May 27, 2023 05:50 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 944. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 48 ya al Fat-h, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 49 ya al-H'ujuraat. Sura hii iliteremshwa Madina, ina aya 18 na inazungumzia misingi muhimu ya adabu na akhlaqi za kijamii. Misingi ambayo inapochungwa na kufanyiwa kazi huimarisha upendo, udugu na urafiki baina ya watu katika jamii; na isipochungwa na kutekelezwa husababisha chuki na uadui, mifarakano na kila mtu kumshuku na kumtizama mwenzake katika jamii kwa jicho baya. Kwa sababu hiyo, tunaweza kuipa sura hii ya al-H'ujuraat jina la sura ya akhlaqi na adabu za Kiislamu. Baada ya utangulizi huo mfupi tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya ya kwanza ya sura hiyo ambayo inasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

Enyi mlio amini! Msimtangulie (katika lolote) Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mjuzi.

Sura hii imewahutubu waumini kwa kuwaambia: sifa ya imani ya kweli ni kujisalimisha na kutii maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kutowatangulia wao katika lolote, hasa katika masuala ya kijamii, ambapo watu wote wanapaswa wamtii kiongozi wa jamii ya Kiislamu; kwani kumtangulia yeye kwa namna yoyote ile hupelekea kuvurugika mfumo na nidhamu ya jamii na kuzuka mfarakano na mgawanyiko baina ya watu. Baadhi ya Waislamu wenye misimamo ya kufurutu mpaka huwa wanatarajia kiongozi wa jamii ya Kiislamu afanye mambo kwa kufuata utashi, mitazamo na itikadi waliyonayo wao, au achukue hatua kali dhidi ya baadhi ya makundi na watu, au hata aache kabisa kufanya baadhi ya mambo. Hali ya kuwa, yeye kama kiongozi, huwa anachukua maamuzi kulingana na utambuzi halisi alionao juu ya hali na mazingira ya jamii na kwa kuzingatia maslaha ya jamii yenyewe; na kwa hivyo haingepasa kumtarajia afanye vingine ghairi ya hivyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuharamisha baadhi ya mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyahalalisha, au kuhalalisha baadhi ya mambo ambayo Yeye Mola ameyaharamisha, ni namna mojawapo ya kumtangulia Allah SWT na Mtume wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, sheria na kanuni za jamii ya Kiislamu inapasa zitokane na Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Sunna za Bwana Mtume SAW; na utungaji wowote ule wa sheria unaopingana na Qur'ani na Sunna, una maana ya kumtangulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Halikadhalika aya hii inatuelimsha kwamba, watu wanaoitangulia hukumu ya Allah na Mtume wake kwa sababu ya kufuata matashi ya binafsi au mila na desturi za kijamii, huwa kwa hakika wamejiweka mbali na imani na uchaMungu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya pili na ya tatu ambazo zinasema:

‏ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ أَن تَحْبَطَ أَعْمَالُكُمْ وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ

Enyi mlio amini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa sauti kubwa kama mnavyo semezana nyinyi kwa nyinyi, zisije amali zenu zikaharibika, na hali hamtambui.

إِنَّ الَّذِينَ يَغُضُّونَ أَصْوَاتَهُمْ عِندَ رَسُولِ اللَّهِ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ امْتَحَنَ اللَّهُ قُلُوبَهُمْ لِلتَّقْوَىٰ ۚ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ عَظِيمٌ

Kwa hakika wanao teremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao ndio Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa uchamngu. Hao watakuwa na maghufira na ujira mkubwa.

Baada ya aya iliyotangulia kueleza kwamba, Waislamu wasimtangulie Bwana Mtume SAW katika ufanyaji mambo, wala wasichukue hatua ya kufanya lolote kabla ya yeye kutangaza uamuzi juu ya jambo hilo, aya tulizosoma zinasema: msimtangulie Mtume hata katika maongezi na msiinue sauti zenu kuipita sauti yake; na pale mnapokuwa na yeye msipaze sauti wala kupiga makelele. Kwa maelezo ya aya hizi inaonyesha kwamba, baadhi ya Waislamu walikuwa hawachungi murua na adabu za kijamii. Waislamu hao walikuwa wakizungumza na Bwana Mtume bila kuchunga murua na adabu na kwa sauti ya juu kama walivyokuwa wakifanya hivyo wanapoongea na watu wa kawaida, mpaka ikafika hadi Mwenyezi Mungu akawaonya na kuwapa indhari kwamba, tabia na mlahaka wa aina hiyo usio wa adabu na heshima utaporomosha na kuharibu amali zenu bila ya nyinyi wenyewe kujua. Kisha sehemu inayofuatia ya aya inatanabahisha juu ya nukta kwamba, sharti la taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu ni kuchunga adabu na murua mnapokuwa mbele ya Mtume wa Allah na kushusha sauti wakati mnapozungumza mbele ya hadhara ya Nabii huyo mteule wa Mwenyezi Mungu, ambapo kufanya hivyo kutakuwa sababu ya kupata rehma na fadhila zake Mola duniani na akhera. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tujihadhari na kauli zetu, kwa sababu mambo tunayoyafanya, mazuri au mabaya yana athari za kimaisha; na taathira na matokeo ya mambo tunayofanya hayategemei kama tumeyatenda kwa kujua au kwa kutojua. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wanaweza wakawepo watu wengi ambao wanajionyesha mbele ya macho kuwa na adabu, tawaadhui na unyenyekevu, lakini ndani ya nafsi zao wamejawa na kiburi. Kwa maneno mengine ni kwamba, kuchunga heshima na adabu na kuonyesha unyenyekevu huwa na thamani pale kunapofanywa kwa taqwa, ukweli na moyo safi; vinginevyo huwa ni aina mojawapo ya kujipendekeza tu na kujaribu kumhadaa mtu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kuwa na imani na uchaMungu maana yake si mtu kutakasika na kuwa na kinga ya maasi. Kuna watu waumini na wachamungu pia ambao huteleza na kufanya dhambi, lakini hutambua makosa yao haraka wakayafidia kwa kutubia kwa Allah.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya nne na ya tano ya sura yetu ya H'ujuraat ambazo zinasema:

إِنَّ الَّذِينَ يُنَادُونَكَ مِن وَرَاءِ الْحُجُرَاتِ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ

Hakika hao wanao kuita nyuma ya vyumba, wengi wao hawafahamu. 

وَلَوْ أَنَّهُمْ صَبَرُوا حَتَّىٰ تَخْرُجَ إِلَيْهِمْ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ ۚ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Na lau wao wangeli ngojea mpaka uwatokee ingeli kuwa kheri kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, Mwenye kurehemu. 

Aya hizi zinaashiria mfano mmoja hai wa yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia na kueleza kwamba: wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipokuwa nyumbani kwake pamoja na ahli zake akiwa anashughulika na mambo ya familia au amejipumzikia, baadhi ya mabedui wa majangwani wasio na ustaarabu, walikuwa hawasubiri mpaka Mtume atoke nyumbani kwake ili nao wapate kumweleza matilaba yao. Walikuwa hukohuko nje walikokuwa, wakimwita mtukufu huyo kwa sauti kubwa na kueleza wanayoyataka. Qur'ani tukufu ikawahutubu watu hao kwa kuwaambia: hili mlifanyalo ni ishara ya kukosa busara, kwani alama muhimu zaidi ya akili na busara ni kuchunga adabu na heshima katika mahusiano ya kijamii na wakati mtu anapokutana na watu watukufu wanaoheshimika katika jamii. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, Uislamu unazipa umuhimu maalumu adabu za kijamii mpaka kufika hadi ya kuutaja utovu wa adabu na murua kuwa ni ishara na alama ya kukosa busara. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, nyumba na familia zina faragha na heshima yake; na hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuwasumbua watu na familia zao majumbani mwao hata kwa kuwaita kutokea nje ya nyumba zao. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, majukumu na masuulia ya kijamii ya watu hayapasi kuwa kizuizi kwa wao kushughulikia masuala ya familia zao. Vilevile aya hizi zinatutaka tuheshimu ratiba na nyakati za faragha za watu na kutowasumbua kwa kuwaendea wakati usiofaa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 944 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa Waislamu wa kweli wanaochunga heshima, adabu na murua katika miamala ya kijamii wakati tunapolahikiana na Waislamu wenzetu na watu wengine pia miongoni mwa wanadamu wenzetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/