May 28, 2023 07:57 UTC
  • Kombora la Kheibar
    Kombora la Kheibar

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Iran imefanikiwa kurusha kombora lake la teknolojia ya juu zaidi la aina ya Khorramshahr liitwalo Kheibar ambalo ni kombora la masafa ya kati linaloongozwa kwa usahihi na linaweza kubeba vichwa vya kivita vya kilo 1,500.

Kombora la Khoramshahr 4 lilizinduliwa Mei 25 mbele ya Waziri wa Ulinzi Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 41 ya ukombozi wa mji wa kusini magharibi wa Khorramshahr.

Waziri wa Ulinzi wa Iran ameutaja ujumbe wa kuzindua kombora hilo kuwa ni kwa ajili ya kusaidia amani na utulivu katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Kombora hilo lilizinduliwa rasmi kama bidhaa mpya kabisa ya makombora yaliyoundwa na sekta ya  viwanda vya anga ya Wizara ya Ulinzi ya Iran. 

 Waziri wa Ulinzi wa Iran alisema katika hafla ya kuzindua kombora la kistratejia la masafa marefu la Khorramshahr 4 kwamba: "Ujumbe wa hatua hii kwa marafiki zetu ni kusaidia kuimarisha amani na utulivu katika kanda hii na kuziunga mkono kwa pande zote nchi rafiki ambazo zinapambana na mfumo wa ubeberu. 

Waziri wa Ulinzi wa Iran Muhammad Reza Ashtiani ameongeza kusema: Ujumbe wa Wizara ya Ulinzi ya Iran kwa maadui ni kwamba, tumeazimia kuilinda nchi na mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu, na tumemdhihirishia adui kwamba hawezi kuwazuia na kuwawekea vizuizi vijana wetu katika njia ya maendeleo na ustawi. 

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani amesema, Iran itaendelea kuzindua mafanikio yake ya kiulinzi katika nyuga mbalimbali katika siku zijazo.

Kombora la Khaiber linaloendeshwa kwa kioevu, ni toleo jipya zaidi katika kizazi cha kombora la Khorramshahr, na lina uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 2000 mbali na kubeba kichwa chenye uzito wa kilo 1500.

Katika uzinduzi wa kombora hilo, Waziri wa Ulinzi alitangaza mipango ya kurusha satelaiti mbili zaidi katika anga za mbali katika miezi ijayo, huku Iran ikiendelea na juhudi za kukuza tasnia yake ya anga.

Aidha alisema mipango ya makombora na anga za mbali ya Jamhuri ya Kiislamu lazima isonge mbele "bila kusimama."

Amesema Iran ni miongoni mwa nchi chache zinazoongoza duniani katika sekta ya anga za mbali hususan katika masuala ya kurusha satelaiti.

@@@

Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Ushirikiano wa Kisayansi cha Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia ya Iran ametangaza kuwa, Iran na Saudi Arabia zinataka kuendeleza ushirikiano wa kisayansi

Balozi za Iran na Saudi Arabia zitafunguliwa tena hivi karibuni kufuatia makubaliano ya Saudia na Iran ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia ambayo yalifikiwa mnamo Machi 10, 2023, huko Beijing.

Mkuu wa Kituo cha Ushirikiano wa Kimataifa wa Kisayansi cha Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia, Vahid Haddadi-Asl amesema: "Mara tu baada ya balozi wa Iran kuanza kazi Saudi Arabia, Wizara ya Sayansi ya Iran itakuwa idara ya kwanza kuanzisha uhusiano mpya wa kisayansi na Saudi Arabia."

Ameashiria umuhimu wa maendeleo ya maingiliano ya kisayansi ya Iran na Saudi Arabia hasa katika sekta za masuala ya mafuta, maji na mazingira.

Aidha amesema maendeleo ya ushirikiano wa kisayansi na nchi jirani zikiwemo, Uzbekistan, Tajikistan, Kyrgyzstan, na Kazakhstan pia yako kwenye ajenda ya Wizara ya Sayansi.

@@@

Kuanzia mwezi Mei, abiria nchini China wataweza kulipia tiketi ya treni ya chini ya ardhi (Metro) kwenye mojawapo ya njia za usafiri huo mjini Beijing kwa kuskani kiganja cha mkono tu.

Kampuni ya Metro ya mji wa Beijing imetangaza kuwa imeanza kutoa huduma maalumu kwa abiria wake ya kuskani kwa muda mchache mno kupitia kiganja cha mkono ili kulipia nauli ya treni ya chini ya ardhi.

Gazeti la Beijing limeandika kuhusiana na suala hilo kwamba: huduma ya kuskani haraka kiganja cha mkono ni mwafaka zaidi kwa watu walio wazee kiumri, wale wenye matatizo ya kimwili, abiria waliosahau kadi zao za Metro au wale ambao hawawezi kutumia simu za mkononi, ambapo wote hao wanaweza kulipia nauli ya usafiri huo kwa njia hiyo.

Huduma za malipo kwa njia ya kuskani kiganja cha mkono zimepangwa kutolewa katika ofisi, maskuli, kumbi za michezo na mikahawa kwenye maeneo mbalimbali ya China.

Kwa msaada wa teknolojia za kisasa, China inaendelea kila uchao kuboresha utoaji wa huduma katika vituo na maeneo ya umma.

Katika mwendelezo wa utoaji huduma hizo, mnamo mwaka uliopita baadhi ya njia za metro katika mji wa Shenzhen zilizindua mashine za kuskani sura ya mtu kwa ajili ya kulipia nauli ya metro; na mwaka huu, treni ya chini ya ardhi ya Beijing imezindua huduma hiyo kwa kutumia mfumo wa kuskani kiganja cha mkono.

@@@

 

Mchango mpya wa kifedha kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu UNITAID utaongeza kwa asilimia 20 ufadhili wa, miradi ya kuchukua hatua za kupunguza madhara katika nchi 10 duniani.

Mtazamo wa mpango huo unajikita kwa watu wanaojidunga dawa za kulevya katika nchi zenye uchumi wa chini na kati na bidhaa mbili za kuzuia hali hiyo zitajaribiwa ili kupunguza hatari katika idadi hii ya watu.

UNITAID imetangaza kuwekeza fecha hizo ambazo ni jumla ya dola milioni 31 kwa ajili ya mipango ya kupunguza hatari ikilenga zaidi kuzuia homa ya ini aina ya C au Hepatitis C kwa wanaojidunga dawa za kulevya kwenye nchi za kipato cha chini na cha kati.

Ufadhili huo wa UNITAID utasaidia kujumuisha pia huduma za upimaji wa VVU na matibabu na programu za kupunguza madhara.

Tangazo hilo limetolewa wakati wa kongamano la 27 la kupunguza madhara, linalofanyika huko Melbourne, Australia.

Kwa kuongezea UNITAID imesema, rasilimali hii itatumika kufanyia majaribio bidhaa mbili za kuzuia ambazo mosi ni sindano za ujazo wa chini na pili mchanganyiko wa kutolewa polepole dawa ya buprenorphine ambayo hutumiwa kutibu uraibu wa opioid au afyuni.

Homa ya ini aina C ni ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya damu na ukiachwa bila kutibiwa, unaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa ini na hata saratani.

Maendeleo ya hivi karibuni yamesaidia matibabu madhubuti kupatikana katika nchi nyingi za kipato cha chini na cha kati, ambako asilimia 80 ya watu walio na ugonjwa huu wanaishi.

Kulingana na UNITAID, makundi yaliyotengwa yameathirika kwa kiasi kikubwa kwani watu 4 kati ya 10 wanaojidunga dawa wana maambukizi ya homa ya ini. Katika hali ya watu walionyimwa uhuru, kiwango ni mtu 1 kati ya 4. Watu hawa hawana huduma ya kutosha.

Kwa uwekezaji huo mpya, shirika hilo linanuia kufikia makundi haya yaliyotengwa, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za homa ya ini katika programu za kupunguza madhara na teknolojia za kupima ambazo zinaweza kupunguza hatari zinazohusiana na kujidunga dawa za kulevya.

Shirika hilo limesema sindano zenye ujazo wa chini zilizokufa zina hifadhi ndogo ambapo damu inaweza kubaki baada ya matumizi.

Kipimo kinapunguza hatari ya maambukizo yatokanayo na damu wakati sindano inatumiwa na watu wengi.

Michanganyiko inayotolewa polepole ya buprenorphine, dawa ambayo hupunguza hamu ya kutumia opioid na kujiondoa kwenye matumizi, inaweza kuwa chaguo kwa watu wengi, haswa wale ambao wanakabiliwa na changamoto na kipimo cha kila siku cha njia ya mdomo, kama vile gharama kubwa, unyanyasaji wa polisi au ubaguzi.

Bidhaa zote mbili zitajaribiwa katika maeneo ya Misri, India, Kyrgyzstan, Nigeria, Afrika Kusini, Tanzania, Ukraine na Vietnam.

@@@

Na Tanzania  ndiyo nchi kinara katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa na idadi kubwa ya magari yanayotumia umeme.

Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania, limeanzisha vituo vya kuchaji magari yatumiayo umeme Dodoma ili kuchochea zaidi mfumo huo.

Mtaalamu wa miradi wa UNDP Tanzania, Abbas Kitogo anasema data zilizopo zinaonyesha kuwa Tanzania inaongoza Afrika Mashariki katika matumizi ya magari na bajaji zinazotumia umeme, lakini kuna changamoto nyingi za kisera, kiteknolojia, kiuwekezaji, miundombinu na uelewa mdogo.

Kitogo anasema kwa sasa mradi huo upo katika hatua ya majaribio na hawafanyi biashara, bali kuhamasisha matumizi ya magari ya umeme.

Anasema kupitia kituo hicho, wawekezaji na wajasiriamali watajifunza na kupata uzoefu.

“Tumewekeza kwenye mradi huu kuhamasisha matumizi ya teknolojia nchini, ikiwamo kwa wawekezaji na wajasiriamali kujifunza na kupata uelewa.

“UNDP itaendelea kuwekeza katika kujenga uelewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwamo sekta binafsi,” anasema Kitongo.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Tanzania, Felchesmi Mramba alinukuliwa na gazeti la The Citizen akisema Serikali inafanya juhudi zote zinazowezekana kuvutia uwekezaji katika vyombo vya moto vitumiavyo umeme, lakini upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo muhimu ni mdogo.

Anasema kwa sasa serikali ipo katika mpango wa kuandaa mkakati kwa ajili ya matumizi ya nishati safi katika vyombo vya moto.

@@@

Naam na hadi hapo.

 

 

 

Tags