May 24, 2023 10:23 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 893 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 40 ya sura hiyo ambayo inasema:

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا ۖ فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ

Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe, na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.

Katika aya ya mwisho tuliyosoma kwenye darsa iliyopita lilizungumziwa suala la kujihami na kukabiliana na dhalimu, kwa maana kwamba, mtu muumini hawezi kuinyamazia kimya dhulma; na ikiwa italazimu, ataomba msaada pia kwa wenzake ili kumdhibiti mtu dhalimu. Katika mwendelezo wa maudhui hiyo, aya tuliyosoma inasema: pamoja na hayo, katika kumchukulia hatua anayedhulumu, kusiwepo na uchupaji mipaka, bali aadhibiwe kwa haki na uadilifu na kulingana na dhulma aliyofanya, kama inavyosisitiza pia aya ya 194 ya Suratul Baqarah juu ya msingi wa mtu kulipiza kisasi sawa na alivyotendewa. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba, ikiwa mtu dhalimu atajuta kwa aliyoyafanya na akaomba msamaha, basi msameheni na pataneni naye kwa kufanya naye suluhu, kwani Mwenyezi Mungu analipenda zaidi hilo, na atakulipeni thawabu kwa sababu ya kusamehe. Hapana shaka kuwa, amri hii ya Allah SWT haimaanishi kumtetea na kumuunga mkono dhalimu, bali inalenga kuondoa uadui na vinyongo baina ya watu katika jamii na kuleta suluhu na maridhiano kati yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mtu aliyedhulumiwa ndiye mwenye hiari na mamlaka ya kumpa adhabu aliyemdhulumu. Anaweza hata kumsamehe au kumwadhibu kwa msingi wa uadlifu. Kwa hivyo kama ataamua kutomsamehe, adhabu atakayompa ilingane na aina ya dhulma aliyomtendea na wala isichupe na kupindukia mpaka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, linalousiwa zaidi na dini ni kumsamehe aliyekukosea, hata kama utakuwa na uwezo wa kumwadhibu. Na hapana shaka kuwa, mtu anayesamehe atapata kwa Mwenyezi Mungu malipo makubwa ya thawabu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, sambamba na kutakiwa sheria zitawale na kutekelezwa kwa uadilifu, inapasa watu washajiishane pia kuamiliana kiakhlaqi, kwa huruma na upendo. Ni kama inavyousia Qur’ani tukufu juu ya kusamehe, sambamba na kuwepo haki ya ulipizaji kisasi.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 41 na 42 ambazo zinasema:

وَلَمَنِ انتَصَرَ بَعْدَ ظُلْمِهِ فَأُولَٰئِكَ مَا عَلَيْهِم مِّن سَبِيلٍ

Na wanao jitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu.

إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۚ أُولَٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

Bali lawama ipo tu kwa wale wanao wadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumzwa katika aya iliyotangulia kuhusu kuchukua hatua ya kumwadhibu au kumsamehe aliyetenda dhulma na kusisitizia tena kwa mara nyingine nukta ya kwamba, msamaha huo inatakiwa utolewe na mdhulumiwa na kwa hiari yake mwenyewe; na si kwa kulazimishwa na watu. Sababu ni kwamba, yeye anayo haki isiyo na shaka ya kumpa adhabu ya kumlipizia kisasi aliyemdhulumu; na hata kama hatokuwa na uwezo wa kulifanya hilo peke yake, basi aombe msaada kwa watu wengine. Na kwa mintaarifu ya hayo, haifai kumlaumu mtu aliyedhulumiwa pale anapopigania kupata haki yake, kwa sababu si kosa hata kidogo kufanya hivyo. Inavyotakiwa hasa ni jamii kuwalaumu na kuwashutumu watu wanaowanyang’anya na kuwadhulumu wenzao haki zao; ni wale wanaozikanyaga sheria, wakavuka na kuchupa mpaka kwa kujiona bila ya haki kwamba wao ni wabora na wana hadhi na daraja ya juu kuliko wenzao. Watu hao wanastahiki kukemewa na kulaumiwa hapa duniani; na huko akhera wataghadhibikiwa na Allah na kupatwa na adhabu kali ya Moto. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, madhulumiwa ana haki ya kuomba msaada kwa watu; na watu wa jamii yake inapasa wamsaidie ili pate haki yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, uvukaji mipaka wa kudhulumu haki za watu ni uovu usiokubalika, hata ukifanywa na mtu yeyote yule, na inapasa ufuatiliwe na kuchukuliwa hatua za kisheria. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, uovu wa uchupaji mipaka ya sheria za Mwenyezi Mungu na kanuni za kijamii, ambao unasababisha ufisadi na uharibifu katika jamii inapasa ufichuliwe; na wale waliohusika wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua na wanajamii.

Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 43 ambayo inasema:

وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ

Na anaye subiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.

Aya hii inarudia kwa mara nyingine tena suala la kumsamehe aliyekosea na kusisitiza kwamba, haki aliyonayo mdhulumiwa ya kumlipizia kisasi aliyemdhulumu isiwafanye watu wakaghafilika na sifa ya usamehevu na wakalipuuza jambo jema la kurehemeana na kuhurumiana. Na kwa muktadha huo inasema: Kuwasamehe waliotukosea ni jambo gumu linalohitaji subira na uvumilivu; lakini ni jambo lenye thamani kubwa sana. Ni wazi kwamba, kuidhibiti nafsi na hisia za uchungu na kuwa tayari kuisamehe haki si jambo jepesi hata kidogo au linaloweza kufanywa na kila mtu. Lakini watu waungwana, wenye azma na irada thabiti na moyo uliopambika kwa sifa njema, wao huweza kulifanya hilo, wakasemehe na kufumbia macho haki yao. Kwa ujumla aya hizi kadhaa za Suratu-Shuraa zimezungumzia aina mbili za kuamiliana na mtu aliyewafanyia dhulma wenzake: ya kwanza ni kumwadhibu na kumlipizia kisasi na ya pili ni kumhurumia na kumsamehe. Ni wazi kwamba, mazingira na hali za watu pia zinaathiri na kuchangia katika suala hili; yaani mazingira na hali ya aliyedhulumu; na pia ya aliyedhulumiwa. Kwa maana kwamba, yamkini aliyedhulumu, yeye mwenyewe akajuta kwa aliyotenda, akaomba asamehewe. Na yamkini pia asijute kwa uovu aliofanya na akaendelea kujigamba na kujisifu na hata kutetea dhulma aliyofanya. Na kwa upande wa aliyedhulumiwa pia, inawezekana akawa ni mtu muungwana na mwenye moyo rahimu kiasi cha kuwa tayari kirahisi kuwasamehe waliomkosea. Lakini wakati mwingine mdhulumiwa huwa katika hali na mazingira yanayomfanya asiweze kuvumilia dhulma na uovu aliotendewa na hivyo akashikilia msimamo wa kutaka haki itendeke. Katika aya hizi kadhaa na zilizopita tulizosoma, zimechambuliwa na kuzungumziwa hali zote hizo na kubainishwa hukumu ya kufuatwa kulingana na hali na mazingira yalivyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, wasia wa kiakhlaqi wa Qur’ani ni mtu kuvumilia na kuwasamehe wenzake kwa waliyomkosea; ijapokuwa kwa mujibu wa sharia, haki yake ya kulipa kisasi na kuadhibiwa aliyemkosea iko pale pale. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, subira na usamehevu ni miongoni mwa sifa tukufu za kiutu yenye hadhi kubwa mbele ya Allah SWT. Vile vile aya hii inatutaka tujue kwamba Uislamu ni dini iliyokamilisha kila kitu, kwa maana ya kuitambua haki ya mdhulumiwa, lakini wakati huohuo kumshajiisha aonyeshe uungwana wa kusamehe na kufumbia macho haki yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 893 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na ubaya wa kudhulumu haki za watu, na atuwezeshe kuwa wavumilivu na wasamehevu pia kwa wanaotukosea. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/