Sura ya Ad-Dukhan, aya ya 37-50 (Darsa ya 913)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 913 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 44 ya ad-Dukhan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 37 ambayo inasema:
أَهُمْ خَيْرٌ أَمْ قَوْمُ تُبَّعٍ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ أَهْلَكْنَاهُمْ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ
Je! Wao ni bora au watu wa Tubbaa' na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa waovu.
Aya hii inawahutubu washirikina wa Makka waliokuwa wakionyesha ukaidi, jeuri na ukadhibishaji katika kuamiliana na Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: nyinyi mnadhani mna nguvu zaidi kuwashinda watu waliokuwa wakiishi katika ardhi ya Yemen kusini ya Bara Arabu? Wao walikuwa wakimiliki ardhi zenye rutuba na neema nyingi na walikuwa na nguvu na uwezo mkubwa, lakini kutokana na kukitihirisha dhulma, maasi na ufisadi, mwishowe waliangamizwa. Basi tahadharini msije na nyinyi mkafikwa na hatima sawa na iliyowafika majirani zenu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, moja ya nyenzo zinazotumiwa na Qur'ani kwa ajili ya kuwapa watu maonyo na miongozo ni kuwabainishia historia ya kaumu zilizopo ili zitoe ibra na mazingatio kwa wanaokuja baada yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, adhabu za baadhi ya matendo huanza kulipwa papa hapa duniani. Miongoni mwao ni dhulma, maasi na ufisadi vinapokithiri ndani ya jamii.
Ifuatayo sasa ni aya ya 38 na 39 ambazo zinasema:
وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina ya viwili hivyo kwa mchezo.
مَا خَلَقْنَاهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ
Hatukuviumba viwili hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui.
Kwa kuzingatia kuwa katika aya kadhaa zilizotangulia yalizungumziwa Maadi, yaani kufufuliwa kwa viumbe, katika aya tulizosoma, imeashiriwa sababu ya kusimama Kiyama na kuelezwa kwa sura ya kuhoji: hivi mnadhani mbingu na ardhi pamoja na ulimwengu huu wenye adhama vimeumbwa burebure na bila ya lengo lolote, hata vimalizike na kutoweka baada ya kufa viumbe tu? Kama ni hivyo, basi itakuwa sawa na mchezo wa watoto, wanaounganisha vipande tofauti vya kuchezea kutengeneza nyumba, ambayo huibomoa mwisho wa mchezo wao kwa kuiparaganya kwa kidole kimoja tu; kwa sababu hawakuijenga kwa lengo jengine isipokuwa kucheza na kujifurahisha tu. Makafiri na wakanushaji wa maadi, wanayachukulia mauti kuwa ndio nukta ya mwisho ya maisha ya mtu. Kwa maneno mengine ni kwamba, kwa uoni wao, kuumbwa kwa mwanadamu, kisha kutunukiwa uwezo na kila aina ya vipaji na vipawa, kumefanywa kwa ajili ya kupitisha siku chache tu za maisha haya ya dunia, na kwamba kila kitu kinamalizika baada ya kifo. Bila shaka mtu anapokuwa na mtazamo kama huu, uumbaji utakuwa jambo la upuuzi na lisilo na maana. Lakini kinyume na mtazamo huo wa wakanushaji wa maadi, mtazamo wa Qur'ani ni kwamba, mauti ni daraja la kuvuka kutoka ulimwengu huu kuelekea ulimwengu wa milele na wenye adhama kubwa zaidi, kiasi kwamba ulimwengu huu unapolinganishwa na huo huwa ni kitu kidogo mno na kisicho na thamani yoyote. Haiingii akilini hata chembe kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mweza na Mwenye hekima awe ameuumba ulimwengu mkubwa na wenye adhama kama huu bila lengo, bali uwe ni kwa ajili ya kutumiwa siku chache tu za maisha ya mwanadamu. Katika aya hizi imeashiriwa kuumbwa kwa haki mbingu na ardhi. Kuwa haki ulimwengu huu mkubwa kunakufanya kuumbwa kwake kuwe na lengo linaloingia akilini, lengo ambalo halipatikani bila kuwepo ulimwengu mwingine baada ya huu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kama maisha ya mwanadamu yatamalizika kwa kifo, ulimwengu huu wenye adhama, ambao umeumbwa kwa ajili ya kiumbe huyo utakuwa kitu cha upuuzi na kisicho na maana yoyote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ikiwa ulimwengu una lengo maalumu, sisi wanadamu inatupasa tulifahamu kwa usahihi lengo hilo la uumbwaji wake na kwenda sambamba na lengo hilo. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, moja ya sababu za kukanushwa maadi ni kutofahahamika lengo la uumbaji, ambalo watu wengi hawalifahamu kwa usahihi.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 40 hadi 42 ambazo zinasema:
إِنَّ يَوْمَ الْفَصْلِ مِيقَاتُهُمْ أَجْمَعِينَ
Hakika siku ya Upambanuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote.
يَوْمَ لَا يُغْنِي مَوْلًى عَن مَّوْلًى شَيْئًا وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ
Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa.
إِلَّا مَن رَّحِمَ اللَّهُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ
Ila yule ambaye Mwenyezi Mungu atamrehemu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
Katika kuendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu kuwa na lengo mfumo wa ulimwengu, sababu muhimu zaidi ikiwa ni kuthibiti kwa Kiyama, aya hizi zinagusia baadhi ya sifa maalumu za siku hiyo kwa kusema: Hiyo ni siku ya upambanuzi na utengano. Ni siku ambayo mtu atatengana na vitu vyote isipokuwa amali zake tu. Kinyume na duniani, ambako marafiki huweza kusaidiana wakati wa shida ili kuondoleana matatizo waliyonayo, Siku ya Kiyama mahusiano ya kifamilia na kijamii yatakwisha. Si rafiki ambaye ataweza kuitika kilio cha rafiki yake, wala ndugu na jamaa ambao wataweza kusaidiana kwa chochote. Mipango yote ya watu itavurugika na njia zote za utatuzi zitafungika. Ni wazi kuwa hakuna mtu atakayeweza kumuokoa mtu mwingine isipokuwa kwa rehma na ukarimu wa Allah SWT. Yeye Mola Mrehemevu atawarehemu waja wake wema na kuwaneemesha kwa fadhila zake zisizo na ukomo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Kiyama ni siku ya kutengana watu, ambapo mtu ataachana mkono na marafiki, ndugu na jamaa zake wote. Kwa hivyo tusijipe tamaa ya kupata msaada siku hiyo wa yeyote kati ya hao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuhudhurishwa wanadamu Siku ya Kiyama ni jambo lisilo na shaka. Siku hiyo watu wote watakusanywa pamoja, lakini kila mmoja katika mkusanyiko na mjumuiko huo atajihisi yuko peke yake akiwa hana pa kukimbilia. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Siku ya Kiyama hatima za wanadamu zitakuwa kwenye mamlaka ya Mwenyezi Mungu tu. Yeye Mola ataamiliana na makafiri kwa izza na uwezo wake; na ataamiliana na waumini kwa rehma na ukarimu wake.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 43 hado 50 za sura yetu ya Ad-Dukhan ambazo zinasema:
إِنَّ شَجَرَتَ الزَّقُّومِ
Hakika Mti wa Zaqqum,
طَعَامُ الْأَثِيمِ
Ni chakula cha mwenye dhambi.
كَالْمُهْلِ يَغْلِي فِي الْبُطُونِ
Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni
كَغَلْيِ الْحَمِيمِ
Kama mchemko wa maji ya moto.
خُذُوهُ فَاعْتِلُوهُ إِلَىٰ سَوَاءِ الْجَحِيمِ
(Itasemwa:) Mkamateni na mburureni mpaka katikati ya Jahannamu!
ثُمَّ صُبُّوا فَوْقَ رَأْسِهِ مِنْ عَذَابِ الْحَمِيمِ
Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka.
ذُقْ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْكَرِيمُ
Onja! Hakika ulikuwa (ukijidai) kwamba, wewe ndiye mwenye nguvu, mheshimiwa!
إِنَّ هَٰذَا مَا كُنتُم بِهِ تَمْتَرُونَ
Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka.
Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia sifa mojawapo ya Siku ya Kiyama, aya hizi zinatoa taswira ya kutisha ya hali watakayokuwa nayo waovu ndani ya Moto wa Jahannamu, ambayo inaushtusha moyo na kuutetemesha mwili wa mtu kwa hofu. Picha na taswira ya kawaida inayompitikia mtu ni kwamba Moto wa Jahannamu ni kama ulivyo moto wa hapa duniani ambao huunguza na kukifanya kitu kigeuke jivu tu. Hali ya kuwa kwa mujibu wa aya hizi, wakati watu wa motoni wanahiliki kwa adhabu ya moto, watakuwa wanaendelea kuishi, wakila chakula na kunywa maji; lakini ni chakula na maji ambavyo vitawazidishia adhabu, machungu na mateso watu hao. Ni maji yachemkayo na yaunguzayo na chakula kichungu kabisa kiunguzacho, ambavyo havitawazidishia watu wa motoni kitu kingine isipokuwa machungu na mateso na hawatakuwa na pa kukimbilia ili kuyaepuka hayo. Mienge ya moto itakuwa ikiipenya na kuiunguza miili yao kila upande. Lakini mbali na adhabu kali na chungu ya kuhilikisha viwiliwili vyao, kutakuwepo na adhabu nyingine yenye kuumiza mno ya kinafsi. Mtu mwovu na asi ataambiwa: onja haya, wewe ndiye uliyekuwa ukijiona na kujidhani katika nafsi yako kuwa ndiye mheshimiwa zaidi na mwenye nguvu na mamlaka zaidi kuliko mtu yeyote. Ulikuwa ukiwafunga, kuwatesa na kuwaadhibu wanyonge na kuwafanyia kila aina ya dhulma na uonevu, huku ukijihisi ni mwenye nguvu na madaraka yasiyoshindika na uheshimiwa usio na kikomo. Bila shaka kiwango na ukubwa wa adhabu za watu utalingana na kiwango cha maovu na madhambi yao. Wale ambao hapa duniani hawachelei kufanya maovu, jinai na unyama wowote ule kwa kudhani kwamba kutokana na hadhi, madaraka na uwezo walionao hakuna yeyote awezaye kuwadhuru kwa namna yoyote, wao watapata adhabu kali zaidi kuliko watu wengine. Na hayo yatakuwa ni matokeo ya matendo yao ya hapa duniani. Na kwa hiyo wataambiwa: Hayo unayoyashuhudia ndiyo yale uliyokuwa kila mara ukiyadharau na kuyatilia shaka. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Siku ya Kiyama, madhambi yatadhihiri katika sura ya moto, utakaotanda nje na ndani ya mwili wa mtu ukimuunguza na kumhilikisha. Kwa hiyo maadamu tungaliko hapa duniani tuziokoe nafsi zetu na adhabu ya Moto huo kwa kuyaacha madhambi na kuomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, adhabu ya Siku ya Kiyama itakuwa ya kimwili na kiroho. Watu wa motoni wataungua na kuteketea kwa Moto na pia watadunishwa na kudhalilishwa. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 913 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya Moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../