May 24, 2023 13:54 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 918 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 45 ya Al-Jaathiya. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 21 na 22 za sura hiyo ambazo zinasema:

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ

Je! Wanadhani wanao tenda maovu kuwa tutawafanya kama walio amini na wakatenda mema, sawa sawa maisha yao na mauti yao? Ni hukumu mbaya wanayo ihukumu!

وَخَلَقَ اللَّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَلِتُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ

Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na ili kila nafsi ilipwe yale iliyo yachuma. Nao hawatadhulumiwa.

Katika darsa zilizopita tulisoma aya zilizozungumzia hatima ya waumini na makafiri Siku ya Kiyama. Aya hizi zinaashiria kwa kuhoji dhana ya kuyalinganisha makundi hayo mawili kwa kusema: hivi kuna mtu anayetarajia kwamba Mwenyezi Mungu SWT aliye mwadilifu, ataamiliana kwa namna moja na watu wema na wabaya? Je, nyinyi wenyewe mnakubali kuwa hapa duniani, ambako kila mtu anafanya lolote atakalo, wale wanaojitolea kuhudumia jamii na wale wanaowaonea na kuwadhulumu watu, wote hao waangaliwe kwa jicho moja? Kama kuna mtu anadhani kwamba imani na amali njema au ukafiri na madhambi havina taathira yoyote katika maisha ya mtu, dhana na imani hiyo si sahihi. Hapana shaka yoyote kuwa maisha na mauti ya muumini na kafiri yako tofauti. Waumini hupata utulivu maalumu kutokana na athari ya imani na amali zao njema, kiasi kwamba masaibu na misukosuko mikubwa ya maisha inayowapata huwa na taathira hasi ndogo zaidi kwa roho na nafsi zao. Watu waumini hufarajiwa na ahadi za Mwenyezi Mungu na huuangalia mustakabali wao kwa jicho la matumaini na matarajio mema. Ni kama isemavyo aya aya 82 ya Suratul-an Aam ya kwamba: "Wale ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao na dhulma - hao ndio watakao pata amani na wao ndio walio ongoka". Lakini kinyume na watu hao, wale wasiomwamini Allah na wakawa wametopea kwenye maovu na maasi, wao huwa daima wanatawaliwa na wahka na wasiwasi. Hata kama watakuwa wamezungukwa na chungu ya neema za vitu vya kidunia, hofu ya kuwatoka vitu hivyo huwasononesha na kuwanyima raha; na wanapouangalia mustakabali, huuhisi ni kiza kitupu; na mauti kwao wao ni kutoweka na kumalizika. Nuru ya uongofu, huzipa mwangaza nyoyo za watu wa kundi la kwanza na kuwafanya wayafuatilie kwa moyo mkunjufu malengo mema na yenye thamani wanayotaka kuyafikia. Lakini kundi la pili ni la watu wasio na lengo maalumu na linalofahamika kwa ajili ya maisha; hubaki wanamangamanga na kuselelea kwenye mawimbi na dhoruba za viza. Kwa hivyo wakati makundi mawili hayo yanapofikwa na mauti, ambayo ni njia ya kupita kuelekea kwenye ulimwengu wa milele, hatima na majaaliwa yao, yatakuwa tofauti pia. Wakati watu waumini na waliotenda mema wanapofikwa na mauti, hubashiriwa Pepo. Lakini wale waovu waliomkufuru Mwenyezi Mungu, huambiwa piteni kwenye milango ya kuingilia Jahannamu na mtabaki humo milele. Kwa hivyo kwa ufupi ni kwamba, hali za makundi haya mawili katika kila jambo ukiwemo uhai na mauti, Barzakhi na Kiyama ni tofauti kabisa. Nukta nyingine ni kwamba, uumbwaji wa mbingu na ardhi umefanywa kwa msingi wa haki na uadilifu. Si mfumo wa maisha ya wanadamu pekee, bali mfumo wa viumbe vyote katika ulimwengu wa maumbile umeratibiwa kwa msingi wa haki. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu si mwenye kumdhulumu mtu yeyote na pia hakuwaumba wanadamu na kisha kuwaacha vivi hivi ili kila mtu afanye chochote atakacho na vyovyote apendavyo. Bali atawalipa watu adhabu au thawabu kulingana na mfumo wa uadilifu aliouweka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tujiepushe na kumdhania Mwenyezi Mungu mambo yasiyo sahihi na tujue kwamba kipimo kitakachotumiwa kulipwa thawabu au adhabu ni amali zetu tulizofanya, si dhana hewa na matarajio yasiyo na maana tuliyonayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, imani na amali njema na vilevile kukufuru na kufanya maovu vina mchango na taathira katika uhai, kifo na hatima ya mtu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mfumo wa ulimwengu wa uumbwaji umesimamishwa juu ya msingi wa haki. Kwa hivyo unaamiliana na mtu pia kwa msingi wa haki. Vilevile aya hizi zinatutaka tufahamu kuwa, falsafa ya kuwepo Kiyama ni hekima na uadilifu wa Allah SWT ili liweze kuthibiti lengo la uumbaji; na haki imfikie yule anayestahiki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 23 ya sura yetu ya Al Jaathiya ambayo inasema:

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَن يَهْدِيهِ مِن بَعْدِ اللَّهِ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

Je! Umemwona aliye fanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake, na Mwenyezi Mungu akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akambandika vitanga machoni mwake? Basi nani atamwongoa huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Basi je hamkumbuki?

Aya hii inaashiria chimbuko la ufanyaji maasi na madhambi na kueleza kwamba: wafanya madhambi na maasi huwa wanayachukulia matakwa na matamanio ya nafsi zao kipimo cha kufanyia kila jambo, kiasi kwamba huzifanya hawaa na matamanio hayo ya nafsi kuwa ndio mungu wao anayewaamuru wafanye mambo yatakayowastarehesha na kuwapa raha zaidi. Wao hufanya chochote zinachokitamani nyoyo zao na hata huzitumia akili na fikra zao kwa ajili ya kuyafikia matashi ya nyoyo zao. Ni kawaida kwa watu kama hao kuingiwa na upofu na uziwi wa kushindwa kuiona na kuisikia haki, na badala yake kuyaona sahihi na ya sawa yale tu yanayokidhi raha zao na yenye manufaa na wao; na kila kilicho kinyume na hayo hukichukulia kuwa si sahihi. Mtazamo kama huu humfanya mtu afikie hatua ya kupoteza hata ufahamu, ujuzi na uelewa wake wa mambo. Kwa hivyo watu wanaoabudu hawaa na matamanio ya nafsi, hata kama watakuwa wajuzi, wataalamu na wanazuoni huishia kwenye dhalala, upotofu na hilaki. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hii ni kwamba, si masanamu ya miti na mawe tu au mwezi na jua na baadhi ya wanyama, ndio pekee waliogeuzwa kuwa miungu ya kuabudiwa na watu katika zama zote za historia. Kuna watu wengine wanaoabudu hawaa na matamanio ya nafsi zao kwa kufanya yale tu yanayozipendeza na kuzistarehesha nyoyo zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, ikiwa mtu atatawaliwa na matamanio ya nafsi yake elimu, ujuzi na uelewa alionao juu ya mambo hauwi na faida wala haufanyi kazi tena. Ni sawa kabisa na daktari ajuaye kila kitu kuhusu madhara ya sigara, lakini yeye mwenyewe akawa ni mvutaji mkubwa! Halikadhalika aya hii inatutaka tujue kwamba, hawaa na matamanio ya nafsi ni mithili ya miwani yenye vioo vya rangi ambavyo humfanya mtu ashindwe kukiona kitu vile hasa kilivyo na kuweza kuchukua uamuzi sahihi. Kwa hiyo kwa kuabudu matamanio ya nafsi mtu huishia kupotea njia.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 24 na 25 ambazo zinasema:

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ ۚ وَمَا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ

Na walisema: Hapana ila huu uhai wetu wa duniani – tunakufa na tunaishi, na hapana kinacho tuhilikisha isipo kuwa (huu huu) ulimwengu. Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu. 

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ مَّا كَانَ حُجَّتَهُمْ إِلَّا أَن قَالُوا ائْتُوا بِآبَائِنَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wakweli. 

Aya iliyopita ilizungumzia kuabudu matamanio ya nafsi na jinsi kunavyomweka mtu mbali na ufahamu wa haki na ukweli. Aya hizi tulizosoma zinaashiria moja ya matokeo mabaya ya kuabudu hawaa za nafsi na kueleza kwamba, wale wanaofikiria raha na starehe za ghariza tu na kutosheka na kukidhi matamanio ya nafsi zao, huwa wanakanusha kuwepo kwa ulimwengu wa baada ya kifo na Kiyama. Watu hao huwa wanasema: Sisi tunatoweka kwa kufikwa na mauti; na hakuna kitu chochote kitokanacho na sisi ambacho kinasalia, hata tuje kuwa hai tena na kutakiwa kuwajibika kwa amali tulizofanya. Kuna siku tumekuja hapa duniani na kuna siku tutaondoka; na ghairi ya ulimwengu huu tunaoishi ndani yake, hakuna ulimwengu mwingine wowote hata tukae na kuufikiria. Kukanusha kwao Maadi na kufufuliwa viumbe hakutegemei hoja na burhani bali kumesimamia kauli za dhana na kukisia tu. Wao huwaelekea waumini na kuwaambia, kama kufufuliwa tena wafu ni tukio la kweli, wafufueni baba zetu kwanza papa hapa duniani ndipo tuamini kuwa upo uwezekano wa sisi kufufuka tena. Hali ya kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ameonyesha kwa njia tofauti ikiwemo ya uumbaji wa mwanadamu wa mwanzo, uwezo wake wa kuwafufua wafu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kufuata matamanio ya nafsi humfanya mtu akanushe Kiyama ili kwa njia hiyo aweze kukidhi matashi yake kwa raha na buraha na kuendelea kufanya maovu na madhambi bila hofu wala wasiwasi wowote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wanaokanusha maadi hawana hoja yoyote ya maana isipokuwa kulikadhibisha hilo kwa kutegemea dhana tu. Aidha, aya hizi zinatuelimisha kwamba, kama walivyokuwa wakanushaji wa kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, ambao walikuwa wakisema, lazima tumuone Mungu kwa macho yetu ndipo tutaamini, baadhi ya wakanushaji Kiyama na kufufuliwa viumbe, nao pia wanasema: inabidi tuwaone baba zetu kwanza wakifufuliwa ndipo tutaamini. Utadhani ukomo wa akili zao ni macho yao; na kwa hivyo chochote wasichoweza kukiona kwa macho hawako tayari kukiamini. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 918 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/