Sura ya Al-Jaathiya, aya ya 33-37 (Darsa ya 920)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 920 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 45 ya Al-Jaathiya. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 33 ya sura hiyo ambayo inasema:
وَبَدَا لَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا عَمِلُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ
Basi ubaya wa waliyo yatenda utawadhihirikia, na yatawazunguka waliyo yafanyia stihzai.
Katika darsa iliyopita tulinakili maneno ya wakanushaji wa Kiyama na kufufuliwa viumbe waliokuwa wakisema kwa kejeli na stihzai: Sisi hatujui Kiyama ni nini na hatudhani kama kitatokea. Aya tuliyosoma inatoa jibu kwa watu hao kwa kuwaambia: Itakapowadia Siku ya Kiyama, watakabidhiwa madaftari ya amali zao na watayaona yote waliyokuwa wakiyafanya yamesajiliwa ndani yake na hakuna kitakachoweza kukanushwa. Wakati huo, itakapowadhihirikia mbele yao sura halisi ya matendo yao maovu, ndipo watakapotambua kwamba yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha na stihzai yamewazonga na kuwazunguka na hawana njia ya kukimbilia na kuokoka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Kiyama, ni siku ya kudhihiri na kuonekana amali za mtu na matokeo na athari zake zilizokuwa zimefichikana. Aya hii inatutaka pia tujihadhari na kuzifanyia shere na stihzai hukumu na mafundisho ya dini, kwani iko siku yatakuja kutuandama madhara ya mwenendo huo.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 34 ya sura yetu ya al Jaathiya ambayo inasema:
وَقِيلَ الْيَوْمَ نَنسَاكُمْ كَمَا نَسِيتُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَٰذَا وَمَأْوَاكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُم مِّن نَّاصِرِينَ
Na itasemwa: Leo tunakusahauni kama nyinyi mlivyo sahau mkutano wa siku yenu hii; na mahali penu ni Motoni, wala hamna wa kukunusuruni.
Katika misamiati ya Qur’ani, ikiwa kusahau kutamtokezea mtu kimaumbile, hatosailiwa kwa hilo, kwa sababu baadhi ya mambo huwa mtu anayasahau bila kukusudia. Ni kama inapotokezea mtu akasahau kusali. Lakini kama usahaulifu wa mtu utakuwa ni wa namna ya kudharau na kutojali hukumu za Mwenyezi Mungu, huo utamfanya aadhibiwe, kwa sababu hakika yake si kusahau bali ni kujisahaulisha. Kuna baadhi ya watu wanakanusha Kiyama na wanashikilia kwa ndimi zao ukadhibishaji wao huo. Na kuna baadhi ya watu hawako hivyo, lakini matendo yao yanaonyesha kuwa hawajali chochote kuhusu Kiyama, kama kwamba wameamua kujisahaulisha juu ya jambo hilo. Makundi yote haya mawili yataadhibiwa kulingana na imani na matendo yao; na Mwenyezi Mungu Mtukufu ataamiliana nao watu hao kama kwamba amewasahau; na atawakosesha rehma zake zisizo na ukomo. Tab’an inapofika hadi Allah SWT, ambaye ni rahimu na mrehemevu, akamsahau mja wake na kumfungia kikamilifu mlango wa rehma zake, hilo ni jambo litakalompa mtu machungu na mateso yasiyohimilika. Kisha sehemu ya mwisho ya aya inaashiria kuwa, makazi ya watu hao yatakuwa ni motoni na hawatampata yeyote wa kuwanusuru na kuwasaidia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kila mtu ambaye anakisahau Kiyama kwa imani na mwenendo wake, siku kitakapodhihiri atafanywa kama mtu aliyesahauliwa; na Allah SWT atamwacha mtu huyo kama alivyo kwa kumfungia kikamilifu mlango wa rehma zake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, haitoshi kuamini tu kwamba kuna kufufuliwa. Mtu muumini anatakiwa akikumbuke Kiyama na maadi katika kila hali na mazingira anayokuwa.
Ifuatayo sasa ni aya ya 35 ambayo inasema:
ذَٰلِكُم بِأَنَّكُمُ اتَّخَذْتُمْ آيَاتِ اللَّهِ هُزُوًا وَغَرَّتْكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا ۚ فَالْيَوْمَ لَا يُخْرَجُونَ مِنْهَا وَلَا هُمْ يُسْتَعْتَبُونَ
Hayo ni kwa sababu nyinyi mlizifanyia mzaha Aya za Mwenyezi Mungu; na maisha ya dunia yakakudanganyeni. Basi leo hawatatolewa humo wala hao hawatakubaliwa udhuru wao.
Aya hii inaendeleza yale yaliyobainishwa katika aya iliyotangulia kwa kueleza kwamba chanzo cha watu hao kuishia motoni ni mambo mawili: la kwanza ni kuhadaiwa na kutekwa na maisha ya dunia na jengine ni kuzifanya shere na stihzai aya ya Mwenyezi Mungu. Ukweli ni kwamba kuikumbatia dunia kupindukia humfanya mtu ayakanushe maisha ya baada ya kifo na mahakama ya Siku ya Kiyama, ili aweze kujistarehesha na kukidhi hawaa na matamanio ya nafsi yake bila kuwa na hofu wala wasiwasi wa jambo lolote. Watu hao wakutanapo na wenzao wanaowapa indhari kuhusu adhabu ya Moto, huwa wanasema kwa kejeli: nani aliyekuja na habari za ulimwengu huo hata mnatutisha na kutuhofisha sisi? Pepo gani hiyo au Moto gani huo? Hizo ni ahadi hewa tu mnazopewa. Chukua kilichopo mbele ya macho yako na achana na kitu cha ahadi tupu! Ni wazi kwamba watu kama hawa wenye fikra za aina hii, hawana nia ya kutubia na kuomba maghufira, bali huondoka duniani katika hali hiihii. Siku ya Kiyama hawatapata njia ya kuwaokoa na moto, wala udhuru wa kutoa ukaweza kukubaliwa na kuwanusuru na adhabu ya Jahannamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuhadaiwa na dunia pamoja na mali, madaraka na raha zake ndio chanzo cha kumfanya mtu awe na mwisho mbaya huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Mwenyezi Mungu ametimiza dhima kwa waja wake wote. Na kwa hivyo mtu hatokuja kuwa na kisingizio au udhuru wa kutoa Siku ya Kiyama kwa kudai kwamba: Nilikuwa sijui.
Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 36 na 37 ambazo zinasema:
فَلِلَّهِ الْحَمْدُ رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَرَبِّ الْأَرْضِ رَبِّ الْعَالَمِينَ
Basi sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa mbingu, na Mola Mlezi wa ardhi, na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ
Na ukubwa ni wake Yeye tu, mbinguni na katika ardhi, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Aya hizi ambazo ndizo aya za mwisho za Suratul-Jaathiya zinazungumzia nafasi ya Allah SWT katika ulimwengu wa maumbile na kubainisha kwamba: tadbiri na uendeshaji wa mambo yote ya ulimwengu wa angani, wa mbingu zenye adhama na mifumo ya sayari, nyota na maumbo ya ulimwengu huo yasiyohesabika, vyote hivyo viko kwenye mamlaka ya Mwenyezi Mungu; kama ambavyo uendeshaji na usimamiaji wa masuala yote ya ardhini na vyote vilivyomo ndani yake-ambavyo ni haba mno vikilinganishwa na mfumo mzima wenye adhama wa uumbaji- unafanywa pia na Yeye Allah SWT. Yeye Mola Muumba, anauendesha mfumo mzima wa ulimwengu wa maumbile kwa uwezo wake usio na kikomo na usioshindika; na kwa ujuzi na hekima thabiti isiyomithilishika. Kwa hivyo ni wajibu wetu sisi wanadamu kuwa na utambuzi sahihi kuhusu Allah SWT na hadhi na nafasi yake katika ulimwengu wa maumbile; na ni wazi kuwa utambuzi na uelewa huo utatufanya tumhimidi, tumshukuru na kumtukuza Yeye Mola. Kwa sababu kheri na baraka zote zinatokana na dhati yake iliyotakasika; na hamdu na shukurani zote zinamstahikia Yeye. Katika aya ya mwisho ya Suratul-Jaathiya imeashiriwa kwamba, athari za adhama ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ziko wazi kabisa mbinguni kote na katika ardhi yote; na adhama na utukufu wa mbingu na ardhi ni vyake Yeye peke yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mfumo mzima wa ulimwengu wa maumbile unaendeshwa na Mungu Mmoja na wa pekee; na hakuna tofauti yoyote katika suala hilo kati ya mbingu na ardhi au viumbe na vitu mbalimbali. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, nguvu, qudra na uwezo huwa na maana vinapotumiwa kwa ujuzi na hekima. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, kumwabudu Mwenyezi Mungu kunafungamana na maarifa na elimu sahihi ya kumtambua Yeye; na ni Yeye tu Allah SWT ndiye anayestahiki kutukuzwa, kuhimidiwa na kushukuriwa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 920 ya Qur’ani imefikia tamati. Na ndiyo darsa ya mwisho ya sura ya 45 ya Al-Jaathiya. In shaa Allah tuwe tumeelimika, tumeaidhika na kunufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba pia Allah atuzidishie elimu na ufahamu sahihi wa kumjua Yeye na adhama yake, utakaozidisha na kuzifanya thabiti zaidi imani zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/