May 24, 2023 16:08 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 912 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 44 ya ad-Dukhan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 28 na 29 za sura hiyo ambazo zinasema:

كَذَٰلِكَ ۖ وَأَوْرَثْنَاهَا قَوْمًا آخَرِينَ

Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wengine. 

فَمَا بَكَتْ عَلَيْهِمُ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ وَمَا كَانُوا مُنظَرِينَ

Mbingu wala ardhi hazikuwalilia; wala hawakupewa muda.

Katika kuhitimisha simulizi za hatima iliyoipata kaumu ya Firauni, aya tulizosoma zinasema: baada ya Firauni na watu wake kuangamizwa kwa kugharikishwa kwenye Mto Nile, kila walichoacha kilirithiwa na Bani Israil; wakazimiliki mali na utajiri wao wote bila kuuhangaikia wala kuupatia usumbufu wowote. Ni kama ilivyoelezwa pia katika Suratu-Shuaraa ya kwamba, baada ya kugharikishwa kina Firauni na kuporomoka mihimili ya utawala wao, kundi moja la Bani Israil lilirudi tena Misri na kutawala katika ardhi hiyo ya Mafirauni. Kisha aya zinaendelea kubainisha kwamba, kutokana na ukubwa wa dhulma ilizofanya kaumu ya Firauni, wakati walipoangamizwa na kuondolewa katika mgongo huu wa ardhi, hakuna yeyote aliyeguswa na kuondoka kwao au hata kutokwa na chozi. Hata mbingu na ardhi pia zilifarijika kwa kuangamizwa kwao wala hazikuhuzunika au kuwasikitikia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuangamizwa kaumu za madhalimu ni moja ya utaratibu aliouweka Allah ili uwe onyo na mazingatio kwa watu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ulimwengu wa maumbile unayo aina fulani ya hisi na utambuzi. Kwa hivyo si wanadamu peke yao, bali hata ulimwengu huo pia hupata hisia nzuri kwa kuangamizwa madhalimu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 30 hadi 33 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ نَجَّيْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنَ الْعَذَابِ الْمُهِينِ

Na hakika tuliwaokoa Wana wa Israili na adhabu ya kuwadhalilisha,

مِن فِرْعَوْنَ ۚ إِنَّهُ كَانَ عَالِيًا مِّنَ الْمُسْرِفِينَ 

Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka.

وَلَقَدِ اخْتَرْنَاهُمْ عَلَىٰ عِلْمٍ عَلَى الْعَالَمِينَ

Na hakika tuliwachagua kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wengine. 

وَآتَيْنَاهُم مِّنَ الْآيَاتِ مَا فِيهِ بَلَاءٌ مُّبِينٌ

Na tukawapa katika ishara (zetu) ambazo ndani yake mna majaribu yaliyo wazi.

Nabii Musa (as) alisimama kukabiliana na Firauni aliyekuwa akitakabari. Kwa hakika Firauni alikuwa mtawala dhalimu na mwagaji damu, ambaye alijihisi bora kuliko wanadamu wengine na aliwazidi watu wote kwa israfu na ufisadi. Mafirauni walikuwa wakiwaadhibu Bani Israil na kuwapa mateso yasiyohimilika. Wakiwachinja watoto wao wachanga wa kiume na kuwaacha hai wa kike ili waje kuwatumikisha na kuwafanya wajakazi wao. Waliwatumikisha na kuwafanyisha kazi ngumu na za sulubu Bani Israil bila kuwapa chochote. Lakini hatimaye Mwenyezi Mungu Mtukufu aliikomboa kaumu hiyo iliyokuwa ikidhulumiwa ya Bani Israil na kuitoa kwenye makucha ya Firauni jabari na mwagaji damu kwa mapambano yaliyoendeshwa na kuongozwa na Nabii Musa (as). Na kama tulivyotangulia kueleza, si tu Bani Israil walikomboka kutokana na madhila waliyokuwa wakiyapata kwa Mafirauni, lakini pia walihodhi mali na milki zao zote; na wao wenyewe wakawa kaumu yenye nguvu na uwezo iliyoishi kwenye ardhi kubwa. Lakini mbali na mali na milki, Mwenyezi Mungu SWT aliwatunuku pia neema zingine, ambazo ziligeuka mtihani kwao wa kujaribiwa. Ni kuteremshwa vyakula maalumu vya mbinguni kama Manna na Salwa, ambavyo vimeashiriwa katika Suratul-Baqarah, au kupasuka jiwe gumu na kutiririka ndani yake chemchemi kumi na mbili za maji kwa ajili ya matumbo yote kumi na mbili ya Bani Israil. Yote hayo yalifanywa ili yawe mtihani kwao. Kwani hiyo ndio kaida na utaratibu wa Allah. Hulitahini kundi moja kwa misiba na mabalaa; na hulijaribu kundi jengine kwa fadhila na neema zake. Ilivyo hasa katika mantiki ya Qur’ani, misiba na tabu ni wenzo wa kujaribiwa mtu, kama ulivyo utajiri, mali na madaraka. Kwa hivyo wakati Bani Israil walipokuwa wakiteswa na kuadhibiwa na Firauni walikuwa wakijaribiwa, na vivyohivyo walipowezeshwa kuhodhi mali na madaraka na kuwa na mamlaka ya kila kitu. Hata hivyo hawakujali wala kushukuru neema hizo, wakafeli mtihani huo waliopewa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, watu wanaomsaidia Mtume wa Mwenyezi Mungu na kufuata mafundisho yake, wanaweza kuokolewa na madhila ya madhalimu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kujifanya bora, kufurutu ada na kupindukia mipaka ni hulka ya kifirauni, hata kama mwenye shakhsia iliyojengeka kutokana na hulka hiyo hatokuwa Firauni mwenyewe. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, sifa chafu na matendo maovu ndio chanzo cha kuangamizwa umati na kaumu mbalimbali. Aidha, aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, neema ambazo Allah anawapa watu na jamii mbalimbali ni wenzo wa kuwatahini tu; na si hoja ya kudhani kwamba wao ni bora kwake Yeye Mola.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 34 hadi 36 za sura yetu hii ya Ad-Dukhan ambazo zinasema:

إِنَّ هَٰؤُلَاءِ لَيَقُولُونَ

Hakika hawa wanasema:

إِنْ هِيَ إِلَّا مَوْتَتُنَا الْأُولَىٰ وَمَا نَحْنُ بِمُنشَرِينَ

Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi.

فَأْتُوا بِآبَائِنَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

 

Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.

Baada ya kumalizika kisa cha kina firauni na Bani Israil, aya hizi zinazungumzia kwa mara nyingine tena habari za washirikina wa Makka na kauli zao za kukanusha maadi pale waliposema: mwisho wa maisha ni haya mauti mnayoyaona; na hakuna chochote chengine baada ya hapo, seuze mtu kudai kwamba tutakuwa hai tena na kuwa na maisha mengine mapya. Makafiri hao walikuwa wameing’ang’ania itikadi hiyo mpaka wakawa wanamwendea Bwana Mtume SAW na kumwambia: kama usemayo ni kweli, kwamba wafu watakuwa hai tena, wafufue basi baba zetu waliokufa miaka na miaka iliyopita ili tuwaone hapahapa duniani ndipo tutaamini. Ni wazi kuwa maadi, yaani kufufuliwa viumbe, yamewekwa kwa ajili ya kwenda kuwalipa watu malipo ya thawabu au adhabu huko akhera; na utaratibu alioupanga Allah SWT si kuwafufua wafu hapa duniani. Lakini hata tukijaalia kuwa Mtume angeifanya kazi hiyo ya kuwafufua wafu, lakini kwa watu wakaidi, wabishi na watafutaji visingizio, wangeamua kuzusha hoja nyingine na kusema, wanayoyaona ni uchawi na mazingaombwe na wasingekuwa tayari kuuamini muujiza huo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kubainisha mitazamo ya wapinzani na kuitolea majibu ni mbinu inayotumiwa Qur’ani kuthibitisha ukweli wa imani na itikadi wanazofuata waumini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kukanusha ulimwengu na maisha baada ya kifo, hakufanywi kwa hoja na burhani; ni madai ambayo makafiri wamekuwa wakiyatoa katika zama zote za historia bila ya hoja wala mantiki. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 912 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atusamehe madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/