Sura ya Ash-Shuura, aya ya 36-39 (Darsa ya 892)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 892 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 36 ya sura hiyo ambayo inasema:
فَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَمَا عِندَ اللَّهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ
Basi chochote mlicho pewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu kwa ajili ya walio amini, na wakawa wanamtegemea Mola wao Mlezi,
Katika darsa kadhaa zilizopita tulizungumzia neema za Allah SWT kuanzia nchi kavu hadi baharini. Aya hii ya 36 inasema: vitu vyote ambavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa waja wake hapa duniani ni neema za kupita na zinazomalizika, kwa hivyo msidhani kwamba zitabakia kwenye mamlaka yenu daima dawamu. Lakini neema za ulimwengu wa akhera ni za kuendelea na za milele na wataneemeshwa kwazo waumini kutokana na amali njema na za kheri walizofanya. Kwa hivyo atakayefadhalisha kupata rasilimali na neema hizo za milele za akhera badala ya starehe za kupita za maisha mafupi ya dunia, huyo atakuwa amefanya muamala na biashara yenye faida kubwa mno. Neema za hapa duniani wanajaaliwa watu wote, na wala Allah SWT hatafautishi baina muumini na kafiri; lakini neema za akhera ni makhsusi kwa waja safi na waumini, ambao wamezitumia neema za duniani kwa njia sahihi ili kuijenga na kuistawisha akhera yao pia. Ni wazi kwamba ili kuyashika barabara mafundisho ya dini, muumini huyaepuka mambo maovu na pia hulazimika kujikhini baadhi ya mambo, lakini Allah SWT atakwenda kumfidia yote hayo huko akhera na kumneemesha kwa neema bora zaidi na fadhila kubwa na nyingi za milele. Kinyume na watu waliokumbatia dunia wenye ubakhili na uchu wa kujilimbikizia mali, waumini hutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu; na badala ya kujikusanyia mali tu huwa wanafikiria zaidi kutoa na kuwasaidia wahitaji. Na badala ya kutegemea mali na mamlaka waliyonayo ambavyo wanaamini ni vitu vya kupita na kumalizika, wanatawakali na kutegemea rehma na uwezo wa Allah SWT ambavyo wanajua kuwa vinabakia milele. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mtu muumini hujinufaisha na neema za dunia, lakini lengo lake hasa ni akhera; na kwa mtazamo huo, huyafanya mambo hayo ya kupita na yanayomalizika yawe na athari za kudumu kwake huko anakoelekea. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kwa yale anayoyakosa muumini hapa duniani atafidiwa kwa yaliyo bora zaidi na Allah Siku ya Kiyama. Malipo ya akhera ni makhsusi kwa waumini waliotawakali kwa Mola wao. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, kutawakali kwa Allah badala ya kutegemea mali na madaraka ni alama ya mtu muumini. Kutawakali ni sifa ya kudumu ya waumini.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 37 ambayo inasema:
وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُونَ
Na wanao yaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, na wanapo kasirika wao husamehe,
Aya hii inaendeleza yale yaliyoelezwa katika aya iliyotangulia kuhusu sifa maalumu za waumini kwa kuashiria sifa nyingine mbili muhimu za tabia na akhlaqi za watu hao kwa kusema: watu watakaolipwa thawabu na malipo mema akhera ni wale wanaojiepusha na madhambi na maovu na kuzitakasa nafsi zao na machafu, kwa sababu imani na mambo machafu haviendani pamoja. Waumini ni watu wanaodhibiti nafsi zao. Wanapopandwa na ghadhabu wakakasirika, ambayo ni hali mbaya zaidi inayompata mtu, hudhibiti mikono na ndimi zao, wakajizuia kutenda uovu au kutamka maneno machafu. Hasira kwa hakika ni moto uunguzao, unaofukuta na kuwaka ndani ya nafsi ya mtu; na kuna watu wengi sana ambao wanapoghadhibika hushindwa kuzidhibiti nafsi zao. Bila shaka hasira ni jambo la kimaumbile kwa mwanadamu linaloweza kumtokea mtu yeyote yule; lakini la muhimu ni uwezo wa mtu kuidhibiti nafsi yake wakati anapokasirika. Imani, ina uwezo wa kumjenga mtu kuwa na moyo wa huruma na usamehevu, ili pale anapokosewa, akawa mwepesi wa kusamehe na kufumbia macho mabaya aliyotendewa. Na ndio maana waumini wa kweli wanapokasirika huweza kudhibiti nafsi zao na kujizuia kufanya vitendo viovu na vya kuaibisha. Hupoza moto wa hasira zao kwa kuyatumia maji ya usamehevu kuzitaksa nyoyo zao na vinyongo, na kuwasamehe waliowakosea. Imepokewa katika Hadithi kwamba, mfahamu rafiki yako wakati anapoghadhibika, uone kama je, anaweza kuidhibiti nafsi yake au la? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, imani si suala la moyoni tu, bali inapasa ijidhihirishe pia katika maneno na mwenendo wa mtu. Kujiepusha na madhambi na kudhibiti ghadhabu na matamanio ni miongoni mwa alama za imani ya kweli. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa, muumini huwa anadhibiti hawaa na matamanio ya nafsi yake; na si yeye kutiwa shemere akaburuzwa na matamanio hayo. Halikadhalika aya hii inatutaka tuelewe kwamba, kuwa msamehevu kwa wanaokukosea ni moja ya masharti ya imani. Mtu asiye tayari kuwasamehe wenzake si muumini wa kweli.
Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 38 na 39 ambazo zinasema:
وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ
Na wanao mwitikia Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na mambo yao yakawa ni kwa kushauriana baina yao, na wanatoa katika tuliyowaruzuku,
وَالَّذِينَ إِذَا أَصَابَهُمُ الْبَغْيُ هُمْ يَنتَصِرُونَ
Na ambao wanapo fanyiwa jeuri hujitetea.
Aya hizi zinaendelea kuzungumzia maudhui ya zilizotangulia kuhusu alama za waumini kwa kueleza kwamba, wao ni watu wanaoitikia mwito wa Muumba wao wa kuishika njia iliyonyooka ya uongofu, wanajisalimisha na kutii kikamilifu amri za Mola wao na wanasimama kusali na kumwabudu Yeye peke yake. Lakini mbali na hayo, wanawajali wanyonge na wahitaji; na wanatoa kuwasaidia sehemu ya mali waliyoruzukiwa na Allah. Katika masuala ya kifamilia na kijamii pia, wanaheshimu rai na mawazo ya wenzao na wanashauriana nao katika ufanyaji mambo yao. Historia na taarikh ya Uislamu inaonyesha kuwa, Bwana Mtume Muhammad SAW na masahaba zake walikuwa na tabia na mwenendo huu mwema. Kwani hata yeye Bwana Mtume, aliyekuwa akiteremshiwa wahyi, alikuwa akishauriana na watu katika masuala ya kijamii; na kama waliowengi walikuwa na maoni fulani, aliyaheshimu maoni yao, hata kama yalitafautiana na yake. Mfano wake ni kilichotokea katika Vita vya Uhud, ambapo Bwana Mtume SAW alifuata maoni ya waliowengi kuhusu namna ya kupambana na washirikina wa Kikureishi katika vita hivyo, japokuwa hatima yake ilikuwa ni kushindwa Waislamu na kuuawa zaidi ya masahaba zake 70. Bila ya shaka na ifahamike vyema kwamba, mashauriano hayo aliyokuwa akifanya Bwana Mtume SAW na watu, yalihusu masuala ya kifamilia, kijamii, kiuchumi, namna ya uendeshaji wa jamii na mengineyo, si kuhusiana na hukumu za Mwenyezi Mungu. Na ndiyo maana aya inaeleza wazi kwamba, waumini wanashauriana katika mambo yao, na si katika jambo ambalo hukumu yake wameshabainishiwa tokea hapo kabla na Mola wao. Na nukta yenye kutoa mguso maalumu hapa ni kwamba, kati ya sifa zote za waumini zilizotajwa ndani ya sura hii, sifa ya kushauriana imepewa umuhimu mpaka jina la sura hii likatokana na sifa hiyo. Sifa ya mwisho ya waumini iliyotajwa katika aya hizi tulizosoma, ni muqawama na kuwa imara katika kukabiliana na dhulma na madhalimu. Mtu muumini haridhii kufanyiwa dhulma na huomba msaada kwa wenzake ili kupambana na madhalimu na kuondoa dhulma na shari yao. Ni kama inavyoelezwa katika aya nyingine ya Qur’ani ya kwamba: muumini huwa hadhulumu wala hakubali kudhulumiwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Uislamu ni dini iliyokamilika inayojumuisha mambo yote; na inazingatia na kushughulikia pande tofauti za maisha ya mwanadamu zikiwemo za kiuchumi, kiakhlaqi, kijamii, kiibada na kisiasa. Baadhi ya mifano yake ni ile iliyoashiriwa ndani ya aya hizi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kudai mtu ameamini, lazima kuthibitishwe kwa amali na matendo. Muumini anatakiwa awe na tabia njema na sahihi inayomridhisha Allah katika hali zake zote za binafsi na za kijamii; na si kuwa mtu wa Sala na ibada za kiroho tu, lakini akaghafilika na kupuuza masuala ya kijamii. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, udikteta katika maamuzi hauendani na sifa ya uumini. Kwa sababu mtu muumini huwa anajali na kuheshimu rai na maoni ya wenzake. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, kukubali kudhulumiwa na kukaa kimya mbele ya dhulma kunakinzana na kumwamini Allah. Kwa hiyo inampasa mtu muumini asimame kukabiliana na dhalimu na kutetea haki yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 892 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waumini wa kweli wanaoshauriana katika mambo yao na wanaotekeleza mafundisho ya dini yake tukufu katika kila nyanja ya maisha yao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/