavyoweza kuombwa katika mipaka ya akili ya mwanadamu. Na huo, ni upeo wa juu kabisa wa rehma na fadhila makhsusi za Mwenyezi Mungu kwa waumini. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, hakuna mkwamo na kugonga mwamba katika Uislamu. Mlango wa toba uko wazi muda wote; na mtu yeyote yule na katika mazingira yoyote yale, anaweza kutubia na kumuomba maghufira Allah na akasamehewa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaahidi wafanyao madhambi kuwa, kama watatubia, atawasamehe madhambi yao. Na kusema kweli kwa kuwapa ahadi hiyo, Allah SWT anawashajiisha waja wake hao kutubia. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, sharti la kutakabaliwa dua ni kumwamini Allah na kufanya amali njema.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 27 na 28 ambazo zinasema:

وَلَوْ بَسَطَ اللَّهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ وَلَٰكِن يُنَزِّلُ بِقَدَرٍ مَّا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ بِعِبَادِهِ خَبِيرٌ بَصِيرٌ

Na lau Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia riziki waja wake, basi bila ya shaka wangeliasi katika dunia. Lakini anaiteremsha kwa kipimo akitakacho. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.

وَهُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ الْغَيْثَ مِن بَعْدِ مَا قَنَطُوا وَيَنشُرُ رَحْمَتَهُ ۚ وَهُوَ الْوَلِيُّ الْحَمِيدُ

Naye ndiye anaye iteremsha mvua baada ya wao kukata tamaa, na hueneza rehema yake. Naye ndiye Mlinzi Mwenye kuhimidiwa.

Aya hizi zinaashiria msingi wa hikma ya Mwenyezi Mungu inayotawala juu ya mambo yote ya ulimwengu na kueleza kwamba, mfumo wa uumbaji umewekwa kwa mantiki ya kupima uwezo wa vitu na watu; na Mwenyezi Mungu ni Mweza wa kukipa kila kitu na kila mtu uwezo na nyenzo zaidi ya kiwango alichomjaalia, lakini kufanya hivyo hakuendani na hikma yake. Kwani kufanya hivyo kutafanya watu wamwasi na kuchupa mipaka na kuvuruga nidhamu ya jamii. Wanadamu wote humwomba Mwenyezi Mungu awajaalie ukunjufu wa riziki; na inawezekana Yeye Mola kuwatakabalia maombi yao hayo; lakini hikma yake Allah haiendani na kukidhiwa takwa hilo la waja wake. Suala la ugawaji riziki linafanyika kulingana na mahesabu makini ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyakadiria kuhusiana na waja wake, kwa sababu Yeye ni Mjuzi na Mwenye kuwaona wao katika hali zao zote. Yeye Mola anaujua fika uwezo wa kila mtu; na kwa hiyo anaigawa riziki baina ya waja wake kwa kipimo na hisabu kamili na kwa kutilia maanani maslaha. Tajiriba ya historia inaonyesha kuwa, watu wanaojaaliwa ukunjufu wa riziki na uneemevu mkubwa katika maisha, wengi wao humsahau Mwenyezi Mungu, wakawa waasi, wafanya dhulma na wachupa mipaka. Sababu ni kuwa uchu na hamu ya mwanadamu huwa haikomi; na kwa kawaida, mtu huwa hakinai wala hatosheki na kiwango maalumu cha mali na mamlaka. Hutaka apate na walivyo navyo wengine hata kama ni kwa njia ya dhulma na uonevu. Ni kwa sababu hiyo, Allah anawateremshia riziki waja kwa kiwango atakacho Yeye na kwa namna aonayo kuwa ina maslaha. Kwa hivyo wajibu wetu sisi wanadamu ni kufanya juhudi za kuhangaikia riziki na kutafuta ukunjufu wa maisha kwa kiwango kinachoendana na hali ya maumbile. Lakini wakati huohuo tujue kwamba, mfumo wa uumbaji na hikma ya Mwenyezi Mungu havifuati matashi yetu sisi; na riziki itakayotushukia ni ya kiwango ambacho hakitavuruga mfumo wa uumbaji. Ama kuhusu dhiki na uhaba wa riziki, hilo linatokana zaidi na uvivu na ugoigoi wa watu wenyewe. Uhaba na ukosefu huo wa riziki si takwa hasa la Mwenyezi Mungu, bali na matokeo ya matendo ya wanadamu wenyewe, ukiwemo pia uonevu na utovu wa uadilifu unaofanywa na wenye nacho dhidi ya wasio nacho. Kwa hivyo kama tutaacha kujituma na kukaa tu kusubiri ili tushukiwe na riziki, hatutateremkiwa na chochote, kwa sababu Mwenyezi Mungu hajaahidi kuwashushia riziki watu wanaokaa wakajipweteka tu bila kufanya kazi. Kuhusu kuthibitisha kwamba riziki za wanadamu ziko mikononi mwa Allah, mojawapo ya hoja za wazi za kuthibitisha hilo ni unyeshaji wa mvua, ambao mwanadamu hauchangii kwa namna yoyote ile. Kunyesha mvua ni moja ya ishara za ujuzi na uwezo wa Allah SWT. Ikiwa mvua haitanyesha, ukame na njaa vitatawala; na pale inaponyesha, huleta ustawi wa riziki na ukithirifu wa neema kwa watu. Wakati Mwenyezi Mungu anapoteremsha mvua hueneza rehma zake kwa kila kitu. Kutokana na mvua, ardhi mfu na yabisi huhuika ikawa na rutuba, mimea huchipua, maua yakachanua, miti ikastawi na wanadamu pamoja na viumbe wengine wakapata maji ya kunywa na ya mahitaji yao mengineyo. Yote hayo yanaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu anawashugulikia waja na viumbe wake mithili ya familia moja kubwa; na wao waja wanamhimidi na kumshukuru Yeye Mola na Muumba wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kujibiwa na kutakabaliwa maombi ya waja kunaendana na hikma ya Allah. Sababu ni kuwa, kukubaliwa baadhi ya ayatakayo mwanadamu kutamfanya aasi na kuchupa mipaka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mfumo wa uumbaji unafuata hisabu na vipimo maalum, na kila kitu kimewekwa kwa makadirio yake. Aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, mvua ni mfano mmojawapo wa rehma kubwa za Mwenyezi Mungu. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa Allah SWT ndilo kimbilio pekee la mwanadamu wakati wa matatizo na pale anapovunjika moyo na kukata tamaa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 890 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa washukurivu wa neema zake, kubwa na ndogo, tuzijuazo na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/